
Utawala wa Kizayuni wa Israel umewawekea vizuizi vikali Wapalestina kuingia katika Msikiti wa al-Aqsa katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, kwa ajili ya Swala ya Ijumaa ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, huku mamia ya watu wakipanga foleni kwenye kizuizi cha Qalandiya karibu na Ramallah wakitarajia kuingia.
Mamlaka za Israel zimesema kuwa hazitawaruhusu Wapalestina zaidi ya 10,000 kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu kuingia katika Msikiti huo, ambao ni moja ya maeneo matakatifu zaidi ya Waislamu.
Watoto walio chini ya umri wa miaka 12, wanaume wenye zaidi ya miaka 55, na wanawake wenye umri wa miaka 50 au zaidi ndio walioruhusiwa na Wazayuni kuswali Masjidul Aqsa.
“Kuna watu milioni 3.3 wanaoshi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kwa hivyo kuruhusu 10,000 pekee kuswali Ijumaa hii ya kwanza ya Ramadhani ni tone baharini, na ni wachache tu ambao wameweza kuingia,” Nour Odeh, ripota wa Al Jazeera amesema akiwa katika kituo cha upekuzi cha Qalandiya.
Wapalestina wanawewekea vizuizi hivi katika hali ambayo, Walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada juzi walivamia tena Msikiti huo mtakatifu wa al-Aqsa na kufanya vitendo vya kichochezi dhidi ya Qibla hicho cha kwanza cha Waislamu.
Msikiti wa al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds, na utawala pandikizi wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo; lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.