
Arusha. Serikali ameielekeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kuongeza juhudi katika kubuni na kuimarisha teknolojia za kulinda mifumo ya Serikali dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara ya mtandao.
Imebainisha kuwa changamoto kubwa kwa sasa inayokabili nchi ni majaribio ya kushambuliwa mara kwa mara mitandao inayohatarisha usalama wa mifumo ya Serikali.
Hayo yamebainishwa Februari 19, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati akifunga kikao kazi cha sita cha Serikali Mtandao (eGA) kilichofanyika kwa siku tatu jijini Arusha.
Ridhiwani ameeleza hayo wakati ukaguzi wa mifumo ya Tehama kwenye taasisi za Serikali 78 unaonyesha taasisi 42 hazikufanya tathmini za mara kwa mara za udhaifu wa mifumo na majaribio ya usalama, hali iliyoiweka mifumo hiyo kwenye hatari ya mashambulizi ya wadukuzi.
“Taasisi 43 hazikufanya tathmini za usalama wa mtandao mara kwa mara, na taasisi 39 zinaonyesha kuwa na udhaifu katika udhibiti wa utoaji haki za kuingia kwenye mifumo kwa watumiaji wakiwa nje ya mtandao wa taasisi,” inaonyesha sehemu ya ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) iko kwenye hatari zaidi hatari zaidi. Ridhiwani amesisitiza kuwa ni wakati wa wataalamu wa Tehama serikalini kuwekeza zaidi katika utafiti na ubunifu wa teknolojia za kujilinda dhidi ya vitisho vya kimtandao.
“Changamoto kubwa tunayoipata ni mashambulizi ya mara kwa mara ya mtandaoni, niwaombe kupitia kikao hiki, muendelee kusaka na kubuni teknolojia za kulinda mifumo yetu ya ndani isishambuliwe,” amesema Ridhiwani.
Mbali na hilo, amesema kutokana na sekta ya Tehama kubadilika kwa kasi, wataalamu pia wanapaswa kupewa nafasi ya kuendelea kujifunza na kujiendeleza mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
“Elimu haina mwisho, tusipowapa wataalamu wetu fursa ya kuongeza ujuzi, tunaweza kujikuta tunahangaika na teknolojia ya jana huku wenzetu wakiwa hatua nyingi mbele zaidi,” amesema waziri huyo.
Akitolea mfano, Ridhiwani amesema baadhi ya nchi kama Indonesia na Dubai huandaa mashindano maalumu ya kupima uimara wa mifumo yao kwa kuwaalika wataalamu kujaribu kupenya mifumo hiyo ili kubaini upungufu na kuufanyia kazi mapema.
“Na sisi sio mbaya tukaiga mazuri kama haya, anatokea mtaalam wetu anabuni mfumo na akikamilisha mnauweka hadharani na kuruhusu vijana kuuingilia, hii itasaidia kujua uimara wake na njia ya kuzuia endapo utaingiliwa kwa lengo la kujihami,” amesema.
Mbali na hilo, Waziri huyo amesema bado kuna changamoto ya baadhi ya waajiri kutotambua kikamilifu umuhimu wa kuwashirikisha wataalamu wa eGA katika kubuni na kusuka mifumo ya Tehama, hali inayosababisha mamlaka hiyo kuonekana kama “kimbilio la matatizo” pindi changamoto zinapotokea.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba amesema lengo la mkutano huo lilikuwa kubadilishana uzoefu, kujadili mafanikio na changamoto, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa sera, sheria, kanuni, miongozo na viwango vya Serikali mtandao.
Kwa mujibu wa Ndomba, kikao hicho kilijadili jumla ya mada 14 na kuweka maazimio mapya yatakayoongoza hatua zinazofuata katika kuboresha utendaji kazi wa taasisi za umma na utoaji wa huduma kupitia mifumo salama na jumuishi ya Serikali Mtandao.
“Miongoni mwa mada hizo ni changamoto zilizopo kwenye usalama wa mitandao na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua, na kuweka maazimio mapya yatakayotuongoza katika hatua zinazofuata za kuboresha utendaji kazi katika taasisi za umma na utoaji wa huduma za umma kupitia mifumo imara, salama na jumuishi ya Serikali Mtandao,” amesema.
Nje ya mkutano, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Profesa Kenneth Bengesi alisema mashambulizi ya mtandao yanatokea pale ukaguzi wa mara kwa mara usipokuwepo, hivyo kuwashauri wataalamu wa Tehama kufanyia ukaguzi na majaribio ya mara kwa mara mifumo yao.