Ripoti hiyo ya pamoja imetolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Ofisi Jumuishi ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti BINUH.
Kwa mujibu wa ripoti, magenge mengi kati ya 26 yanayofanya kazi nchini humo yanahusika na biashara haramu ya watoto. Watoto hulazimishwa kufanya kazi kama wajumbe, kupeleleza vikosi vya usalama, kukusanya fedha za vitisho, au kushiriki katika vitendo vya uharibifu, utekaji nyara, mauaji yaliyolengwa na ukatili wa kingono.
Mvulana mdogo huko Haiti anafikiria juu ya athari za vurugu za magenge wakati wa uzinduzi wa mpango wa PREJEUNES kuzuia kuajiri watoto.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN, Volker Türk, amesema “Watoto nchini Haiti wananyimwa utoto wao na mustakabali wao. Athari na madhara ya muda mrefu ya biashara haramu ya watoto ni makubwa kwa waathiriwa na familia zao, pamoja na kwa uthabiti wa nchi.”
Ingawa hakuna takwimu kamili za watoto wanaohusishwa, mwaka 2024 UN ilikadiria zaidi ya watoto 500,000 waliishi katika maeneo yaliyodhibitiwa na magenge. Vurugu zimewalazimu zaidi ya watu milioni 1.4 kuyakimbia makazi yao, na zaidi ya nusu yao ni watoto.
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini Haiti, Carlos Ruiz Massieu, akizungumzia ripoti hiyo amesema “Mstakabali wa sasa na wa muda mrefu wa Haiti unategemea ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka za kitaifa na washirika wao wa kimataifa ili kujenga jamii imara na mifumo madhubuti ya ulinzi wa kijamii. Watoto lazima wawe kiini cha mwitikio wetu kwa mzozo wa usalama nchini Haiti,”
Ripoti inaeleza kuwa umaskini, taasisi dhaifu, kutengwa kijamii na vurugu za silaha vinaongeza hatari kwa watoto, hasa wale wa familia maskini, wanaoishi mitaani au katika makazi ya wakimbizi wa ndani. Baadhi huvutiwa na ahadi ya mamlaka au ulinzi, huku wengine wakishawishiwa kwa vitisho, njaa au dawa za kulevya.
Pia inaonya kuwa hatua zilizopo hazitoshi na mara nyingi watoto waliotumikishwa hutazamwa kama wahalifu badala ya waathiriwa, huku wengine wakiripotiwa kuuawa kiholela.