
Kamanda wa Jeshi la Wanamaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza udharura wa ushirikiano kati ya vikosi vya majini vya Iran na vile vya Afrika Kusini na Sri Lanka ili kukabiliana na vitisho vya pamoja na kuhakikisha usalama endelevu katika maji ya kimataifa.
Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo alipokutana na kufanya mazuungumzo na Admeri Monde Lobese, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Afrika Kusini, na Admeri Kanchana Banagoda, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Sri Lanka, pambizoni mwa manuva ya kijeshi ya majini ya “Milan 2026”.
Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mazungumzo hayo sera ya kuendeleza maingiliano ya baharini na nchi huru na akasema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutoa uzoefu wake katika nyanja za mafunzo, teknolojia, na shughuli kwa jeshi la majini la Afrika Kusini na Sri Lanka.”
Aidha ameashiria jukumu muhimu la ushirikiano kati ya vikosi vya majini katika kukabiliana na vitisho vya baharini na kuhakikisha usalama wa njia za mawasiliano ya kimataifa, akisema: “Diplomasia ya baharini ni mojawapo ya nguzo kuu za mkakati za Jeshi la Wanamaji.
Kwa upande wake Admeri Monde Lobese, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Afrika Kusini ameashiria uwezekano wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, na kusema: “ushirikiano wa kitaaluma, kubadilishana mafunzo kwa wajumbe, na kunufaika na uzoefu wa pamoja wa uendeshaji kunaweza kuchukua jukumu muhimu katika kuimarisha usalama wa njia za mawasiliano ya baharini na kuimarisha utulivu wa kikanda.