Dar es Salaam. Benki ya Stanbic Bank Tanzania kwa kushirikiana na Uwezo Tanzania wamezindua mpango wa kuanzisha maktaba katika shule za msingi 45 za Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe, ili kuboresha upatikanaji wa vitabu na vifaa vya kujifunzia vinavyoendana na mtaala mpya wa taifa.
Mpango huo unahusisha ujenzi na uanzishaji wa maktaba za shule pamoja na ugawaji wa vitabu vya hadithi na rasilimali za kielimu kwa wanafunzi na walimu, ukiwa na lengo la kukuza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, kuongeza ushiriki wa wanafunzi darasani na kuimarisha elimu msingi katika ngazi ya jamii.
Kupitia mpango wa My Village, Uwezo Tanzania inaunga mkono maktaba za jamii kwa kutoa vitabu vinavyoendana na mtaala wa taifa, hatua inayokwenda sambamba na Mpango wa Kitaifa wa Maendeleo ya Elimu wa KKK uliozinduliwa Januari 29, 2026 na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mpango huo unalenga pia kuimarisha ufuatiliaji na uungaji mkono wa elimu ya msingi kwa watoto katika jamii.
Fedha za Stanbic Bank Tanzania zitagharamia ununuzi wa vitabu vya mtaala na ziada, ambapo takribani watoto 33,619 wanatarajiwa kunufaika kila mwaka kwa kipindi cha miaka 10 hadi 20.
Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa benki hiyo, Dickson Senzi, amesema ushirikiano huo unaakisi uwekezaji wa kijamii unaolenga miradi yenye matokeo yanayopimika na yenye kugusa mahitaji halisi ya jamii.
Katika utekelezaji wake, Uwezo Tanzania inashirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), Maktaba ya Taifa ya Tanzania na wachapishaji wa Mkuki na Nyota kuhakikisha upatikanaji wa vitabu bora na vinavyoendana na mtaala.
Mbali na uanzishaji wa maktaba, walimu watapatiwa vijitabu vya mbinu za kufundisha kusoma, kuandika na kuhesabu, huku mahudhurio ya maktaba yakirekodiwa kwa utaratibu maalum. Walimu pia watahamasishwa kuchangia vitabu vya ziada vilivyopo shuleni ili kuongeza rasilimali za maktaba.
Hatua hiyo inatarajiwa kuboresha matokeo ya elimu ya msingi, kukuza utamaduni wa kusoma na kuendeleza ubunifu na fikra pevu kwa wanafunzi, huku Uwezo Tanzania ikisisitiza dhamira ya kuhakikisha upatikanaji wa haki wa rasilimali bora za elimu kwa watoto kote nchini.