Dar es Salaam. Katika kalenda za dini mbili kubwa duniani Uislamu na Ukristo, kuna vipindi maalumu vya waumini kujizua kula na kunywa vinavyojulikana kwa majina tofauti lakini vyenye lengo linalofanana.

Ni lengo la kumkaribia Mwenyezi Mungu kwa nidhamu, toba na utakaso wa nafsi. Kwa Waislamu ni Mwezi wa Ramadhani, na kwa Wakristo ni kipindi cha Kwaresma. Ingawa msingi wake ni wa kiroho, wataalamu wa afya wanaeleza kuwa funga hizi pia zina manufaa makubwa kwa mwili wa mwanadamu.

Je, Ramadhani na Kwaresma zina uhusiano gani na afya? Je, dini hizi zinazungumziaje mwili katika ibada ya funga? Na sayansi inasemaje kuhusu kujinyima chakula kwa muda maalumu? Haya ndio maswali yatakayojibiwa na makala haya.

Saumu ya Ramadhan, nidhamu na uchamunu

Kwa Waislamu, Ramadhani ni mwezi mtukufu uliotajwa katika Qur’ani Tukufu:

“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa saumu kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kuwa wachamungu.” (Al-Baqarah: 183)

Saumu ya Ramadhani ni nguzo ya nne ya Uislamu. Katika mwezi huu, Waislamu hufunga kuanzia alfajiri hadi machweo ya jua, wakijizuia kula, kunywa na matamanio mengine ya kimwili. Lakini kama wanazuoni wanavyofafanua, lengo si mtu kushinda na  njaa wala kiu, bali ni kujenga taqwa yaani ucha-Mungu unaoathiri mwenendo wa maisha.

Mtume Muhammad (Rehema na amani ziwe juu yake) amesema katika hadithi iliyopokelewa na Sahih al-Bukhari: “Saumu ni ngao.”

Wanazuoni wa Kiislamu wanaeleza kuwa neno “ngao” hapa lina maana pana, likimaanisha kinga dhidi ya dhambi, lakini pia kinga dhidi ya madhara ya kiafya yanayotokana na ulaji usio na mipaka.

Imam Ghazali katika kitabu chake Ihya Ulum al-Din anaandika kuwa tumbo ni lango la matamanio mengi, na kulidhibiti ni hatua ya kwanza ya kuudhibiti mwili mzima.

Kwa mtazamo huu, saumu ni mazoezi ya kuutawala mwili badala ya mwili kumtawala mwanadamu.

Kisayansi, wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kufunga kwa muda maalumu kama ilivyo katika Ramadhani, hufanana na kile kinachojulikana kitaalamu kama “intermittent fasting.”

Aina hii ya funga kwa mujibu wa watafiti, inaweza kusaidia kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu, kupunguza uzito uliopitiliza,  kuboresha afya ya moyo na kurekebisha mifumo ya mmeng’enyo wa chakula

Dk Jason Fung, daktari na mtafiti wa lishe kutoka Canada, katika kitabu chake The Obesity Code anaeleza kuwa mwili unapokaa muda bila kula, huanza kutumia akiba ya mafuta kama chanzo cha nishati, hali inayosaidia kupunguza uzito na kuboresha usikivu wa homoni ya insulin.

Aidha, kazi za kitafiti za kisasa kuhusu mchakato unaoitwa “autophagy ambapo mwili huondoa seli zilizochoka na kuanza kujirekebisha, zinaonyesha kuwa kufunga kunaweza kuchochea mchakato huo. Mwanasayansi wa Kijapani,  Yoshinori Ohsumi alitunukiwa Tuzo ya Nobel mwaka 2016 kwa utafiti wake kuhusu autophagy, unaoonyesha namna mwili unavyojirekebisha pale unapokosa chakula kwa muda.

Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa manufaa haya hupatikana iwapo mfungaji atazingatia lishe bora wakati wa futari na daku, na kuepuka ulaji kupita kiasi.

Wakristo wanapochagua kujinyima vyakula fulani wanatekeleza kanuni zinazokubaliana na mapendekezo ya kitabibu.

Kwaresma: unyenyekevu na nidhamu ya mwili

Kwa Wakristo, Kwaresma ni kipindi cha siku 40 za maandalizi kuelekea Pasaka, kuadhimisha mateso na ufufuko wa Yesu Kristo.

Katika madhehebu mengi, waumini hujitolea kufunga au kujinyima baadhi ya vyakula au anasa kama ishara ya toba na unyenyekevu.

Biblia inazungumzia funga katika maeneo mbalimbali. Katika Injili ya Mathayo 6:16, Yesu anasema:

“Mnapofunga, msiwe na uso wa huzuni kama wanafiki…”

Hii inaonyesha kuwa funga ni tendo la ndani la ibada, si la maonesho. Aidha, Yesu mwenyewe alifunga siku 40 jangwani (Mathayo 4:2), tukio linaloipa Kwaresma msingi wake wa kiimani.

Katika Catechism of the Catholic Church, Kanisa Katoliki linaeleza kuwa funga ni njia ya “kutakasa moyo na kujiandaa kupokea neema ya Mungu.” Hapa tena tunaona muunganiko kati ya mwili na roho yaani kujinyima kwa mwili kama daraja la kuinua roho.

Faida za kiafya katika Kwaresma

Ingawa Kwaresma haina mfumo mmoja wa kufunga kama Ramadhani, waumini wengi hujinyima nyama, vyakula vizito au milo fulani.

Wataalamu wa lishe wanasema kuwa kupunguza ulaji wa nyama nyekundu na vyakula vyenye mafuta mengi kunaweza kusaidia kupunguza kiwango cha lehemu, kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na kuboresha mmeng’enyo wa chakula.

Kazi za kitafiti zilizochapishwa katika jarida la American Heart Association,  zinaonyesha kuwa lishe yenye mboga, matunda na nafaka zisizokobolewa hupunguza hatari ya shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Kwa hiyo, wakati Wakristo wanapochagua kujinyima vyakula fulani wakati wa Kwaresma, mara nyingi bila kutambua, wanatekeleza kanuni zinazokubaliana na mapendekezo ya kitabibu.

Wakristo wanapochagua kujinyima vyakula fulani wanatekeleza kanuni zinazokubaliana na mapendekezo ya kitabibu.

Faida za kiafya kwa jumla

Mbali na mwili, funga ina athari chanya kwa afya ya akili. Wanasaikolojia wanaeleza kuwa kujinyima kwa hiari huimarisha uwezo wa mtu kujidhibiti (self-control). Nidhamu hii huongeza kujiamini na kupunguza msongo wa mawazo.

Katika Ramadhani, maombi ya mara kwa mara, usomaji wa Qur’ani na ibada za usiku huongeza utulivu wa nafsi. Vivyo hivyo, katika Kwaresma, maombi, tafakari na toba huchangia ustawi wa kiroho na kisaikolojia.

Mtakatifu Augustine wa Hippo aliwahi kusema: “Mwili unapotawaliwa, roho huinuliwa.” Kauli hii inaendana na mtazamo wa Kiislamu kwamba nafsi inapodhibitiwa kupitia saumu, moyo hupata mwanga wa kiimani.

Tahadhari za kiafya

Wataalamu wanakubaliana kuwa funga inapaswa kufanywa kwa hekima. Watu wenye magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu au wajawazito wanapaswa kushauriana na madaktari kabla ya kufunga.

Katika Uislamu, Qur’ani inatoa ruhusa kwa wagonjwa na wasafiri kutofunga na kulipa baadaye (Al-Baqarah: 184–185). Hii inaonyesha kuwa afya ya mwili inalindwa hata ndani ya ibada.

Katika Ukristo pia, makanisa mengi huruhusu waumini wenye udhaifu wa kiafya kushiriki Kwaresma kwa namna nyingine kama sala na matendo ya huruma badala ya kufunga chakula.

Funga ni zawadi

Funga za Ramadhani na Kwaresma, licha ya tofauti za kimfumo, zina kiini kinachofanana: kumweka mwanadamu katika hali ya unyenyekevu mbele za Mungu na kumfundisha nidhamu ya mwili.

Kwa mtazamo wa dini, funga ni daraja la utakaso wa moyo. Kwa mtazamo wa sayansi, ni mfumo unaoweza kusaidia kurekebisha afya ya mwili.

Hivyo, katika makutano haya ya imani na utafiti wa kitabibu, tunaona ukweli mmoja: mwili na roho havipingani, bali vinakamilishana.

Iwapo itafanywa kwa uelewa, usawaziko na lishe bora, funga si tu ni ibada ya kiroho bali pia ni zawadi kwa afya ya mwanadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *