
Unguja. Baada ya kufanya tathmini ya miradi inayotekelezwa na wajasiriamali waliopata mikopo ya bei nafuu inayotolewa na Serikali, imebainika kwamba miradi ya sekta ya kilimo na uzalishaji haikuleta tija na kufikia malengo ya utoaji wa mikopo hiyo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa, miradi ya wajasiriamali iliyotoa tija zaidi ni ile iliyopo katika sekta ya biashara na utengenezaji wa bidhaa za mikono.
Hayo yamebanishwa leo Februari 20, 2026, wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika Mkutano wa Pili wa Baraza la 11 la Wawakilishi, ambapo mwakilishi wa Chakechake (CCM), Abdulwahab Said Abubakar, alipohoji iwapo Serikali imefanya tathmini ya kubaini ni kwa kiasi gani wananchi wameweza kunyanyuka kiuchumi kupitia fursa hii ya uwezeshaji wa Serikali.
Pia alihoji kuhusu eneo gani la miradi ya ujasiriamali ambalo limetoa tija zaidi na miradi ipi ambayo haikufikia malengo yaliyokusudiwa.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Hassan Khamis Hafidh, amesema miradi ambayo haikufikia malengo yaliyokusudiwa kwa kiasi kikubwa ni ile ya sekta ya kilimo na uzalishaji. Kutofikia tija kwa miradi hiyo kumesababishwa na utaalamu mdogo wa wajasiriamali katika shughuli za kilimo na sekta ya uzalishaji.
“Changamoto ya miundombinu, ikiwemo umeme wa uhakika na gharama kubwa za uzalishaji wa bidhaa,” amesema Hafidh.
Wizara, kupitia Wakala wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi (ZEEA), na kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, ilifanya tathmini kwa lengo la kutambua athari za mikopo nafuu iliyotolewa katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Tathmini hiyo ilifanyika Septemba 2023, ambapo jumla ya Sh18.036 bilioni zilikuwa zimeshatolewa kwa wanufaika 18,854.
Tathmini ilibaini ukuaji wa biashara kwa asilimia 83 ya wanufaika. Aidha, asilimia 21 ya wanufaika walitengeneza ajira moja hadi tano za moja kwa moja, na asilimia 25 walitengeneza ajira moja hadi tano zisizo za moja kwa moja tangu walipopokea mikopo.
Amesema tathmini nyingine imepangwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2026/27.