Chanzo cha picha, Tumaini Tv
Muda wa kusoma: Dakika 2
Kanisa Katoliki nchini Tanzania na Afrika linaomboleza kifo cha Kardinali Polycarp Pengo aliyefariki usiku wa Alhamis Februari, 19, 2026, kama ilivyotangazwa na Askofu Mkuu wa Dar es Salaam Thaddaeus Ruwa’ichi kuwa Pengo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete akiwa na umri wa takribani miaka 82.
Alifahamika kwa tabia ya upole na kuzungumza taratibu hata pale alipozungumzia masuala nyeti na mazito ya kiimani au kuikosoa mifumo ya uongozi wa kisiasa, serikali na viongozi wake.
Hata alipochokozwa alijibu kwa upole. Wakati mmoja, Askofu Josephat Gwajima wa kanisa la Ufufuo na Uzima alimtolea maneno makali, lakini Pengo alipoulizwa na chombo kimoja cha habari alijibu kuwa hamfahamu huyo askofu.
Tayari alikwishaeleza bayana anapendelea azikwe eneo la Pugu, lililopo takribani kilomita 25 nje ya jiji la Dar es Salaam.
Pengo si tu alichagua eneo la kuzikwa bali pia aliratibu kaburi atakamozikwa. Katika moja ya mahojiano na Kituo cha televisheni cha Tumaini kinachomilikiwa na jimbo kuu la Dar es Salaam, Pengo alisema eneo hilo alililependa na anatarajia uamuzi na chaguo lake hilo litaheshimiwa.
Hatahivyo, mara nyingi maaskofu, maaskofu wakuu na makadinali wa Kanisa Katoliki huzikwa ndani ya makanisa ya Kiaskofu (Cathedrals)
Kadinali Pengo ni nani?
Polycarp Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5, 1944 huko Sumbawanga mkoani Rukwa, eneo la nyanda za juu kusini lililo jirani na ziwa Tanganyika. Alipadrishwa mwaka 1971.
Alisomea Thiolojia ya Maadili mjini Roma katika Chuo Kikuu cha Pontifical Lateran, ambako alipata shahada ya uzamivu (udaktari) mwaka 1977.
Alifundisha Thiolojia ya Maadili katika Seminari kuu ya Kipalapala iliyo Tabora kwa muda mfupi, kisha akawa Gombera (Rector) wa kwanza wa Seminari Kuu ya Segerea jijini Dar es Salaam hadi mwaka 1983.
Aliteuliwa kuwa Askofu wa Nachingwea (sasa Lindi) mwaka 1983, na baadaye Askofu wa Tunduru–Masasi mwaka 1985.
Mwaka 1990 aliteuliwa kuwa Askofu Mwandamizi (Coadjuctor) Dar es Salaam, akingojea kustaafu rasmi kwa Laurean Kardinali Rugambwa. Mwaka 1992 akawa Askofu Mkuu wa Dar es Salaam kufuatia kustaafu kwa Kardinali Rugambwa ambaye alifariki dunia Desemba 1997.
Pengo alitangazwa kuwa Kardinali na Papa John Paul II katika mkutano wa makadinali (consistory) wa tarehe 21 Februari 1998.
Chanzo cha picha, Tumaini TV
Alikuwa miongoni mwa makardinali waliopiga kura katika mkutano wa kumchagua Papa mwaka 2005 uliomchagua Papa Benedict XVI na pia katika mkutano wa mwaka 2013 uliomchagua Papa Francis.
Alikuwa mwanachama wa vyombo mbalimbali vya Curia ya Vatican, ikiwemo uinjilishaji wa mataifa, mafundisho ya imani, mazungumzo ya kidini na tamaduni (mabaraza), pamoja na Baraza Maalum la Afrika la Sinodi ya Maaskofu.
Tangu mwaka 2007 alikuwa rais wa SECAM (Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar).
Chanzo cha picha, Tumaini TV
Septemba 18, 2012, aliteuliwa na Papa Benedict XVI kuwa mmoja wa wajumbe wa Sinodi kwa Mkutano Mkuu wa 13 wa kawaida wa Sinodi ya Maaskofu uliofanyika Oktoba 2012.
Papa Francis aliridhia ombi la Kardinali Pengo kustaafu uaskofu mkuu Agosti 15, 2019 na baadaye nafasi yake kuchukuliwa na Thaddaeus Ruwa’ichi.
Tarehe 19 Februari 2026 majira ya saa 4 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kama ilivyotangazwa na Askofu Mkuu wa Dar es Salaam Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, Kardinali Polycarp Pengo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete.