Lindi. Katika Kijiji cha Mandwanga, kilichopo Kata ya Mandwanga, Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi, maisha ya Mzee Abdulrahman Suleiman Kassim yalikuwa yakining’inia kati ya matumaini na majaribu ya kiafya.
Kabla ya kupata kadi ya Bima ya Afya kwa Wote, dawa yake kubwa ilikuwa mwarobaini. Katika mahojiano, anasimulia kwa sauti tulivu, lakini yenye maumivu ya muda mrefu:
“Siku moja mwanangu aliumwa. Sina hela ya kwenda hospitali, sina hata ya bodaboda kutoka hapa Mandwanga hadi kituo cha afya kilichopo kijiji jirani. Duka la dawa wakasema lazima apimwe kwanza. Nikarudi nyumbani nikatafuta mti wa mwarobaini,” amesimulia.
Walijifukiza pamoja. Baadaye akamwambia anywe kidogo dawa hiyo ya asili. Kisha akachukua shuka lake na kwenda kumkanda chooni, akitumaini maumivu yangepungua.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mandwanga namna sahihi ya matumizi ya kadi hizo.
Hayo ndiyo yalikuwa mazingira yake—maisha ya kuomba Mungu na kutegemea mitishamba pale fedha zinapokosekana.
“Kama huna hela, kwenye vituo vyetu vya afya ni changamoto. Unafika kwenye foleni, lakini mwenye fedha anahudumiwa kwanza. Wewe unaambiwa dawa hakuna, nenda kanunue dukani. Wakati huo hata nauli umekopa,” amesimulia Mzee huyo mwenye zaidi ya miaka 59, akilea watoto wanaomtegemea.
Wakati mwingine, amesema, wanarudi nyumbani mikono mitupu. Wanachukua mitishamba, wanapondaponda na kunywa. “Mungu akitaka unapona, kama wa kupotea, unapotea.”
Maumivu yake yanachangiwa na kumbukumbu ya bima ya zamani ya CHF. Anasema waliwahi kukatwa Sh30,000 kwa kila mtu. Kwa familia ya watu watano, ilifikia Sh150,000 kiasi kikubwa kwa mkulima wa kipato cha chini. Lakini miezi michache baadaye waliambiwa kadi zimekwisha muda.
“Kilichoniuma zaidi, kadi ile sikuitumia hata mara nyingi. Ukienda unaambiwa imekwisha. Lakini ukitoa hela, inafanya kazi,” anasema kwa uchungu.
Ndiyo maana alipopokea kadi mpya ya Bima ya Afya kwa Wote, kupitia mpango wa kaya masikini Tasaf, hakuficha shukrani zake kwa Rais Samia Suluhu Hassan na uongozi wa wilaya. Hata hivyo, anaomba usimamizi uwe wa karibu:
“Isiishie njiani tena. Ifanye kazi kweli.”
Si yeye pekee aliyepitia hali hiyo. Mkazi mwingine wa Mandwanga, Hamisi Mkuva, anakumbuka siku mtoto wake alipojikata kwa upanga. Walimuwahisha zahanati ya kijiji jirani, wakaambiwa matibabu yana gharama. Wakarejea kijijini kuomba msaada kwa majirani. Harambee ndiyo iliyookoa maisha ya mtoto.
“Zamani mpaka ukalime kibarua ndipo upate fedha ya matibabu. Sasa naamini bima hii itatusaidia wakati wa dharura,” amesema Mkuva, baba wa watoto wawili.
Mkewe, Salima Machemba, anakiri kuwa mara nyingi walikuwa wakijitibu kwa mitishamba au kulazimika kulima vibarua kwanza kabla ya kwenda zahanati. “Sasa tunashukuru, watoto wakiumwa tutakuwa na uhakika wa matibabu.”
Kwa Bibi Mwajawa Juma, changamoto ilikuwa mjukuu mwenye ngiri. Kila walipoenda hospitali waliambiwa gharama ya upasuaji ni takribani Sh3 milioni, fedha ambayo hakuwa nayo. Mara nyingi walipewa dawa za maumivu tu, hivyo asilimia kubwa walienda kwenye tiba za jadi na mitishamba.
“Sasa naamini mjukuu wangu atafanyiwa upasuaji,” anasema kwa matumaini mapya.
Kwa mujibu wa Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, NHIF Mkoa wa Lindi, Janeth Kibambo, Serikali imetenga zaidi ya Sh48 bilioni kwa ajili ya kuanza na kaya zenye kipato cha chini, hasa wanufaika wa Tasaf, katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Amesema wameanza uandikishaji Februari 2 na zaidi ya asilimia 30 ya walengwa wameshasajiliwa. Awamu ya kwanza ni jumla ya wanufaika 20,086 sawa na kaya 4,164. Tumekamilisha usajili wa Lindi Mjini, vijijini, Liwale, Kilwa na kuanzia wiki ijayo tunaendelea Wilaya ya Nachingwea na Ruangwa.
Amesema huduma za bima kwa wote zinapatikana kuanzia ngazi ya msingi hadi rufaa, ikiwemo hospitali za juu kama Hospitali ya Taifa Muhimbili, kwa kufuata utaratibu uliowekwa.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, amewahakikishia wananchi kuwa huduma zaidi ya 370 na dawa zaidi ya 270 zitapatikana, huku mafunzo maalum yakitolewa kwa wahudumu na ukaguzi wa mara kwa mara kufanyika ili kuondoa kasoro zilizojitokeza hapo awali.
Mwanziva amesema ugawaji wa kadi hizo ni awamu ya kwanza kwa wale walengwa wanaotoka kaya zisizojiweza, ambao wamebainika kupitia Tasaf, wameandikishwa, kuchukuliwa taarifa zao, na leo wamekabidhiwa kadi hizo zitakazowawezesha. Zaidi ya kaya 4,000 zipo katika mchakato huo.
Amesema Manispaa ya Lindi zaidi ya kaya 3,900 zimeshaandikishwa na mteja wa kwanza ameshapata huduma. Rais aliahidi siku 100 za kwanza na ametekeleza.
“Awamu zijazo, tunaendelea na makundi mengine, tutajitahidi kuendelea kuisimamia,” amesema.
Hata hivyo, mamlaka zimetahadharisha kuwa kadi si ya kukopeshana. Atakayebainika kuitumia kinyume cha utaratibu atachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi bado wanauliza kwa tahadhari: Je, mfumo huu mpya utabeba matarajio yao? Je, hautakumbwa na changamoto zilezile za dawa kukosekana au kadi kukatishwa ghafla?
Kwa sasa, Mzee Abdulrahman anashikilia kadi yake kwa makini. Watoto wake wengine bado wanaandikishwa, picha zikichukuliwa na taarifa kurekodiwa. Anaamini safari hii mambo yatakuwa tofauti.
“Kama huna hela, matibabu ni shida. Sasa tumepewa bima, ni matumaini yetu itatusaidia sisi wa kipato cha chini.”
Kutoka kwenye mwarobaini wa kujifukiza hadi kadi ya bima mkononi, safari ya Mzee Kassim na wenzake Mandwanga ni hadithi ya matumaini yanayochanganyika na tahadhari, wakisubiri kuona kama ahadi ya Bima ya Afya kwa Wote itageuka kuwa tiba ya kweli, au itabaki kuwa matumaini mengine yaliyosubiriwa kwa muda mrefu.