WIZARA ya Afya kupitia Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (NPHL) imeanza mwaka wa tatu wa utekelezaji wa mradi wa kuboresha maabara za afya ya jamii ili kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza, ambapo mwaka huu mkazo utawekwa kwenye udhibiti wa kipindupindu nchini.

Akizungumza katika uzinduzi wa mwaka wa tatu wa mradi huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa NPHL, Ambele Mwafilango, amesema mradi huo wa miaka mitano unafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Afya la Korea (KOFIH) na unatekelezwa kwa awamu.

Amesema hadi sasa utekelezaji umefanikiwa ambapo mwaka wa kwanza ulitumia zaidi ya Sh milioni 460, mwaka wa pili Sh milioni 674, huku mwaka huu ukiwa na bajeti ya Sh milioni 694 kwa ajili ya kuendeleza shughuli za mradi. Mwafilango amesema KOFIH tayari imetoa fedha hizo na kuipongeza kwa imani waliyoonyesha kwa Tanzania, huku akiahidi kuwa utekelezaji utafanyika kwa weledi. Pia amesema baadhi ya vifaa vya maabara na vitendanishi tayari vimenunuliwa.

Ameeleza kuwa mradi ulianza katika mkoa wa Dar es Salaam ukilenga magonjwa ya Dengue na Chikungunya pamoja na magonjwa ya njia ya hewa kama kikohozi na mafua. Kwa mwaka huu, utekelezaji utaenea nchi nzima na kuangazia zaidi ugonjwa wa kipindupindu ambao umekuwa changamoto katika maeneo mbalimbali.

Akizindua mradi huo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohamed Mang’una, ameishukuru Serikali ya Korea Kusini kupitia KOFIH kwa ufadhili huo na kuahidi kusimamia vyema matumizi ya fedha ili kuimarisha utambuzi wa mapema wa magonjwa. Amesema utambuzi wa haraka wa magonjwa unarahisisha udhibiti wake na kwamba hali ya magonjwa nchini inaendelea kuimarika.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Dk Otilia Gowele, ameipongeza Maabara ya Taifa kwa kuweka mikakati inayolenga kudhibiti magonjwa ya mlipuko. Amesema idara ya kinga ina jukumu la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na magonjwa ya kuambukiza kupitia programu za afya ya umma.

Ameongeza kuwa elimu hiyo inalenga kubadili tabia, kuboresha mazingira ya makazi na kuhakikisha wagonjwa wanaofika vituo vya afya wanapatiwa huduma kwa haraka. Aidha, amesema maabara hiyo sasa ina vifaa vya kisasa vya uchunguzi, hivyo sampuli nyingi zitachunguzwa ndani ya nchi badala ya kupelekwa nje. SOMA: Tufuate maelekezo ya wataalamu kujikinga magonjwa ya milipuko

Mtaalamu wa afya kutoka KOFIH, Hansol Park, amesisitiza umuhimu wa mipango madhubuti ili kudumisha ubora na uwajibikaji katika utekelezaji wa mradi, pamoja na kuandaa mahitaji ya mwaka wa nne mapema. Amesema lengo kuu la mradi ni kuimarisha miundombinu ya kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza ili hatua za haraka zichukuliwe pale milipuko inapotokea, akibainisha kuwa miaka miwili iliyopita imeonyesha mafanikio makubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *