Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameomboleza kifo cha Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliyefariki dunia usiku wa Februari 19, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ich, Kardinali Pengo alifariki dunia saa 4:00 usiku wa Februari 19, 2026 katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu, ambapo taratibu za mazishi zitatangazwa baadaye.

Katika salamu zake za rambirambi leo Februari kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho.

Rais Samia amemtaja Kardinali Pengo kuwa alikuwa kiongozi wa kiroho na mzalendo aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani, maadili, umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia uongozi wake wa muda mrefu ndani ya Kanisa Katoliki.

“Taifa limepoteza kiongozi aliyelitumikia kwa uadilifu na kujitolea. Mchango wake katika malezi ya kiroho na maadili utaendelea kukumbukwa, kuthaminiwa na kuenziwa,” amesema Rais Samia.

Pia, Rais Samia ametuma salamu za pole kwa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), viongozi wa dini pamoja na waumini wote walioguswa na msiba huo.

Aidha, Rais Samia ameungana na Kanisa Katoliki na Watanzania kwa ujumla katika kipindi hiki cha majonzi, akimuomba Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi.

“Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana lihimidiwe,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *