Dar es Salaam. Alianza kama utani kuipambania ndoto yake ya kuwa mwanamuziki tangu akiwa mdogo na sasa anasimama kama kioo na mfano wa kuigwa kwa jamii hasa wanawake.

Ni Luiza Nyoni. Ndiyo majina halisi la mwanadada huyo, kabla ya kubadili na kufahamika zaidi kama Luiza Mbutu baada ya kuolewa na aliyekuwa mpiga gitaa la bass wa Kilimanjaro Connection, Fariala Mbutu, ambaye kwa sasa ni marehemu na alifariki dunia Desemba 25, 2025.

Mwanamuziki huyo mkongwe wa muziki wa dansi na kiongozi wa Bendi ya Twanga Pepeta, akizungumza na Mwananchi, anasema haikuwa kazi rahisi kufika alipo na aliishi na ndoto za kazi aliyoipenda akikabiliana na kila changamoto hadi kufika alipo sasa.

Kuhusu safari ya maisha yake ya muziki, Luiza anaweka bayana changamoto alizopitia, mafanikio na jinsi anavyotumia sauti kuhamasisha wanawake kujisimamia.

Safari yake inadhihirisha jinsi mwanamke anavyoweza kuinuka na kuwa mfano wa kuigwa kwa vizazi vingi.

Luiza anasema safari yake ya muziki ilianzia kanisani akiimba kwaya tangu akiwa darasa la nne na kuota siku moja awe mwimbaji mkubwa nchini.

“Kipaji changu cha kuimba kilianza tangu nikiwa darasa la nne na nikajiendeleza zaidi kwa masomo ya muziki katika kanisa la Mtakafifu Joseph kabla ya kuibukia kikundi cha Chemungwao,” anasema.

Anasema wimbo uliomtambulisha Luiza ni ‘Tumetoka Wote Mahenge’ miaka ya 1990 kabla ya kuibukia Magoma Moto Sound na baadaye mwaka 1998 alijiunga na African Stars ‘Twanga Pepeta’ aliyopo hadi sasa akiwa ndiye mkurugenzi wake.

Mwanadada huyo aliyezaliwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam na kuanza masomo katika Shule ya Msingi ya Mkamba, Kilombero darasa la kwanza hadi la tatu kabla ya kuhamishiwa Shule ya Msingi ya Mzinga, Morogoro Mjini na kusoma hadi darasa la sita na kuja kumaliza darasa la saba katika Shule ya Msingi Mushono iliyopo Arumeru, mkoani Arusha.

Baada ya kumaliza elimu ya msingi aliendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Mabibo, jijini Dar es Salaam, kisha kujiunga na masomo ya utunzaji wa stoo katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar es Salaam na kuishia kiwango cha Stashahada kutokana na ishu za ada na kujiunga baadaye na masomo ya Kompyuta Kituo cha Msimbazi, jijini Dar es Salaam, alikopata ujuzi wa kuandaa kurasa za magazeti.

Licha ya kiu ya elimu, anasema akili na ndoto zake zilikuwa katika muziki zaidi ndipo akajiunga katika masomo ya muziki yaliyokuwa yakitolewa na Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam na alisoma hatua ya kwanza hadi ya tatu kuendeleza ujuzi wa kuimba kwaya aliokuwa nao tangu darasa la nne kabla ya kuacha baada ya kujifungua mwanae, Brain.

BENDI ZA DANSI

Anasema safari ya muziki wa dansi ilianza mwaka 1997 katika bendi ya Magoma Moto, wakati huo dada yake wa kwanza, Modesta Nyoni alikuwa akiimba katika bendi ya Kalunde ya Deo Mwanambilimbi.

Baada ya hapo alitua Twanga Pepeta akiwa anaimba na kunengua, kabla ya kuwa mtunzi wa baadhi ya nyimbo na kiongozi wa bendi, akiwa pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi (CHAMUDATA).

CHANGAMOTO

Anasema moja ya changamoto alizopitia katika safari yake ya muziki ni kuonekana muhuni kutokana na mitazamo ya jamii hasa wanaponengua jukwaani.

Anasema kuna baadhi ya jamaa zake walikuwa wakimponda, lakini alisimamia kile anachokitaka na kufikia ndoto zake. Pia anasema akiwa jukwaani anajiheshimu na kujua mipaka yake kwa heshima ya familia ya Mzee Nyoni.

“Kuna wakati nilikaribia kukata tamaa, lakini nikajiuliza kwa nini nisipambane na kujiamini kwa kipaji nilichonacho na ninashukuru nilipata sapoti kubwa kwa mume wangu kipenzi na kupiga kazi hadi leo hii bila ya hofu,” anasema.

Hata hivyo, Luiza anasema kuna wakati anakumbana na changamoto binafsi kama bindamu na zile za kibiashara, lakini imani yake, nidhamu na mapenzi katika muziki vilimpa nguvu ya kuendelea kupambana bila kukata tamaa.

“Ninamshukuru Mungu kwa kuniweka hai hadi leo, kwani wenzetu wengi tuliokuwa nao wametangulia mbele ya haki, hivyo imani yangu ilinipa nguvu ya kuendelea kufanya kazi bila ya kukata tamaa,” anasema Luiza.

FURSA ALIZOTUMIA

“Kabla ya kuhamia Twanga Pepeta mwaka 1998 kutoka Magoma Moto, sikuwa mzoefu mkubwa, lakini kutua kwangu Twanga Pepeta ilinipatia nafasi ya kujifunza muziki, kupata uzoefu wa kutamba jukwaani na kuibuka kama kiongozi wa kundi lenye mashabiki wengi nchini,” anasema na kuongeza; “Hii kwangu niliona ni fursa na nilipata nafasi ya kushirikiana na wanamuziki wenzangu na kujenga kizingiti cha kufika mbele zaidi kwenye muziki wa dansi.”

Anasema ushirikino huo umemsaidia kuwa Mkurugenzi  wa bendi hiyo, huku akiahidi kuibadilisha na kuipeleka kwa viwango vipya vya mafanikio, akisisitiza mshikamano, nidhamu na ubunifu miongoni mwa wanamuziki.

“Mafanikio yamenifanya kuheshimika kama kiongozi wa muziki wa dansi nchini (CHAMUDATA), pia nimebaki kwenye bendi moja kwa muda mrefu hatua inayochukuliwa kama mfano wa kuigwa, lakini maana halisi ni kuona mashabiki wakifurahia muziki wangu pia.”

Alipuolizwa siri ya kudumu muda mrefu, Luiza anasema amebaini hakuna bendi yenye uwezo na kiuchumi na kimuziki kama Twanga Pepeta na kumwagia sifa Asha Baraka aliyeijengea misingi imara na kusema ndiyo maana kuna wenzao wamekuwa wakihama na kurejea hapo baada ya muda mfupi.

Anasema wanamuziki wanapohama hupoteza mashabiki na wengine kupotea kabisa katika tasnia ya muziki.

“Changamoto zipo kwenye bendi, ila hupaswi kuzikimbia kwa kuwa hazikosekani hata katika nyumba tunazoishi, hiyo ndio siri ya kukaa Twanga Pepeta kwa miaka karibu 30 sasa mfululizo,” anasema Luiza.

MBINU ZILIZOMBEBA

Alipoulizwa ni jambo gani linalompa msukumo wa kuendelea kuwa juu kila siku, anacheka kisha anajibu;

“Msukumo wangu unatokana na kuona kipaji changu cha kuimba na kucheza kinawafurahisha mashabiki wangu wengi, pia kutokata tamaa ya kushindwa kufanya kazi kwa kuambiwa umri umeenda, kwani mwanamuziki anaweza kuendelea kuimba hata akiwa na umri mkubwa, ili mradi awe bado ana nguvu na sauti, mfano kama Bi Kidude alivyoishi na kuimba hadi mauti kumkuta.”

Kuhusu jambo analotamani kuliona katika maisha yake ya muziki, anasema;

“Kuendeleza muziki wangu nikiwa mstari wa mbele wa Twanga Pepeta na ndoto ya kuona bendi hiyo inakua zaidi na kuleta burudani kwa vizazi vipya.”

UJUMBE KWA WANAWAKE

Luiza anawahimiza wanawake wenzake wasiogope kuchagua kazi wanayopenda kufanya, kushikilia nidhamu na kuendelea kujifunza.

“Kuwa na nidhamu na ubunifu ndiyo siri ya mwanamke anayetaka kufanikiwa.”

Kuhusu siku ya Wanawake itakayoadhimishwa duniani kila Machi 8 ya mwaka anasema;

“Siku ya wanawake Duniani ni tukio la kukumbuka nguvu, nidhamu na msukumo wa mwanamke ambaye kwa upande wa muziki, nitumia kuibua hadhi yangu, historia na kuhamasisha wengine kufuata ndoto zao bila kukata tamaa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *