
Mwaka mzima wa mwaka jana, kama ilivyo miaka mingine ya nyuma, mstaafu wetu wa taifa wa kima cha chini amejikuta akishuhudia siku mbalimbali maalumu za kuadhimisha kitu ama jambo lililowekwa na Umoja wa Mataifa ama na taifa letu ili kuadhimisha jambo ama kitu hicho.
Yako mambo mengi. Kuna Siku ya Wanawake Duniani, ambayo mara kadhaa mgeni rasmi ama mhutubiaji mkuu anakuwa, ajabu, mwanaume. Kuna Siku ya Watoto. Kuna Siku ya Vijana, ambayo mara nyingi mhutubiaji mkuu anakuwa ni mzee kuliko huyu mstaafu anayeshia kuwahutubia vijana kuwa “vijana ni Taifa la Kesho” isiyofika!
Kuna siku ya… mama wee!… choo, hiki hiki choo ambacho mara kadhaa tumepata msaada wa kuchimbiwa choo na mataifa ambayo baadhi, kama siyo yote, tuna kawaida ya kuwaita mabeberu ama wakoloni tunapopishana nao kauli, lakini huwaita wafadhili tukitaka mikopo kwao ama tukitaka watuchimbie vyoo. Mwe.!
Mstaafu wetu anafikia hata kushangazwa na dunia inapoadhimisha siku isemekanayo kuwa ni “Siku ya Wapendanao”, ambayo miaka ishirini au ishirini na tano tu iliyopita, Wabongo tulikuwa hatuna hata habari nayo, na watu walikuwa wakipendana tu bila kuhitaji siku moja maalumu ya kuonesha wanavyopendana!
Ni bahati mbaya sana kwamba, kama mambo mengine mengi, siku hiyo sasa imeshikiwa bango na Wabongo kiasi kwamba siku hiyo hiyo nchi nzima inakuwa imevaa “wekundu wa Msimbazi”, hata kama siyo kushabikia ile timu yetu inayovaa nyekundu!
Sisi tuna wakulima, ambao wakichoka kulima na wakastaafu hakuna cha pensheni, wala hata shilingi elfu hamsini tu wajipongeze kwa kazi ngumu ya kutulimia. Sana sana wameishia kupewa maneno ya kanga tu, tena rejekti, badala ya matibabu ya bure walioahidiwa kupewa!
Siri-kali haijasema lolote kuhusu watu hawa muhimu kwa Taifa. Ikumbuke tu kwamba wao ndio walitulisha kwa mazao ya chakula na yale ya biashara yaliyoipa nchi fedha zilizotuwezesha wakati tuijenga nchi, halafu hata pensheni ya kijishilingi elfu hamsini hatuwapi, achilia hili mbali, matibabu ya bure kwa wazee!
Halafu humu humu nchini kuna wanaosemekana kuwa ni wawakilishi wa wananchi wanaopokea shilingi milioni… my God (Kisambaa kwa msisitizo!)… kumi na nne kwa mwezi! Yale yale ya “Shamba la Wanyama”: binadamu wote wako sawa, lakini wengine wako sawa zaidi ya wengine!
Tuna Siku ya Mashujaa, ambayo zamani ilifanyika Septemba mosikila mwaka, lakini alipoangia mjuzi mmoja na kuibadilisha tarehe hiyo bila kutoa sababu za msingi, mstaafu wetu sasa hajui tarehe za Siku ya Mashujaa. Anashituka pale anapoona wakongwe kadhaa wakijikongoja kuweka ñgao na mikuki pale bustani ya Mnazi Mmoja, kama ilivyokuwa zamani.
Mstaafu wetu huwaza sana kwamba siku hii muhimu ya mashujaa wetu, wakipaswa kuwemo wastaafu’ walioijenga nchi, iliamuliwaje iwahusu wakongwe tu waliopigana vita huko Burma na kwingineko kwenye jeshi la King’s African Rifles (KAR), ambao kwa hakika sasa wengi wameishatangulia mbele za haki.
Mstaafu hujikuta akijiuliza sana kila akifungua runinga, kukuta ni Siku ya Mashujaa na pamoja na kupewa chupa mbili, tatu za soda na sahani ya pilau au chips, mnawalipa pensheni ya shilingi ngapi kwa mwezi? Au baada ya Siku ya Mashujaa hamuwajui tena mpaka mwaka ujao tena, kama bado wapo?
Mstaafu wa kima cha chini ni shujaa wa Taifa, pamoja na kwamba waheshimiwa wanajikanyaga-kanyaga kuhusu hilo. Ndio ameifanya nchi hii iwepo na kuheshimika, japo huku kuheshimika sasa ni jambo la kujadiliana. Kwa hakika siyo zile enzi zile za “Mwenyekiti wa nchi tano zilizo mstari wa mbele”!
Ianzishwe “Siku ya Wastaafu Tanzania”, ili wastaafu wapate mahali pa kueleza matatizo yao, na siyo kuweka ngao na mikuki tu Mnazi Mmoja.
Tunataka zaidi, kubwa na la kwanza likiwa lile la kutupatia pensheni ya shilingi laki tano kwa mwezi na kuwapa wastaafu hizo milioni tano na laki tano, wakiwa hai wajifariji, maana miaka 40 ya ajira ni mingi. Msingoje mpaka wafe. Si hela yao? Si mnafanyia biashara bila angalau kuwaambia tu?
Kama siri-kali unaweza kumpangia mwakilishi wake kupata shilingi milioni kumi na nne kwa mwezi kwa kuunga mkono hoja, hata mstaafu inaweza kumpangia shilingi laki tano kwa mwezi kwa kazi njema aliyofanya kuijenga nchi, ikiwemo kuandamana kuunga mkono Azimio la Arusha, ambalo kwa bahati mbaya leo ni hadithi tu!
0754 340606 / 0784 340606