Morogoro. Wahenga walisema, ‘Baada ya dhiki ni faraja.’ Methali hii imejidhihirisha wazi katika maisha ya Jemima Bashite, mwanamke jasiri aliyekulia katika familia yenye kipato cha kawaida na ambaye amepitia changamoto nyingi kabla ya kufikia mafanikio ya kumiliki saluni inayotoa huduma zote za urembo wa nywele, kucha na ngozi.
Kuelekea Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani (IWD), Machi 8, 2026, Mwananchi limemtembelea na kuzungumza naye kuhusu maisha yake, changamoto, mafanikio, fursa na vikwazo alivyopitia katika harakati za kujenga ustawi wake.
Anasema jina lake limeanza kutambulika miongoni mwa wanawake wajasiriamali wanaochipukia, lakini safari yake haikuwa nyepesi.
Jemima anasema 2009 akiwa mwanafunzi wa kidato cha nne, alikumbwa na pigo kubwa la kufiwa na baba yake mzazi. Tukio hilo lilibadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yake na familia kwa ujumla.
Mfanyabiashara Jemima Bashite akiwa anamtengeneza nywele mmoja wa wateja wake.
Anasema mama yake alibaki na jukumu la kulea familia peke yake, hali iliyosababisha misingi ya kiuchumi kuyumba. Ndoto za Jemima za kuendelea na masomo ya juu zilianza kufifia.
Anasema tangu akiwa shuleni, ndoto yake kubwa ilikuwa kuajiriwa serikalini. Alitamani kujiunga na Chuo cha Utumishi wa Umma ili baadaye apate ajira rasmi itakayomwezesha kusaidia familia yake.
Hata hivyo, baada ya baba yake kufariki dunia, hali halisi ya maisha ilimlazimisha kuacha mpango huo. Badala ya kwenda chuo, aliolewa na kuanza maisha ya ndoa mapema kuliko alivyotarajia.
“Baada ya baba yangu kufa, maisha yalibadilika sana. Mama alibaki peke yake akihangaika kutunza familia. Sikupata nafasi ya kwenda chuo kama nilivyokuwa nimepanga. Lakini Mungu ni wa ajabu, akanipa mlango mwingine wa kutokea, nikapata mchumba, nikaolewa nikaanza maisha ya ndoa,” anasimulia Jemima.
Ingawa mumewe aliweza kumudu mahitaji ya msingi ya familia, Jemima anasema hakutaka kubweteka. Alijitosa katika biashara ndogondogo na vibarua ili kujiongezea kipato. Aliuza mkaa, akafanya kazi viwandani, katika ofisi binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali. Kila alipopata fursa, aliichangamkia, akiwa na lengo la muda mrefu la kumiliki biashara yake mwenyewe.
Tangu akiwa shuleni, alikuwa na mwanga wa kufanya biashara inayohusiana na mambo ya urembo.
Anasema jirani yao mmoja alikuwa anamiliki saluni na mara kwa mara alimwita akamsaidie kazi ndogondogo. Kupitia uzoefu huo wa awali, alianza kuvutiwa na kazi za saluni na kujifunza kwa vitendo.
Hata hivyo, hakuwahi kufikiria kuwa siku moja angekuwa mmiliki wa saluni yake binafsi.
Mwaka 2022, baada ya kujikusanyia akiba kutokana na vibarua mbalimbali, aliamua kuchukua hatua ya ujasiri. Alinunua vifaa vya msingi vya saluni na kufungua biashara yake. Alianza kwa mtaji mdogo na wafanyakazi wawili tu. Hakukuwa na samani za kifahari wala mapambo ya kuvutia, lakini kulikuwa na dhamira, nidhamu na huduma bora.
Wafanyakazi wa Jemima Bashite wakiwa wanamsuka mmoja wa wateja wake.
Anasema mwanzo haukuwa rahisi. Baadhi ya watu walimdharau na kubeza biashara yake kwa kuiona ndogo na isiyo na mwelekeo. Wengine walimkatisha tamaa wakimwambia ushindani ni mkubwa na hatadumu. Lakini aliamua kusimama imara.
“Nilianza kidogokidogo, lakini nilijua ninachokitaka. Nilihakikisha huduma ninazotoa ni bora na wateja wanaridhika. Taratibu, wateja walianza kuongezeka,” anasema.
Kadri siku zilivyopita, saluni yake ilianza kupata wateja wa kudumu. Sifa ya ubora wa huduma ilisambaa kwa njia ya mdomo.
Aliongeza wafanyakazi akizingatia uadilifu, bidii na weledi. Hapo ndipo alipoanza kutimiza ndoto nyingine iliyokuwa moyoni mwake ya kuwawezesha wasichana waliokata tamaa, hususan wenye ulemavu nao wajitegemee.
Anasema kwa kupitia familia ya mume wake, alikutana na Lipsa Daud, binti mwenye ulemavu wa kutosikia lakini mwenye kipaji kikubwa cha kusuka nywele za mitindo mbalimbali.
Jemima anasema alitambua kipaji hicho na akaamua kumpa nafasi ya kufanya kazi katika saluni yake. Baadaye alipokea binti mwingine mwenye ulemavu pia kama huo, na akawafundisha kazi nyingine za saluni kama kuosha nywele, kukausha, kuseti na kupamba nywele.
“Niliona kuna vipaji vingi vimejificha. Wasichana hawa walikuwa wanasuka mitaani wanalipwa kati ya shilingi 200 mpaka 1,000 na wakati mwingine walikuwa wakiwasuka watu bure. Nilipowaleta hapa, walikutana na mitindo mipya na wateja wa aina tofauti. Leo hii wanafanya kazi ya kusuka kwa kujiamini,” anasema Jemima.
Kwa sasa saluni yake iliyopo Barabara ya Kitope ina wafanyakazi sita, wakiwamo wasichana wawili wenye ulemavu na mfanyakazi mmoja wa kiume anayehusika na huduma za kusafisha miguu na upakaji rangi za kucha.
Je, amewezaje kuelewana na wafanyakazi wake ambao hawasikii?
Anasema kujifunza lugha ya alama ilikuwa changamoto mwanzoni, lakini aliweka juhudi za makusudi. Leo, anaweza kuwasiliana nao kwa urahisi na hata baadhi ya wateja wamejifunza ishara za msingi.
Kwa upande wake, Lipsa anasema alianza kusuka tangu akiwa mdogo. Baada ya kumaliza shule, aliendelea kusuka mitaani kwa ujira mdogo. Kupata nafasi katika saluni ya Jemima anasema kumebadilisha maisha yake.
“Sasa nasuka karibu mitindo yote ya nywele, hata ya gharama kubwa. Ninaweza kujikimu na kusaidia familia yangu. Nawaomba watu wasitutazame kama hatuwezi, bali watupe nafasi ya kuonyesha uwezo wetu,” anasema Lipsa.
Kwa Jemima, mafanikio si tu kipato anachopata, bali ni mabadiliko anayoyaona kwa wengine. Anasema kupitia biashara hiyo, anachangia gharama za masomo ya watoto wao, anasaidia familia yake na tayari ameanza ujenzi wa nyumba.
Mbali ya maendeleo yake binafsi, Jemima anasema biashara yake inalipa pia kodi za Serikali, “Kifupi mimi ni mlipa kodi wa Serikali licha ya kuwa biashara yangu si kubwa kivile, lakini kodi nalipa, TRA wakija hapa mimi sikimbii,” anasimulia huku akitoa kicheko kwa kujiamini.
Anasema siri ya mafanikio yake ni kujituma, kujifunza kila mara na kuhakikisha ubora wa huduma anayoitoa unabaki kuwa kipaumbele. Anasisitiza kuwa saluni yake si mahali pa umbea bali ni eneo la kazi.
“Kuna mazoe watu husema ooh saluni wanawake wanafanya umbea tu, hapana hii ni ofisi kama zilivyo ofisi za biashara nyingine. Mimi na watu wangu hawa tunaendesha maisha kupitia ajira ya biashara hii,” anasisitiza.
Anasema anathamini sana ushirikiano na ushindani kama nyenzo ya kupambania mafanikio, akiamini kuwa ushindani chanya huleta maendeleo kwa wote.
Akizungumzia Siku ya Wanawake Duniani, anasema ni siku muhimu ya kutambua mchango wa mwanamke katika maendeleo ya familia, jamii na taifa. Anasema maadhimisho hayo humtia moyo na kumkumbusha kuwa juhudi zake zina thamani.
Katika ushauri wake kwa Serikali, Jemima anapendekeza kuwepo kwa mkakati wa kuwapatia wanawake mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali kabla ya kuwapa mikopo.
Anasema mtaji bila maarifa unaweza kupotea kirahisi. Hivyo anashauri kuimarishwa kwa ufuatiliaji wa wasichana wenye ulemavu ili kuwabaini wenye vipaji na kuwasaidia kuviendeleza.
Safari ya Jemima ni ushahidi kwamba changamoto hazipaswi kuwa mwisho wa ndoto. Kutoka maumivu ya kumpoteza baba, kukosa fursa ya elimu ya juu na kuanza maisha ya ndoa mapema, ameweza kujijenga upya na kuwa mwanga kwa wengine.
Amegeuza dhiki kuwa daraja la kufikia faraja na sasa ana ndoto ya kumiliki saluni kubwa zaidi yenye huduma zote za urembo, eneo la maharusi, masaji na duka la vipodozi.
Kwa uthubutu, uvumilivu na moyo wa kuwainua wengine, Jemima anasema ameonyesha kuwa mafanikio huanza pale mtu anapoamua kutokata tamaa.
Anasema ndoto ya usemi usemao ‘Baada ya dhiki ni faraja’ anaamini itatimia kwa kuwa safari bado inaendelea.