ENZI ya watalii kupotoshwa kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya imepita. Sasa wengi wanahamia vivutio vya nchi nyingine za Afrika Mashariki. Hali hii inaathiri uchumi wa Kenya na kudhoofisha sekta ya utalii, hasa kwa sababu ya barabara na hoteli chakavu ambazo huwakatisha tamaa wageni wanapowasili.
Watalii waliohojiwa jijini Nairobi wiki hii wamelalamikia gharama kubwa za kuingia kwenye hifadhi za wanyama hususan Maasai Mara pamoja na hoteli zilizochakaa na msongamano katika mbuga maarufu. Wengine wameeleza kuwa barabara mbovu na hofu ya usalama pia inapunguza mvuto wa kutembelea nchi hiyo hivyo kusukuma wageni kutafuta huduma bora na maeneo yasiyo na msongamano katika mataifa jirani ya Afrika Mashariki.
Uchambuzi unaonyesha kuwa sababu kuu za kushuka kwa utalii Kenya ni pamoja na miundombinu duni, gharama kubwa za huduma na changamoto za usalama.Ripoti ya Wizara ya Utalii na Wanyamapori ya Novemba 5, 2025, inaonyesha alama za chini katika miundombinu ya usafiri wa anga (3.21) na miundombinu ya ardhi na bandari (3.23) kulinganisha na viwango vya kimataifa. SOMA: Uzembe Bandari Mombasa Wapunguza Mapato Kenya
Watalii pia wanasema huduma na vifaa vya utalii ni duni ukilinganisha na nchi kama Mauritius na Afrika Kusini.Tathmini nyingine inaonyesha huduma za utalii Kenya zimepata alama ya 1.25, kiwango cha chini miongoni mwa maeneo makuu ya utalii Afrika. Mapungufu yapo katika alama za maelekezo, huduma za wageni, maji na usimamizi wa taka, hali inayopunguza kuridhika kwa watalii na muda wao wa kukaa.

Aidha, ada kubwa za hifadhi zinazofikia takribani asilimia 45 ya gharama ya safari ya kifahari zinaifanya Kenya kuwa ghali kuliko washindani wake wa karibu.Ripoti ya Benki ya Dunia pia inaonya kuwa mapendekezo ya kuongeza ada za hifadhi kwa hadi asilimia 249 yanaweza kupunguza idadi ya watalii kutoka milioni 2.3 hadi karibu milioni 1.7, na kudhoofisha ushiriki wa utalii wa ndani.
Wataalamu wanasema maendeleo ya miundombinu ya utalii nchini humo hayajasambaa sawasawa. Uwekezaji umejikita zaidi Nairobi, pwani na baadhi ya mbuga chache hali ambayo inayozuia maeneo mengine kuendelezwa na kupunguza uwezo wa sekta hiyo kukua na kustahimili changamoto. Changamoto nyingine ni upungufu wa malazi bora hasa hoteli za nyota nne na tano ambapo msimu wa kilele huongeza msongamano na kushusha ubora wa huduma.
Mfano unaotajwa mara nyingi ni Nyali, Mombasa. Mgeni aliyewahi kuishi eneo hilo tangu miaka ya 1980 anasema zamani lilikuwa na mazingira tulivu, majengo ya chini na hoteli bora zilizovutia wageni wa kimataifa. Sasa, anadai pwani imejaa taka, majengo marefu yasiyo na mpangilio, hoteli zilizoharibika na barabara zenye mashimo, hali inayotia shaka kwa watalii.

Aidha, changamoto za usalama na tahadhari za usafiri kutoka baadhi ya nchi zimewahi kusababisha kushuka kwa idadi ya wageni. Uhalifu mdogo mijini na karibu na maeneo ya hifadhi pia unaathiri taswira ya nchi kwa watalii. Wakati huo huo, mjadala unaendelea kuhusu ujenzi wa malazi ya kifahari kupita kiasi bila kuimarisha miundombinu ya msingi. Baadhi ya kambi za kifahari zinatoza zaidi ya dola 3,500 kwa usiku jambo linaloulizwa kama lina faida kwa jamii na sekta kwa ujumla.
Kwa ujumla, changamoto hizi miundombinu duni, gharama kubwa za ada, masuala ya usalama na viwango visivyo sawa vya huduma zinapunguza uwezo wa Kenya kutumia kikamilifu rasilimali zake za utalii. Pia kuna wasiwasi kuwa nchi hiyo inategemea sana taswira ya safari na wanyamapori bila kupanua aina nyingine za utalii. Hata hivyo, utalii bado ni nguzo muhimu ya uchumi wa Kenya. Inakadiriwa kuchangia takribani Shilingi trilioni 1.2 (dola bilioni 8.6) mwaka 2025 na kutoa ajira karibu milioni 1.7.
Lakini wachambuzi wanaonya kuwa mapato zaidi yanapotea kutokana na miundombinu duni, hoteli chache za ubora wa juu na changamoto za usafiri.Kutegemea jenereta na visima pamoja na barabara mbovu na huduma zisizoaminika, kunaongeza gharama za uendeshaji na kupunguza ushindani dhidi ya nchi nyingine. Hali hii pia huwakatisha tamaa watalii wenye matumizi makubwa na wageni wa kikanda ambao wangeweza kukaa muda mrefu na kutembelea maeneo mengi zaidi.
Licha ya malengo ya kuvutia watalii milioni tano ifikapo 2027 na kuongeza mapato kupitia usafiri wa ndani ya Afrika, Kenya inakadiriwa kupoteza mamia ya mamilioni ya dola kila mwaka kutokana na mapato ambayo hayajapatikana. Faida hiyo sasa inaelekezwa kwa masoko yenye miundombinu bora kama Tanzania, Rwanda, Uganda, Misri na Afrika Kusini.