Dar es Salaam. Mjumbe wa Baraza la Chama cha Wananchi (CUF), Mohammed Ngulangwa pamoja na wenzake wawili, wamejikuta wakishikiliwa na Polisi na kutolewa nje ya kikao kinachoendelea cha Baraza Kuu la chama hicho, ambacho kilikuwa kinajadili majina ya wagombea watakaoingia kwenye uchaguzi wa nafasi za juu ndani ya chama.

Sababu ya kuondolewa kwao katika kikao hicho kilichogubikwa na kelele, ni madai kwamba walikuwa wakipinga kila hoja iliyowasilishwa, jambo lililodaiwa kuwanyima wajumbe wengine utulivu.

Kikao hicho kinaendelea katika makao makuu ya chama hicho, Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Ngulangwa na wenzake ni wafuasi wa Profesa Ibrahim Lipumba na msimamo wao ni kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kutengua uchaguzi uliomrejesha madarakani mwenyekiti huyo pamoja na viongozi wengine.

Kabla ya kikao kuanza, Mwananchi lilizungumza na Ngulangwa na kumuuliza sababu za kushiriki kikao hicho ilhali hawakubaliani na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Huwezi kupinga jambo ukiwa nje ya mchakato. Naenda kushiriki ili niweze kupinga uamuzi utakaofikiwa,” amesema.

Baada ya kuingia kwenye mkutano huo, Ngulangwa na wenzake walionekana kuongoza mjadala kwa muda mwingi, hali iliyosababisha baadhi ya wajumbe mara kwa mara kuwataka Polisi wawaondoe ili kuruhusu kikao kiendelee kwa utulivu.

Jaribio la kulitaka Jeshi la Polisi kuwaondoa ndani ya ukumbi lilifanyika mara tatu bila mafanikio, baada ya katibu wa kikao hicho, Mussa Mbarouk kuendesha kura iliyoonyesha wajumbe wengi walitaka wabaki.

Hata hivyo, kadri muda ulivyokwenda, Ngulangwa alionekana kuwa kinara wa kupinga uamuzi uliokuwa ukifikiwa.

Hatimaye, katibu huyo alitoa amri ya kuwaita Polisi waliokuwa wameweka kambi nje ya ukumbi, kuingia na kuwaondoa.

Endelea kufuatilia yanayojiri kupitia tovuti ya Mwananchi na mitandao ya kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *