Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeziingiza kwenye ushindani mkali kampuni za michezo ya kubashiri baada ya kutangaza rasmi zabuni ya haki ya kubashiri mechi ya watani wa jadi ya Ligi Kuu Bara, Yanga dhidi ya Simba.

Mechi hiyo inayotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi, imepangwa kuchezwa Machi Mosi, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na tayari imeanza kuonekana kama fursa muhimu ya kibiashara kwa sekta ya michezo ya kubashiri.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Februari 18, 2026 na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, shirikisho hilo lilisema haki zote za kubashiri michezo ya Ligi Kuu Bara ni mali yake pamoja na washirika wake waliotambuliwa kisheria.

TFF ilieleza wazi kampuni yoyote ya kubashiri itakayojihusisha na kubashiri mchezo huo au michezo mingine ya ligi bila kuwa mshirika halali wa shirikisho hilo, itakuwa imekiuka taratibu na sheria zilizopo.

Katika taarifa hiyo, shirikisho limetoa onyo kali kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya kampuni au taasisi yoyote itakayokaidi maelekezo hayo, ikiwa ni sehemu ya kulinda masilahi ya mpira wa miguu nchini na kuongeza uwajibikaji.

Hatua hii ni ya awali, kwani tayari TFF imetangaza kutafuta mzabuni wa michezo ya kubashiri (betting partner) kwa ajili ya Ligi Kuu na mashindano yake mengine.

Baadhi ya wadau wa mpira wa miguu walisema hatua hiyo ya TFF inaelezwa ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika usimamizi wa masuala ya kibiashara kwenye soka la Tanzania, huku ikilenga kudhibiti sekta ya kubashiri, kuongeza mapato halali na kuhakikisha maendeleo endelevu ya mchezo huo.

Walisema TFF inatakiwa kuendesha mchakato wa zabuni kwa uwazi na kwa kuzingatia taratibu zote za nchi, huku ikilenga kupata mshirika atakayetoa thamani halisi ya kibiashara kwa mpira wa miguu wa Tanzania.

Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema hatua hiyo itasaidia kupambana na vitendo vya upangaji matokeo kwa kuweka mifumo rasmi ya ufuatiliaji wa miamala ya ubashiri na kushirikiana na mamlaka husika za udhibiti na usalama.

“Huu ni mwanzo mzuri wa udhibiti wa kupanga matokeo (match fixing) na utasaidia kuongeza mapato yatakayorejeshwa kwenye maendeleo ya soka, ikiwemo uendeshaji wa ligi, uboreshaji wa uamuzi wa waamuzi, maendeleo ya vijana na miundombinu ya michezo,” alisema Mwesigwa.

Kwa upande wa katibu mkuu wa zamani wa Simba, Mwina Kaduguda alisema ubashiri ni sehemu muhimu ya uchumi wa soka duniani, hivyo ni jambo zuri kutumia fursa hiyo kuongeza nguvu ya kifedha katika ligi yetu.

“Ligi ikiwa na nguvu kifedha, kila kitu huimarika kwa maana ya klabu, wachezaji, waamuzi na hata timu za taifa,” alisema Kaduguda, akisisitiza uimara wa kifedha unaweza hatimaye kuleta mafanikio makubwa zaidi katika mashindano ya kimataifa.

Peter Simon, mmoja wa wamiliki wa akademi ya soka, alisema soka la Tanzania limekua kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni, lakini bado linahitaji uwekezaji mkubwa ili kushindana kikanda na kimataifa.

“TFF inapaswa kutumia fursa zilizopo kuzalisha mapato kutokana na wadhamini na kampuni za ubashiri,” alisema Simon, huku akisisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kusimamiwa kwa kanuni madhubuti na kuzingatia maslahi ya muda mrefu ya mchezo.

Kwa jumla, wadau wa soka wanaona uamuzi wa TFF kama mwanzo wa zama mpya za usimamizi wa kibiashara katika soka la Tanzania na rasilimali za mchezo zinalindwa, thamani yake inaongezeka na manufaa yanarejea moja kwa moja kwenye maendeleo ya mchezo wenyewe.

Wanaamini mapato ya ziada yanaweza kuboresha maandalizi ya mechi, viwango vya waamuzi, ligi za vijana na soka la wanawake, pamoja na kupunguza mzigo wa kifedha kwa klabu.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, endapo TFF itapata mzabuni (partner) wa michezo ya kubashiri (betting), udhamini huo hautoathiri mikataba ya sasa ya timu mbalimbali za ligi kuu na wadhamini wao wakuu kutoka makampuni ya kubashiri.

Hata hivyo, baadhi ya maofisa wa kampuni za kubashiri zilizopo hapa nchini ambao wameomba majina yao kuhifadhiwa kwa sasbabu si wasemaji wakuu wa suala hilo, wamesema kuwa ni mapema kuzungumzia wakati huu wakati TFF ndiyo kwanza imewatangazia kuomba zabuni hiyo.

“Hili jambo limetangazwa na TFF na kwa upande mwingine, sisi Betway hatuwezi kuzungumzia kwani wasemaji wakuu wapo Afrika Kusini na jambo hili linahitaji uamuzi. Hivyo tunaomba wadau wetu wasubiri,” alisema.

Afisa mwingine wa kampuni ya Betika alisema watawasiliana na wakuu wao nchini Kenya kuhusiana na suala hili.

“Ni jambo ambalo linahitaki maamuzi baada ya kunyanya mchanganuo, kwa sasa ni mapema sana,” alisema afisa huyo.

Kwa upande wake, mmoja wa maofisa wa kampuni ya Sportpesa alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *