Mauaji ya Thiaroye ni mojawapo ya jinai na uhalifu mkubwa zaidi wa umwagaji damu na uliofichika zaidi, ambao ulifanywa na Ufaransa wakati wa utawala wake wa kikoloni nchini Senegal.
Mauaji hayo ya halaiki ya askari wa Kiafrika yaliyofanywa mwaka 1944 katika kambi ya Thiaroye, sio tu ni mfano mmojawapo wa ukatili wa mfumo wa kikoloni, lakini pia ni kielelezo cha miongo kadhaa ya ufichaji na ukanushaji ukweli.
Ukoloni wa Ufaransa barani Afrika, hususan nchini Senegal, haukuishia tu kwenye unyonyaji wa kiuchumi na udhalilishaji wa kiutamaduni, bali uliambatana pia na ukatili wa kimfumo na jinai za kimpangilio. Kuhusiana na hilo, mauaji ya askari wa Senegal kwenye kambi ya Thiaroye nje kidogo ya Dakar yameanika na kuweka wazi alama ya ukatili huo na ufichaji huo uliofanywa kwa muda mrefu.
Mnamo Desemba Mosi, 1944, ilitokea moja ya jinai za umwagaji damu mkubwa zaidi uliofanywa na Ufaransa wakati wa utawala wake wa kikoloni. Waathiriwa walikuwa askari wa Kiafrika waliojulikana kama Thiaroye, ambao walikuwa wameshiriki kwenye vita vya ukombozi wa Ufaransa dhidi ya Ujerumani ya Nazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa simulizi za historia, baada ya kukamatwa mateka na kuachiliwa, askari wapatao 1,300 kutoka makoloni ya Afrika Magharibi ambao walikuwa wamepigana katika medani za vita barani Ulaya, mnamo mwezi Novemba 1944 walihamishiwa kwenye kambi ya Thiaroye. Askari hao walikuwa na matarajio ya kupata bakio la malipo yao ya huko nyuma, lakini badala ya kushukuriwa, walidhalilishwa na kudharauliwa. Walichodai, ilikuwa ni kupatiwa malipo sawa ya mshahara kamili kama walivyofanyiwa askari wenzao wazungu wa Ufaransa. Dai hilo lilichukuliwa kama tishio na hatari kubwa na maafisa wa kikoloni wa Ufaransa, kwa sababu lingeliweza kutoa changamoto kwa nidhamu ya matabaka ya rangi iliyowekwa na dola hilo la kikoloni.

Usiku wa Novemba 30 na alfajiri ya kuamkia Desemba Mosi, jeshi la Ufaransa, lililoongozwa na Jenerali Yves de Boisboissel, liliizingira kambi ya Thiaroye. Alfajiri ilipowadia, bunduki za rashasha zilifyatuliwa, na risasi zake zikawamiminikia askari wasio na silaha waliokuwa wakilalamikia haki yao. Mashuhuda wamesimulia mandhari ya kutisha waliyoshuhudia: ni ya askari waliomiminiwa risasi vitandani mwao, kundi la askari waliofyatuliwa risasi walipokuwa wakikimbia, na majeruhi waliouliwa kwa kupigwa risasi kwa karibu.
Mara baada ya mauaji hayo, maafisa wa kikoloni wa Ufaransa walianza mara moja kufanya kazi ya kuficha ukweli. Idadi ya vifo ilipunguzwa mno na tukio hilo likageuzwa jina na kuitwa “uasi.” Ripoti rasmi za Ufaransa zinasema idadi ya vifo ilikuwa ni 35, au sana sana 70.
Lakini utafiti na uchunguzi wa kina uliofanywa katika miongo ya hivi karibuni, hususan wa Kamati ya Uchunguzi ya Senegal iliyoongozwa na mwanahistoria mashuhuri Mamadou Diouf, umefichua ukubwa wa uhalifu huo. Matokeo ya kazi iliyofanywa na kamati hiyo, ambayo yaliwasilishwa Oktoba 2025 kwa rais wa Senegal kupitia ripoti rasmi ya kurasa 301 yanaonyesha kuwa mauaji ya Thiaroye hayakuwa kitendo cha kujichukulia hatua mikononi, bali ni operesheni “iliyoandaliwa mapema, ikapangwa kwa umakini na kutekelezwa kwa uratibu”, lengo likiwa ni kukandamiza piganio la haki la askari wa Kiafrika la kudai usawa ambalo lilitokana na Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Utafiti wa ugani na uchimbaji wa akiolojia umeonyesha kuwa takwimu zilizotolewa na Ufaransa si sahihi hata kidogo. Makadirio ya kuaminika zaidi yanaonyesha kuwa idadi ya waliouawa ilikuwa kati ya askari 300 hadi 400, au hata zaidi. Kwa mujibu wa tafiti hizo, zaidi ya askari wapiganaji 400 wa Senegal walitoweka, kana kwamba hawakuwahi kuwepo kabla.
Tume ya uchunguzi ilifikia hitimisho kwamba, maafisa wa Ufaransa walifanya kila waliloweza kuficha mauaji hayo. Walighushi hati, ikiwa ni pamoja na za rejista za kusajili uingiaji na utokaji wa askari ndani ya Ufaransa na Dakar, na kubadilisha idadi ya askari waliokuwepo kambini humo. Watafiti walikabiliwa na kilichotajwa kama ukuta wa “moshi na vioo” na vizuizi vya kuzifikia kumbukumbu za hifadhi za kijeshi za Ufaransa.
Uchimbaji wa akiolojia, ulioanza Mei 2025, ulipelekea kupatikana ugunduzi wa kustaajabisha. Wanaakiolojia waligundua kwenye kaburi moja mabaki saba ya mifupa ya watu. Katika moja ya mabaki hayo, ilionekana alama ya risasi kwenye sehemu ya moyo. Katika moja ya makaburi mengine kwenye mabaki ya mifupa hakukuwa na fuvu, mbavu, na uti wa mgongo. Katika kaburi moja, yalikutwa mabaki ya “minyororo ya chuma” iliyozungushwa kwenye mifupa ya miundi ya miguu, ikionyesha kwamba baadhi ya waathiriwa walikuwa wamefungwa pingu kabla au mara tu baada ya kuuawa. Yalipatikana pia makaburi yalioonyesha kuwa mapya kuliko mabaki ya miili iliyozikwa ndani yake, ikiwa ni ishara ya kujaribu kubadilisha hali ya kaburi na kuonyesha kwamba waathiriwa hao walifanyiwa mazishi ya heshima. Ushahidi unaonyesha pia kwamba, yamkini mauaji hayo yalienea hadi kituo cha reli. Serikali ya Senegal imeagiza uchimbaji uendelee kwenye maeneo yote yanayoshukiwa kuwa na makaburi ya halaiki.
Thiaroye ilikuwa mfano mmoja tu wa mauaji ya kimfumo yaliyofanywa na Ufaransa katika makoloni yake. Ripoti ya gazeti la L’Expression imeyalinganisha mauaji ya Thiaroye na mauaji ya halaiki ya Oktoba 17, 1961 yaliyotokea kwenye kitovu cha mji wa Paris, ambapo mamia ya waandamanaji Waalgeria waliuliwa na polisi wa Ufaransa wakiongozwa na Maurice Papon na miili yao ikatupwa kwenye Mto Seine. Chimbuko la jinai zote ni la aina moja: nidhamu iliyowekwa na ukoloni haikuweza kukubali athari za ukombozi zilizotokana na Vita vya Pili vya Dunia kwa watu wa Afrika na ukaamua kukabiliana nazo kwa mabavu. Mauaji ya halaiki ya Mei 8, 1945 nchini Algeria nayo pia yalifanywa kwa mantiki hiyo hiyo. Thiaroye haikuwa mfano wa kipekee, bali ni sehemu ya mfano wenye wigo mpana wa ukandamizaji wa mapiganio ya kudai usawa katika makoloni.
Kwa kutegemea mamlaka yake ya kujitawala, Senegal, ambayo ilipata uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo Juni 20, 1960, sasa inadai haki kwa waathiriwa wa jinai ya Thiaroye. Katika ripoti rasmi ya serikali, Senegal imeitaka Ufaransa “iombe radhi” rasmi. Ripoti hiyo inasisitizia ulazima wa kuendelezwa uchunguzi, kuweza kupatikana kikamilifu hifadhi za kumbukumbu za serikali ya Ufaransa, kutambuliwa na kurejeshwa miili ya waathiriwa, na kulipwa fidia.

Kutokana na kuzidi kufichuka ukubwa wa jinai zilizofanywa, hatimaye mnamo Novemba 2024, kwa mara ya kwanza, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyatambua mauaji ya Thiaroye kuwa ni “mauaji ya halaiki” yaliyofanywa na vikosi vya kikoloni vya Ufaransa, baada ya kupita miongo minane ya kuyakana; hata hivyo alikataa kuomba msamaha rasmi.
Mauaji ya Thiaroye ni nembo nyingine ya ukatili wa ukoloni na kumbukumbu iliyofichika ya Afrika, lakini ukweli hauwezi kupotea kamwe katika vumbi la historia…/