RAIS wa Malawi, Peter Mutharika amepiga marufuku waajiriwa katika hospitali za serikali au taasisi nyingine za afya za umma kumiliki hospitali binafsi. Pia, amri ya Rais Mutharika aliyoitoa Februari 16, mwaka huu inazuia watumishi hao kufanya kazi katika hospitali binafsi au kuwa na hisa katika vituo binafsi vya huduma za afya au maduka ya dawa.
Amri hiyo pia inazuia waajiriwa katika hospitali za serikali au taasisi nyingine za afya za umma kuomba, kulazimisha au kupokea malipo au fedha kwa wagonjwa ili wawapatie huduma za afya. “Yeyote atakayebainika anafanya vitendo hivi ataondolewa mara moja kwenye utumishi na atachunguzwa kwa kuzingatia sheria za Malawi,” ameeleza Rais Mutharika.
Rais Mutharika ameagiza mwajiriwa yeyote ambaye kwa sasa ana umiliki uliotajwa hapo juu au hisa, awe ameusitisha ndani ya siku 30 tangu atoe amri hiyo. SOMA: Serikali Zanzibar kushirikisha sekta binafsi huduma za hospitali
Kwa mujibu wa amri hiyo, ambaye hataitekeleza atafukuzwa kazi na atachukuliwa hatua za kisheria. Katika amri hiyo Namba 1 ya Mwaka 2026, Rais Mutharika alieleza kuwa ameapa kuilinda katiba ya Malawi inayotoa haki kwa wananchi wote katika nchi hiyo kupata huduma za tiba bila ubaguzi.
Rais Mutharika amewatuhumu baadhi ya watumishi katika sekta ya afya wamekuwa wakiwashawishi wagonjwa waende kwenye hospitali zao binafsi ili wapate huduma bora za afya. “Kitendo kama hiki ni kuvunja sheria, kinyume na maadili na kwa ujumla hakikubaliki, ni haki ya kikatiba ya mgonjwa kupata huduma za afya,” alieleza.
Umoja wa Madaktari Wasaidizi wa Malawi (PAUM) umepinga amri ya Rais Mutharika na umetahadharisha kuwa inaweza kuongeza matatizo katika sekta ya afya nchini humo. Rais wa PAUM, Solomon David Chomba amedai amri hiyo ni adhabu na haitasaidia kumaliza matatizo, badala yake alishauri changamoto zilizopo zitafutiwe ufumbuzi kwa majadiliano, uwekezaji na mipango. Chomba alidai watumishi wa serikali katika sekta ya afya wana mishahara midogo, hivyo wanalazimika kufanya kazi binafsi ili kukidhi mahitaji.
