BAADA ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Magnet FC, Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, amesema umerudisha morali kwa wachezaji ikijiandaa kuipokea Yanga keshokutwa Jumapili.

Namungo, iliyotinga hatua ya 32 Bora katika michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB, itakuwa wenyeji wa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga kesho kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi, ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi iliyopita ugenini kwa Tanzania Prisons kwa kipigo cha mabao 3-2.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda amesematimu hiyo haikuwa katika hali nzuri ya ushindani kutokana na kudondosha pointi tano mfululizo, baada ya kukubali kichapo na sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar na kwamba ushindi iliyoupata dhidi ya Magnet umewarudisha mchezoni.

“Nimefurahi kupata matokeo mazuri kabla ya kuivaa Yanga Jumapili. Ninaamini wachezaji wangu kisaikolojia sasa wapo vizuri na watakuwa bora katika mchezo ujao, kwani tunahitaji matokeo mazuri ili kuendelea kujitengenezea mazingira mazuri ya ushindani,” amesemaMgunda na kuongeza;

“Mchezo na Magnet FC niliutumia kama sehemu ya maandalizi, lakini ulikuwa muhimu kwetu kupata matokeo mazuri ili kurudisha morali ya wachezaji. Nafurahi tumefanikiwa, tutaendelea tulipoishia Jumapili kwa kuhakikisha tunapata matokeo mbele ya Yanga.”

Amesemawanaenda kukutana na timu bora iliyotoka kufanya vizuri Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya kushindwa kuendelea hatua inayofuata. Hilo halimpi presha kwani anatambua ubora na mapungufu ya wapinzani wake hao, na anaamini mbinu bora ndizo zitakazompa matokeo mazuri.

“Mechi kubwa kama tunayoitarajia Jumapili, wachezaji wengi hunaitaka ili kuonyesha ubora wao dhidi ya wachezaji bora. Hivyo sina wasiwasi, natarajia wachezaji wangu watafanya kila kitu kuhakikisha tunabaki na ushindi nyumbani.”

Akizungumzia hali za wachezaji wake, amesemawapo katika ubora na hana majeruhi na kwamba kazi aliyonayo ni kuandaa jeshi hilo analoamini litatoa upinzani wa kutosha na hatimaye kubaki na pointi tatu nyumbani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *