Dar es Salaam. Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa katika Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) ni hali ya amani na usalama barani Afrika, ambayo imeelezwa kuwa si shwari.
Bara hilo linapitia wimbi jipya la mitihani inayochochewa na ushindani wa rasilimali, migogoro ya muda mrefu pamoja na changamoto za kijiografia zinazoendelea kubadilika.
Hayo yalibainika katika mkutano huo uliofanyika Februari 14 na 15, 2026, jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Hata hivyo, wakati viongozi hao wakijadili masuala hayo, imepita zaidi ya miongo sita tangu mataifa mengi ya Afrika yapate uhuru. Ndoto ya bara lenye amani, umoja na ustawi imeendelea kupishana na uhalisia wa migogoro ya mara kwa mara.
Ripoti na tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa, licha ya mafanikio ya kisiasa na kiuchumi katika baadhi ya nchi, maeneo kadhaa ya Afrika bado yanakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, mapinduzi ya kijeshi, ugaidi na migogoro ya kikabila.
Ripoti ya Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Stockholm ya mwaka 2023 ilionyesha Afrika ndilo eneo lenye ongezeko kubwa zaidi la migogoro ya silaha duniani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa takwimu za Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI), zaidi ya migogoro 35 ya silaha ilirekodiwa barani Afrika mwaka 2022, ikilinganishwa na 28 mwaka 2017.
Wakati huo huo, matumizi ya kijeshi katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara yalifikia dola bilioni 20.6 mwaka 2022.
Lawama za nje au ndani?
Kauli inayojirudia miongoni mwa baadhi ya viongozi wa Afrika ni kwamba rasilimali za bara hilo, yaani madini, mafuta, gesi na ardhi yenye rutuba, ndizo zinazoliponza, wakidai mataifa ya nje huchochea migogoro ili kuvuna.
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).
Hata hivyo, hoja hiyo ina mizizi ya kihistoria, hasa ukizingatia ukoloni na siasa za Vita Baridi. Wachambuzi wanakiri kuwepo kwa ushawishi wa nje, lakini wanasisitiza mizizi mikuu ya migogoro iko ndani ya mifumo ya uongozi na taasisi za Afrika yenyewe.
Mchumi wa maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, Paul Collier, katika kitabu chake The Bottom Billion kilichochapishwa mwaka 2007, anaeleza mataifa masikini yenye rasilimali nyingi lakini taasisi dhaifu huwa katika hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katika kitabu hicho, anasisitiza mapato ya rasilimali yanapokusanywa na vikundi vidogo vya watawala bila uwajibikaji, huongeza ushindani wa kisiasa unaochochea migogoro.
Kama hiyo haitoshi, ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2020 kuhusu Udhaifu, Migogoro na Vurugu ilikadiria ifikapo 2030 hadi asilimia 67 ya watu masikini zaidi duniani wataishi katika nchi zilizoathiriwa na migogoro, nyingi zikiwa Afrika.
Benki hiyo ya Dunia inaeleza udhaifu wa taasisi, rushwa na ukosefu wa huduma za msingi ni vichocheo vikuu vya migogoro ya ndani.
Ombwe la uongozi na taasisi
Wataalamu wa siasa za Afrika wanasema tatizo si rasilimali, bali namna zinavyosimamiwa. Ripoti ya mwaka 2022 ya Mo Ibrahim Foundation kuhusu hali ya utawala barani Afrika ilionyesha licha ya maendeleo katika miundombinu na huduma za afya katika baadhi ya nchi, viashiria vya usalama na utawala wa sheria vilidorora katika zaidi ya nusu ya mataifa ya Afrika tangu mwaka 2012.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi 21 zilishuhudia kuporomoka kwa viwango vya usalama na haki, huku mapinduzi ya kijeshi yakirejea katika ukanda wa Sahel.
Katika kipindi cha 2020 hadi 2023, mapinduzi ya kijeshi yalishuhudiwa katika mataifa ya Mali, Burkina Faso, Guinea na Niger.
Hali hiyo imeibua mjadala kuhusu udhaifu wa taasisi za kidemokrasia na kushindwa kwa mifumo ya kikatiba kujenga imani kwa wananchi.
Mchambuzi wa masuala ya utawala kutoka nchini Ghana, Profesa Adebayo Olukoshi, amewahi kueleza katika makala zake kuwa “tatizo la Afrika si ukosefu wa katiba au sera, bali utekelezaji na utamaduni wa uwajibikaji.”
Anaeleza kuwa pale ambapo taasisi zinakuwa chini ya matakwa ya mtu au chama tawala, migogoro ya kisiasa hubadilika kuwa migogoro ya kijamii na hata ya kijeshi.
Nafasi ya jumuiya za kikanda
Katika juhudi za kudumisha amani, bara lina miundo ya kikanda na kibara kama Umoja wa Afrika (AU) na jumuiya za kikanda kama Jumuiya ya Uchumi kwa Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Intergovernmental Authority on Development (IGAD).
Mtaalamu wa Siasa za Afrika, Dk Mallik Mesa amesema miundo hiyo imefanikiwa katika baadhi ya nyakati kuzuia au kupunguza migogoro, lakini imekumbwa na ukosoaji.
“Kwa mfano, ECOWAS ilichukua hatua kali dhidi ya mapinduzi ya Mali mwaka 2020 kwa kuweka vikwazo vya kiuchumi,” amesema.
Hata hivyo, amesema vikwazo hivyo vilikuwa na athari kwa wananchi wa kawaida zaidi kuliko kwa watawala wa kijeshi.
Aidha, amesema hatua za kijeshi zilizotishiwa dhidi ya Niger mwaka 2023 zilionyesha mgawanyiko miongoni mwa wanachama.
Kwa upande wa AU, amesema licha ya kuwa na Itifaki ya Amani na Usalama na Baraza la Amani na Usalama, utegemezi wake mkubwa wa kifedha kwa wahisani wa nje umekuwa changamoto.
Ripoti ya AU ya mwaka 2021 ilionyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya bajeti ya shughuli za amani ilitoka kwa wafadhili wa kimataifa.
Dk Mesa amesema hali hiyo inapunguza uhuru wa uamuzi na kasi ya utekelezaji.
Muktadha wa kimataifa, ugaidi
Hali ya usalama Afrika pia imeathiriwa na mitandao ya ugaidi. Takwimu za Kituo cha Afrika cha Tafiti za Kimkakati za mwaka 2023 zinaonyesha zaidi ya vifo 23,000 vilihusishwa na makundi yenye itikadi kali barani Afrika mwaka 2022, ongezeko la asilimia 48 kutoka mwaka 2021.
Ukanda wa Sahel ulitajwa kuwa kitovu kipya cha ugaidi duniani.
Wakati baadhi ya viongozi wakilaumu kuingiliwa na mataifa ya nje, wataalamu wa usalama wanaona ukosefu wa ajira kwa vijana, mipaka isiyolindwa na rushwa ndani ya vyombo vya dola vinachangia kuimarika kwa makundi hayo.
Ripoti ya Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ya mwaka 2017 kuhusu safari za kuelekea itikadi kali ilibaini asilimia 71 ya vijana waliojiunga na makundi yenye misimamo mikali barani Afrika walitaja ukosefu wa ajira na kutoridhishwa na Serikali kama sababu kuu.
Uchumi, usawa na mpasuko wa kijamii
Mbali na siasa, pengo la kipato na ukosefu wa usawa ni chanzo kingine cha misuguano. Ripoti ya UNDP ya mwaka 2022 ilionya kuwa janga la Uviko-19 lilisukuma takribani Waafrika milioni 30 zaidi katika umasikini uliokithiri.
Wakati huohuo, nchi zenye rasilimali kama mafuta na madini zimeendelea kushuhudia migogoro inayohusishwa na ugawaji wa mapato.
Mchumi wa Zambia, Dambisa Moyo, katika andiko lake, anaeleza kuwa misaada isiyo na masharti madhubuti imechangia kuimarisha tawala zisizo na uwajibikaji.
Kwa mtazamo wake, suluhisho la kudumu linahitaji kuimarisha sekta binafsi, kuongeza ajira na kupunguza utegemezi kwa misaada ya nje.
Nini kifanyike?
Waasisi wa harakati za ukombozi wa Afrika walitamani bara lenye umoja na amani. Kwame Nkrumah aliwahi kusisitiza kuwa umoja wa kisiasa na kiuchumi ndio kinga dhidi ya migogoro na ubeberu.
Hata hivyo, wataalamu wa sasa wanaona kuwa umoja huo hauwezi kujengwa bila misingi imara ya utawala bora, kama anavyoeleza Mchambuzi wa Siasa za Kimataifa, Said Majjid.
“Kwanza, kuna haja ya kuimarisha taasisi huru, yaani mahakama, vyombo vya uchaguzi na mabunge, ili kujenga imani kwa wananchi,” amesema.
Kwame Nkrumah enzi za uhai wake.
Hata hivyo, utafiti wa Taasisi ya Afrobarometer wa mwaka 2023 unaonyesha zaidi ya asilimia 60 ya Waafrika wanapendelea demokrasia kuliko aina nyingine ya utawala, lakini asilimia 48 wanahisi demokrasia katika nchi zao haifanyi kazi ipasavyo.
Majjid amesema mageuzi ya sekta ya usalama ni muhimu, akisisitiza jeshi na polisi vinapaswa kuwajibika kwa raia na si kwa watawala binafsi.
“Nchi kama Ghana na Botswana ni mifano ya mafanikio ya kudumisha nidhamu ya kijeshi chini ya mamlaka ya kiraia,” amesema.
Mchambuzi mwingine wa siasa za kimataifa, Dk Benson Bana amesema jumuiya za kikanda zinahitaji uhuru wa kifedha na kisera.
Amependekeza kuongeza michango ya ndani ya nchi wanachama kwa AU na kuanzisha mifuko maalumu ya dharura ya kukabiliana na migogoro bila kusubiri wahisani.
Dk Bana amesema uwekezaji katika elimu na ajira kwa vijana ni mkakati wa muda mrefu wa kuzuia migogoro, hivyo unapaswa kuzingatiwa.
Kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), takribani vijana milioni 12 huingia katika soko la ajira kila mwaka, lakini nafasi rasmi zinazozalishwa ni chini ya milioni nne.
“Pengo hili linazalisha hali ya kukata tamaa inayoweza kutumiwa na wanasiasa au makundi yenye misimamo mikali,” amesema mchambuzi huyo.