Picha ya Vladimir Akeev, kutoka kijiji cha Sedanka mashariki mwa Urusi, ambaye alifariki miezi minne baada ya kujisajili kupigana vita vya Ukraine.

Chanzo cha picha, Kamchatka government

Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika Kijiji kimoja kinachotegemea uvuvi cha Sedanka, mashariki mwa Urusi, maisha yamekuwa magumu.

Makaazi kadhaa yamekosa huduma muhimu kama maji, vyoo vya ndani, vifaa vya joto licha ya eneo hilo kushuhudia kibaridi cha hadi nyuzi joto -10 majira ya baridi.

Eneo hilo limezingirwa na msitu na ardhi iliyolowa maji. Wakaazi wa eneo hilo hutembelea soko lao kati ya mwezi Mwei na Oktoba kwa kutumia boti au magari yanayoweza kuendeshwa juu ya barafu, na katika majira ya baridi usafiri ni kwa kutumia magari yanayoendeshwa juu barafu au ndege.

Nafasi za ajira hapa ni finyu sana, na wakaazi wengi hutegemea uvuvi na kukuza chakula chao wenyewe.

Ila sasa karibu wanaume wote wa Sedanka wenye umri kati ya miaka18-55 hawapo tena, kulingana na wakaazi, karibu wote walijiunga na jeshi kupigana vita kati ya Urusi na Ukraine,

‘Hakuna mtu wa kuteka kuni’

“Inavunja moyo, watu wengi wameuawa,” anasema Natalia, mkaazi wa Kijiji hiki ambaye tumebadilisha jina lake kwasababu za kiusalama.

“Mume wa dadangu na binamu yangu wako katika mstari wam bele wa vita. Katika kila familia kuna mtu mmoja ambaye ameenda kupigana”

Kijiji hiki cha Sedanka kiko kaskazini magharibi mwa peninsula ya Kamchatka, karibu na bahari ya Okhotsk, kilomita 7,000 kutoka mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine.

Wanaume 39 kutoka Kijiji hiki walitia saini mkataba na Urusi kupigana katika vita vinavyoendelea Ukraine kutoka kwa idadi ya wanaume 258. Kati ya hao 12 wameuawa huku 7 wakiwa hawajulikani waliko.

“Wanaume wetu wote walijiunga na oparesheni ya kijeshi” kundi moja la wanawake lilimwambia gavana wa mkoa huo alipozuru Kijiji hicho mwezi Machi 2024.

“Hakuna mtu wa kuteka kuni ya kutumia majira ya baridi” walisema katika kipindi kimoja cha televisheni nchini humo.

Wale wanaopigana katika jeshi la Urusi wengi wao huwa wameshawishiwa, wengine hujitolea, kuna wanajeshi kutoka kampuni za kibinafsi, wafungwa, na wale wanaopewa kandarasi kupigana.

Shirika la habari la BBC pamoja na shirika la habari la Urusi la Medizona na watafiti wakujitolea, kufikia sasa tumedhibitisha kuwa wanajeshi 40,201 wa Urusi waliuawa mwaka wa 2025.

Kulingana na uchambuzi wetu tunakadiria kuwa wanajeshi waliofariki mwaka wa 2025 wanafika 80,000. Na hii inasemekana kuwa mwaka wenye mauti zaidi kwa Urusi tangu vita kati yake na Ukraine kuanza mwezi Februari 2022.

Vifo vilivyodhibitishwa mwaka wa 2024 vinafika 69,362 ikiwa idadi sawa ya vifo vilivyotokea mwaka wa 2022 na 2023 na vifo hivyo vimeongezeka tangu mwisho wa mwaka wa 2024.

Tumedhibitisha vifo hivyo kwa kutumia ripoti rasmi zinazotolewa na daftari la usajili wa watu waliofariki, pia kupitia taarifa za magazeti, taarifa zinazochapishwa katika mitandao ya kijamii na familia au jamaa wa karibu, na data kutoka makaburini.

Kwa jumla BBC imedhibitisha vifo vya wanajeshi 186,102 wa Urusi waliofariki vitani.

Ila idadi kamili ya vifo inasemekana kuwa juu zaidi, kwani vifo vinayotokea eneo la vita hazinakiliwi.

Wataalam wa masuala ya jeshi wanasema takwimu zetu zinawakilisha kati ya 45-65% ya jumla ya vifo, na kusema kuwa idadi hiyo inaweza kuwa kati ya 286,000 hadi 413,500.

Ukraine pia imewapoteza wanajeshi wake wengi.

Mwezi uliopita, Rais Volodymyr Zelensky aliambia kituo kimoja cha televisheni cha France 2, kuwa idadi ya wanajeshi waliofariki vitani ni 55,000.

Aliongezea kuwa bado kuna idadi kubwa ya watu ambao hawajulikani waliko,na hawana idadi kamili.

Kulingana na mtandao wa UA Losses, idadi ya wanajeshi wa Ukraine waliofariki ni takriban 200,000.

Waombolezaji waliovaa koti wanaonekana wamekusanyika karibu na jeneza la Akeev.

Chanzo cha picha, Kamchatka government

Warusi wengi waliouawa vitani wanamajina ya kislavoni.

Ila idadi kubwa ya vifo vimerekodiwa miongoni mwa jamii ndogo ndogo, haswa katika maeneo ambayo hayajaendelea kiuchumi kama Siberia na Sedanka.

Sedanka ni nyumbani kwa Koryaks na Itelmens, jamii ya kiasili ambazo wakati wa vita wanafaa kutohusishwa na hamasisho la kujiunga na jeshi.

Mwanaharakati mmoja wa vita Maria Vyushkova, anasema kituo cha televisheni cha kitaifa cha Urusi hupaza sauti sana, kuwa watu kutoka kabila za kiasili ‘huzaliwa na uwezo wa kupigana” na wana ujuzi wa kufyatua bunduki ili kuwashawishi kujiunga na jeshi kupigana vita.

“Jamii nyingi za kiasili hujivunia utamaduni wao, na Ikulu ya Kremlin imekuwa ikitumia fahari yao kuwasajili kujiunga na vita” alisema Vyushkova.

Mwanaume mmoja kutoka Sedanka Vladimir Akeev, mwenye umri wa miaka 45, muwindaji na mvuvi alijiunga na jeshi la Urusi mwaka wa 2024.

Miezi minne baadaye aliuawa akiwa vitani.

Waombolezaji katika sherehe yake ya mazishi iliofanyika mwezi Novemba 2024, waliweza kufika makaburini kwa kutumia gari zinazoendeshwa juu ya barafu.

Kwingineko vifo kutoka jamii za kiasi ni kundi la Nenets 201, Chukchi 96, Khanty 77, Koryaks 30, Inuit 7.

Uchambuzi wa BBC umebaini kuwa 67% ya vifo ni kutoka vijiji na miji midogo ambazo zinawaakazi chini ya laki moja.

Miji mikubwa kama Moscow, zilirekodi idadi ndogo ya vifo vya wanajeshi. Kulingana na takwimu ya miji hizi kubwa wanajeshi watano kati ya wanaume 10,000 walifariki.

Katika maeneo maskini kama Buryatia, mashariki mwa Siberia na Tuva kusini mwa Siberia idadi ya vifo ipo juu kati ya 27-33% ikilinganishwa na miji mikubwa.

Kinachowashawishi wengi kujiunga na jeshi la Urusi kutoka vijijini, ni hali ya Uchumi, mshahara watakaolipwa, na elimu anasema mtaalam wa demografia Alexey Raksha.

Kutokana na hili, idadi kubwa ya wanajeshi wa Urusi, wanatokea maeneo maskini, na wao ndio hurekodi idadi kubwa ya vifo.

“Kwa wengi kinachowapa hamasa si umaskini tu ila kukosa matumaini na kuwa na hisia za hawana chochote cha kupoteza”

Moja kati ya nyumba tano eneo la Sedanka, zilizojengwa wakati wa Umoja wa Kisovyeti, zinasemekana kuwa hatari kwa maisha ya watu

Chanzo cha picha, Kamchatka government

Katika kijiji cha Sedanka, sanamu ya kumbukumbu ya “walioshiriki oparesheni maalum ya kijeshi” ilizindliwa majira ya kupukutika majani 2024.

Mwaka uliopita, serikali ya mkoa huo iliahidi kuwasaidia familia waliowapoteza jamaa zao katika jeshi la Urusi, na pia kuwapa “jina la heshima kijiji hicho” kwa kutoa wanaume wake kushiriki vita vya Urusi na Ukraine. Ila kufikia sasa kijiji hicho hakijapewa heshima hiyo wala familia zilizoathirika kupewa msaada.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *