
Dar es Salaam. Sharia ya Allah, Mwingi wa hekima na Mjuzi wa kila kitu, imekuja ikiwa kamili kwa mahitaji ya mwanadamu; inarekebisha maisha yake, inanyoosha upotovu wa nafsi yake, na wakati huo huo huzingatia udhaifu wake na ubinadamu wake pamoja na hali mbalimbali zinazompata na kumuathiri.
Ndiyo maana Uislamu umejengwa juu ya msingi wa wepesi, huruma na upole katika sharia zake zote. Sharia ya Uislamu haiwalazimishi wafuasi wake yale wasiyoyaweza. Allah Mtukufu amesema: “Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim…” (22:78).
Kadhalika Allah amesema: “ “Mwenyezi Mungu anataka kukupeni yaliyo mepesi wala hataki kukupeni yaliyo mazito.” (2:185)
Saumu ni ibada inayohitaji subira na ustahimilivu. Wapo katika jamii ambao huenda wasiweze kuimudu katika hali fulani.
Kwa mujibu wa kanuni ya Uislamu ya kurahisisha na kuondoa uzito, Allah Mtukufu amewaruhusu baadhi ya waja wake kuacha kufunga kwa kuwahurumia na kuwapunguzia uzito.
Msafiri anaruhusiwa kutofunga mchana wa mwezi wa Ramadhani. Ikiwa ni safari ya halali isiyo na maasi ndani yake.
Allah Mtukufu amesema: “Basi atakayekuwa miongoni mwenu ni mgonjwa au yuko safarini, basi atimize idadi katika siku nyingine..” (2:185)
Huu ni ushahidi wazi kwamba msafiri anaruhusiwa kufungua saumu, na atalazimika kulipa siku alizofungua baada ya Ramadhani.
Sheria ya Kiislamu imehusisha kupunguza swala na kuruhusu kufungua saumu katika “safari” kwa ujumla, bila kutaja umbali maalumu.
Hata hivyo, kwa kuwa safari mara nyingi huambatana na mashaka, ambayo kwa kawaida hupatikana katika safari ndefu, wanazuoni wamekhitalifiana katika kubainisha umbali unaoruhusu kufungua saumu.
Wapo waliosema umbali unaoruhusu kufungua saumu ni wa safari ya siku mbili kamili au zaidi kwa mwendo wa ngamia au miguu, unaokadiriwa kuwa takribani kilomita 80.
Wapo waliosema hakuna umbali maalumu; kila kinachoitwa safari kwa desturi (‘urf) ni halali kufungua saumu. Kauli yenye nguvu ni ya kwanza, kwa kuwa safari ya siku mbili huhitaji maandalizi na ndani yake kuna mashaka yaliyo wazi.
Lililo bora kwa msafiri ni kufanya jambo jepesi kwake kati ya kufunga na kufungua. Ikiwa vyote viwili ni sawa kwake (hakuna ugumu wowote), basi kufunga safarini ni bora ili kupata fadhila ya wakati wa Ramadhani.
Hata hivyo, ikiwa kufunga kunamsumbua au kumletea mashaka, basi inampasa asifunge safarini.
Ikiwa mtu amekusudia kukaa zaidi ya siku nne katika mji fulani safarini, basi atawajibika kufunga saumu na kuswali swala kamili kama wakazi wengine, kwa kuwa hukumu za safari zinakuwa zimekatika kwake.
Hali hii ni sawa iwe amekaa kwa ajili ya masomo, biashara, au mambo mengine halali. Ikiwa amekusudia kukaa siku nne au chini ya hapo, au amekaa kwa ajili ya haja fulani bila kujua ni lini itamalizika, basi anaruhusiwa kufungua saumu, kwa kuwa hukumu za safari bado hazijakatika kwake.
Kadhalika hatofunga asiyeweza kufunga kwa sababu ya ulemavu wa kudumu usio na matumaini ya kupona. Mfano wa kikongwe au mgonjwa asiyetarajiwi kupona.
Na Kikongwe ana hali mbili: Kuna ambaye amerukwa na akili kwa sababu ya ukongwe, huyu hatofunga wala kulipa fidia.
Ama yule ambaye hajarukwa na akili huyu ndio atatoa fidia ya kulisha masikini mmoja kila siku.
Katika hali hii, haimlazimu kufunga kwa kuwa sumu haimudu, na katika Uislamu hakuna kulazimishwa jambo lisilowezekana. Allah Mtukufu amesema: “Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi ila kwa kadiri ya uwezo wake.” (2:286)
Anapofungua asiyeweza kufunga, itamlazimu kulisha maskini mmoja kwa kila siku aliyofungua, ana hiari, akitaka atalisha nafaka (kama vile mchele au unga) kwa maskini, kila mmoja atapewe kiasi cha robo pishi (takribani gramu 562 au nusu na robo). Au akitaka ataandaa chakula kilichopikwa na kuwaita maskini kwa idadi ya siku alizofungua.
Mfano: Akiwa amefungua siku 30, awaalike maskini 30.
Mgonjwa ambaye ugonjwa wake unatarajiwa kupona ameruhusiwa kufungua saumu, lakini atalazimika kulipa siku alizofungua.
Mgonjwa wa aina hii ana hali tatu Mosi: Ikiwa kufunga hakumsumbui wala hakumdhuru, basi ni lazima afunge, kwa kuwa hana udhuru wa kufungua.
Pili, Ikiwa kufunga kunamsumbua lakini hakumdhuru, basi ni bora afungue, na haifai kwake kufunga, kwa kuwa kufanya hivyo ni kuacha ruhusa ya Allah na kujitaabisha nafsi bila sababu. Sharia imejengwa juu ya urahisi na kuondoa mashaka.
Tatu, Ikiwa kufunga kunamdhuru, basi ni lazima afungue, na hairuhusiwi kwake kufunga. Ikiwa mgonjwa atapatwa na maradhi katikati ya siku ya Ramadhani akiwa amefunga, na ikawa ni vigumu kuendelea hadi jioni, anaruhusiwa kufungua kwa kuwa udhuru umetokea.
Hivyo atalazimika kulipa siku alizofungua.
Vilevile, ikiwa daktari bingwa, mwaminifu katika dini yake, atathibitisha kwamba kufunga kutamsababishia maradhi au kutachelewesha kupona kwake, basi anaruhusiwa kufungua, ili kulinda afya yake na kujiepusha na madhara, kisha atalipa siku hizo baadaye. Itaendelea katika toleo lijalo In Shaa Allah.