Arusha/Dar. Nani waliomteka na kwenda kumuua mfanyabiashara kikatili? Ndilo swali linagonga vichwa vya watu wengi jijini Arusha kufuatia kutekwa na kuuawa kwa mfanyabiashara wa madini, Abdilah Mussa (54) maarufu kama Banjoo.

Macho na masikio vinaelekezwa kwa Jeshi la Polisi ili liweze kutatua haraka kitendawili hicho cha utekaji na mauaji, lakini kamera za Usalama (CCTV) katika eneo alilotekwa mfanyabiashara hiyo, zimekuwa vigumu kupatikana.

Jengo la Ngorongoro linalomilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) alikotekewa mfanyabiashara huyo, lina CCTV tatu ambazo kwa namna na eneo zilipofungwa, watekaji wa Banjoo wangeweza kuonekana waziwazi.

Mbali na CCTV za jengo hilo, katika eneo linalozunguka jengo hilo kuna majengo mengine ya taasisi za umma na binafsi ambayo yana kamera, jambo ambalo wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema zinapaswa kuwa nyenzo muhimu ya kufanikisha haraka upelelezi.

Banjoo mkazi wa Sanawari Jijini Arusha anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana Februari 12, 2026 chini ya Jengo hilo la NCAA lenye ghorofa 10, alipokuwa akitoka katika ukumbi wa mazoezi (Gym) uliopo ndani ya jengo hilo.

Baada ya kuchukuliwa hakuonekana tena hadi Februari 18, 2026 mwili wake ulipokutwa pembeni ya barabara eneo la Bereko wilayani Kondoa katika Mkoa wa Dodoma, ukiwa na majeraha makubwa kichwani, kuvunjwa mikono na kutobolewa macho.

Kifo hicho cha kikatili mbali na kuzua hofu na majonzi pia imeleta mashaka miongozo mwa wafanyabiashara wa madini jijini Arusha na pia imezua maswali juu ya ukimya uliopo kuhusu watuhumiwa, licha ya eneo alipotekewa kuwa na kamera.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alipoulizwa kwa njia ya simu, amesema hawezi kuweka chochote hadharani hadi upelelezi ukamilike.

“Upelelezi unaendelea tutawapa taarifa kwa hatua za awali tulipofikia tukikamilisha,” alisema Kamanda huyo na alipoulizwa iwapo kuna watu wanaoshikiliwa na Polisi.

Matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana na kutoonekana na wengine kupatikana wameuawa, yanazidi kuitikisa nchi ambapo kwa miaka 10 iliyopita tangu, watu zaidi ya 100 wanadaiwa kutekwa.

Miongoni mwao ni Ally Kibao ambaye alikuwa mmoja wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyeshushwa kwenye basi Septemba 8, 2024 na baadaye mwili wake kupatikana akiwa ameuawa kikatili.

Wengine ambao wametekwa na hawajulikani walipo ni pamoja na Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Cuba, Huphrey Polepole, makada wa Chadema Mdude Nyagali na Deusdedit Soka na makada wa CCM, Daniel Chonchorio wa Mwanza na Sinda Mseti wa Tarime, mkoani Mara.

Kauli za wafanyabiashara

Wakizungumza katika eneo la tukio, baadhi ya wafanyabiashara walidai kuwa Banjoo alitoka mazoezi na kukutana na watu watatu waliokuwa eneo la mapokezi na kuondoka naye kuzunguka pembeni ya jengo upande wa kulia.

“Huyu kaka huwa namuona hapa mara kwa mara anakuja kufanya mazoezi na kuna muda ananunua maji hapa, lakini siku hiyo aliingia na kufanya mazoezi kisha akatoka na watu watatu ambao sijaweza kuwafahamu na kuondoka naye kabla ya juzi hapa kuona picha mitandaoni kuwa ameuawa,” alidai mfanyabiashara huyo.

Mwananchi ilifika eneo la tukio na kwa haraka ilifanikiwa kuona  kamera tatu za CCTV kwa mbele moja ya jengo na moja ipo upande wa kushoto, na nyingine kulia lakini pia katikati karibu na mlango mkubwa wa kuuingilia nako kuna nyingine, kamera zote zikiwa zinamulika waingiaji, wanaotoka ndani ya jengo na wanaozunguka

Mbali na kamera hizo za usalama pia wako askari wanaolinda jengo hilo kwa upande wa kushoto, na kulia na wako wanaokaa eneo la mapokezi wakiwa na silaha za moto.

Upande wa kushoto jengo hilo la NCAA linapakana na jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mita chache upande wa kushoto lipo jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na makao makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa na Wilaya.

Halikadhalika hatua sizizozidi 10 mkabala na jengo hilo, zipo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha na Ofisi ya mbunge. Upande wake kulia kuna Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Arusha ambalo limepakana na jengo la Halmashauri ya Jiji la Arusha na Hoteli ya Palace yenye pia ya Benki ya NMB.

Majengo hayo yote yana kamera za usalama na Askari Polisi wanaolinda majengo hayo na hoteli, hivyo kufanya mazingira ya watekaji kuwa hadharani hasa taarifa zinazoeleza kuwa watekaji hawakuwa wamejifunika sura.

Mmoja wa wafanyabiashara wa madini, Festo Lucas amesema ni ajabu hadi sasa Jeshi Polisi kudai upelelezi unaendelea wakati vifaa saidizi vipo.

“Hatutegemei Polisi hadi sasa waseme wahusika hawajapatikana na uzuri watu waliwaona, na CCTV zipo za jengo na taasisi hizo za Serikali, tunaomba ukweli uwekwe wazi tujue undani wa kifo cha mwenzetu,” amesema.

Taarifa za mauaji

Banjoo mkazi wa Sanawari jijini Arusha,  anaichukuliwa na watu wasiojulikana Februari 12, 2026 hadi Februari 18, 2026 mwili wake ulipokutwa Kondoa katika Mkoa wa Dodoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Galus Hyera alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kwamba uchunguzi unaendelea.

“Hizo taarifa tumezipokea na sisi ndio tuko katika kuzifuatilia, lakini kwa haraka haraka ni kweli mtu huyo amefariki,” alisema Kamanda huyo.

Mtoto wa marehemu, Mussa Abdilah alisema baba yake aliondoka kwenda mazoezi kama kawaida yake Alhamisi ya Februari 12, 2026   hakurudi.

“Tulihangaika kupiga simu zake bila kupokelewa na ndio tukapata mashaka zaidi na kuanza kutafuta kwa watu wa karibu na ndugu wengine bila mafanikio,”alidai.

“Tuliamua kutoa taarifa za baba kupotea katika vyombo vya habari ndio tukapigiwa simu na watu kuwa kuna mwili umeokotwa Februari 18, 2026 pembeni ya barabara eneo la Bereko huko Dodoma,” alisema kijana huyo.

Alisema walipofika Dodoma wakautambua mwili ni wa baba yao na umekutwa na majeraha mbalimbali ya kipigo, kuvunjwa mikono na kutobolewa macho.

“Kiukweli ni ngumu kuelezea lakini tulikuta mwili wa baba ukiwa umeharibika vibaya huku ukiwa na majeraha na mikono yote kuvunjwa na mbaya zaidi wauawaji walimtoboa macho,” alieleza mtoto huyo.

Alidai hadi kufikia juzi walikuwa hawajaweza kutambua wahusika wa tukio hilo na wameliomba Jeshi la Polisi kufanya upelelezi wa kina kuhakikisha wahusika wapatikana kujua chanzo cha mauaji hayo.

“Hatujui waliohusika na kifo cha baba yetu maana eneo la tukio wanasema baba alionekana akifanya mazoezi na baada ya kumaliza aliondoka na watu wasiojulikana na hiyo ikawa mwisho wa maisha yake hadi tunaokota mwili.

“Tunaomba jeshi la Polisi na vyombo vyote vya usalama kutusaidia kupeleleza kwa kina wahusika wa mauaji haya na tukajua chanzo ni nini ili angalau haki ya baba yetu ipatikane na wao wapate adhabu stahiki,” alisema na kuangua kilio.

Marehemu Banjoo ameacha mke mmoja na watoto watatu na mwili wake ulitarajiwa kuzikwa Februari 20, 2026 katika makaburi ya familia eneo la Moivo Jijini Arusha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *