Dar es Salaam. Naibu Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Mame Mandiaye Niang, amekutana na viongozi wa nchi kadhaa za Afrika wakiwemo Liberia, Mauritania, Tanzania na Botswana katika mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa haki za kimataifa na kulinda haki za waathirika wa uhalifu wa kimataifa.

Mikutano hiyo imekuja wakati Tanzania ikiweka historia nyingine, baada ya Deo Nangela, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, kujumuishwa kwenye orodha ya wagombea wa nafasi za ujaji wa ICC, hatua inayoipa nchi nafasi ya kuimarisha ushawishi wake katika utekelezaji wa sheria ya kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya ICC iliyochapishwa kwenye tovuti yake, mikutano kati ya Niang na viongozi hao ilijikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na nchi wanachama.

Aidha, mazungumzo hayo yalilenga kuendeleza juhudi za kitaifa na kikanda kupambana na vitendo vya kutokuwajibika kwa wahalifu wa uhalifu wa kimataifa, pamoja na kusisitiza nafasi ya sheria ya kimataifa katika kulinda na kutetea haki za waathirika.

Niang alifanya mazungumzo hayo ya kikazi kuanzia Februari 12 hadi 16, 2026, mjini Addis Ababa, ambako alihudhuria Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).

Viongozi waliokutana na Niang jijini Addis Ababa ni Rais wa Liberia, Joseph Boakai, aliyekuwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Sara Beysolow Nyanti, pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa na Muungano wa Kiuchumi, Dk Ibrahim Nyei.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano na Wamarekani wa Mauritania wa Jamhuri ya Mauritania, Mohamed Salem Ould Merzoug; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mahmoud Thabit Kombo; na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa wa Botswana, Phenyo Butale.

Rais Samia Suluhu Hassan akimuapisha Jaji Dk Deo Nangela kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Januari 22, 2025 Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma. Picha na Maktaba

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ICC, Niang alisema ujumbe wake mkuu kwa viongozi wa Afrika ulikuwa ni kwamba ICC iko tayari kufanya kazi bega kwa bega na mataifa ya Afrika kama mshirika wa kweli katika mapambano dhidi ya kutokuwajibika kwa wahalifu.

“Hili ni jukumu la pamoja,” alisema Niang, akitaja ushirikiano unaoendelea kati ya Ofisi yake na mamlaka za kitaifa katika nchi kama Guinea, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pamoja na wadau wengine wanaosaidia juhudi za ndani za kuhakikisha haki inapatikana kwa wahanga wa uhalifu wa kikatili.

Alieleza kuwa kupitia Sera ya Ujazilizi na Ushirikiano, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka inafanya kazi kama kitovu cha kubadilishana utaalamu na uzoefu na washirika wa kitaifa katika kushughulikia uhalifu wa kimataifa ulio chini ya mamlaka ya ICC.

“Wakati dunia ikikabiliwa na changamoto zinazotishia mshikamano wa kimataifa, jibu letu ni kuonesha kwa vitendo jinsi ICC inavyoshirikiana kwa karibu na Nchi Wanachama wake ili kuleta haki,” alisisitiza.

Haki za waathirika

Katika mazungumzo yake, Niang pia alisisitiza kuwa waathirika wa uhalifu mkubwa wa kimataifa hawapaswi kusahaulika katika mijadala ya kisiasa au kidiplomasia.

Alibainisha kuwa kuhakikisha sauti za waathirika zinasikika, haki zao zinalindwa na mchakato wa haki unasonga mbele kwa njia yenye uadilifu na kuaminika ni wajibu wa msingi kwa wadau wote wanaopambana na uhalifu wa kimataifa.

“Tunashuhudia ongezeko la mateso duniani yanayotokana na uhalifu wa kikatili. Hisia ya kutokuwajibika kwa wahalifu inachochea wimbi hili la vurugu. Lakini hatuko wanyonge; tunazo zana za kukabiliana na hali hii. Tunachohitaji sasa ni ushirikiano wa kweli na wa dhati,” alisema.

Ushirikiano na Afrika ni kipaumbele

Washirika waliokutana na Niang walieleza kutambua umuhimu wa mamlaka ya ICC katika kipindi hiki chenye changamoto nyingi za usalama na kisiasa, wakiahidi kuendeleza ushirikiano chanya na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka.

ICC imeeleza kuwa katika miezi ijayo itapanua na kuimarisha zaidi shughuli zake za ujazilizi barani Afrika kwa kushirikiana kwa karibu na mamlaka za kitaifa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa uhalifu mkubwa wa kimataifa hauendi bila kuwajibishwa.

Ziara ya Niang mjini Addis Ababa imeonekana kama ishara ya dhamira ya ICC ya kuimarisha uhusiano wake na bara la Afrika, wakati ambapo wito wa haki na uwajibikaji unazidi kushika kasi katika jamii za kimataifa.

Uchaguzi wa majaji ICC

Baraza la Nchi Wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) linatarajiwa kuchagua majaji sita wapya katika kikao chake cha 25 kitakachofanyika kuanzia Desemba 7 hadi 17, 2026, huku jina la Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Dk Deo John Nangela, likitajwa kuwamo kwenye orodha ya wagombea.

Kwa mujibu wa mfumo wa kisheria wa Mkataba wa Roma, kifungu cha 36(3)(a), majaji wa ICC huchaguliwa miongoni mwa watu wenye maadili ya hali ya juu, uadilifu usiotiliwa shaka na sifa zinazowawezesha kushika wadhifa wa juu kabisa wa kimahakama katika nchi zao.

Katika kuhakikisha mchakato unakuwa wa uwazi na unaozingatia viwango vya juu vya maadili, Baraza la Nchi Wanachama lilipitisha azimio ICC-ASP/22/Res.3 lililoanzisha utaratibu wa kudumu wa uhakiki wa kina kwa maofisa wanaochaguliwa.

Kupitia utaratibu huo, Chombo Huru cha Uangalizi (IOM) kimefungua njia ya siri ya kupokea tuhuma zozote za utovu wa nidhamu dhidi ya wagombea walioteuliwa.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, “utovu wa nidhamu” unajumuisha ukiukwaji wa haki za binadamu, unyanyasaji kazini au unaohusiana na kazi, ikiwemo wa kijinsia, matumizi mabaya ya madaraka, ubaguzi, uonevu, pamoja na makosa mazito ya kimaadili au kisheria kama rushwa au udanganyifu.

Tuhuma zinaweza kuwasilishwa kwa siri hadi Mei 31, 2026, na zitashughulikiwa kwa kuzingatia masharti ya utaratibu huo kwa lengo la kulinda hadhi ya mchakato na haki za wahusika.

Kuhusu Dk Nangela

Dk Deo John Nangela ni miongoni mwa majaji wenye wasifu mpana katika taaluma ya sheria na utumishi wa umma nchini. Januari 2025 aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, ngazi ya juu zaidi ya mahakama nchini.

New Content Item (1)

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dk Deo John Nangela wakati akila kiapo Januari 22, 2025 Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma. Picha na Maktaba

Kabla ya hapo, aliwahi kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, na pia kuhudumu katika Mahakama ya Biashara. Kabla ya kuingia kwenye mhimili wa mahakama, alifanya kazi katika Tume ya Ushindani (FCC) akiwa Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti wa Biashara.

Dk Nangela ana Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town (Afrika Kusini), Shahada ya Uzamili (LLM) kutoka SOAS – Chuo Kikuu cha London, na Shahada ya Kwanza ya Sheria (LLB) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amewahi pia kuwa mhadhiri katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa takribani muongo mmoja.

Maeneo yake ya ubobezi yanajumuisha sheria za biashara na ushindani, mikataba ya kielektroniki, utatuzi wa migogoro na masuala ya haki za binadamu.

Umuhimu kwa Tanzania

Iwapo atachaguliwa, uteuzi wa Dk Nangela katika jopo la majaji 18 wa ICC, lenye makao yake The Hague, Uholanzi, utakuwa hatua kubwa kwa taswira ya Tanzania kimataifa.

Majaji wa ICC husikiliza kesi za uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari, wakitoa maamuzi yenye athari pana katika ulinzi wa haki za binadamu duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *