
London. Bukayo Saka ameingia na kupaa hadi nafasi ya tano katika orodha ya nyota 10 wa Ligi Kuu England (EPL) wanaoongoza kwa kulipwa mishahara mikubwa zaidi kufuatia mkataba mpya ambao amesaini na Arsenal mwanzoni mwa wiki hii.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24, amesaini mkataba mpya wa miaka mitano utakaomuweka klabuni hapo hadi 2031 utakaomfanya alipwe kiasi cha Pauni 300,000 (Sh1.04 bilioni) kwa wiki.
Kiasi hicho kinamfanya Saka awe ndio mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye kikosi cha Arsenal akimpiku Kai Havertz ambaye analipwa kiasi cha Pauni 280,000 (Sh971 milioni) kwa wiki.
Awali, Bukayo Saka alikuwa akilipwa kiasi cha Pauni 195,000 (Sh677 milioni) kwa wiki katika mkataba wake uliopita wa miaka minne kabla ya huu ambao alisaini mwaka 2023.
Mshahara wa awali, ulimfanya Saka asiwepo katika orodha ya nyota 10 wanaolipwa zaidi katika Ligi Kuu England lakini sasa amepanda hadi katika nafasi ya tano.
Kinara wa chati hiyo ni nyota wa Manchester City, Erling Haaland ambaye kwa wiki anapokea kiasi cha Pauni 525,000 (Sh1.8 bilioni) kwa wiki.
Na kiwango hicho cha mshahara kwa Haaland kinaonekana hakipati kwa upendeleo kwani amekuwa na kiwango bora na anatoa mchango mkubwa kwa timu hiyo tangu alipojiunga nayo mwaka 2022 akitokea Borussia Dortmund.
Haaland akiwa na Man City, ameweka rekodi ya kufunga idadi kubwa ya mabao ndani ya msimu mmoja ambayo ni 36 lakini pia ndiye mchezaji aliyefikisha kwa haraka zaidi mabao 100 katika EPL akifanya hivyo kwenye mechi 111.
Msimu huu tayari Haaland ameshapachika mabao 22 katika mechi 26 za Ligi Kuu England na ndiye kinara wa kufumania nyavu.
Orodha ya nyota 10 wanaolipwa mishahara mikubwa Ligi Kuu England
1. Erling Haaland- Pauni 525,000 (Sh1.8 bilioni)
2. Mohamed Salah (Liverpool)- Pauni 400,000 (Sh1.4 bilioni)
3. Casemiro (Man United)- Pauni 350,000 (Sh1.2 bilioni)
4. Virgil van Dijk (Liverpool)- Pauni 350,000 (Sh1.2 bilioni)
5. Bukayo Saka (Arsenal)- Pauni 300,000 (Sh1.04 bilioni)
6. Bruno Fernandes (Man United)- Pauni 300,000 (Sh1.04 bilioni)
7. Omar Marmoush (Man City)- Pauni 295,000 (Sh1.02 bilioni)
8. Alexander Isak (Liverpool)- Pauni 280,000 (Sh971 milioni)
9. Kai Havertz (Arsenal)- Pauni 280,000 (Sh971 milioni)
10. Gabriel Jesus (Arsenal)- Pauni 265,000 (Sh919 milioni).