Bofya hapa kutazama ramani inayoonesha maeneo husika.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR) imetoa ripoti mpya inayoanika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya mamia ya maelfu ya watu waliosafirishwa kwa hila kufanya kazi katika vituo vya utapeli, hasa Kusini-Mashariki mwa Asia na maeneo mengine duniani.
Waathirika wanatoka maeneo gani?
Taarifa iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi inanukuu ripoti hiyo ikieleza kuwa kati ya mwaka 2021 na 2025, waathirika kutoka nchi za Bangladesh, China, India, Myanmar, Sri Lanka, Afrika Kusini, Thailand, Viet Nam na Zimbabwe walisafirishwa kwenda vituo vya utapeli vilivyoko Cambodia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Lao, Myanmar, Ufilipino na Falme za Kiarabu (UAE).
Shughuli hizo pia zimeripotiwa kuenea katika eneo la Mekong, baadhi ya visiwa vya Pasifiki, Asia Kusini, nchi za Ghuba, Afrika Magharibi na Amerika.
Kituo cha kazi katika kituo cha utapeli nchini Kambodia kimetelekezwa kufuatia uvamizi wa polisi.
Ahadi za uongo
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, waathirika walivutwa kwa ahadi za kazi halali mtandaoni, lakini walilazimishwa kushiriki katika ulaghai wa kimtandao ukiwemo utapeli wa kujifanya watu wengine, ulaghai wa kimapenzi, na udanganyifu wa kifedha.
Wengi walifungiwa katika majengo makubwa yenye ulinzi mkali, uzio wa waya wenye miiba na walinzi wenye silaha.
Zahma za mateso ikiwemo utoaji wa mimba
Ripoti inabainisha mateso makubwa yaliyowapata waathirika, yakiwemo kuteswa, kunyimwa chakula, kufungiwa peke yao, unyanyasaji wa kingono, utoaji mimba wa kulazimishwa na adhabu kali kwa wanaojaribu kutoroka.
Baadhi walilazimishwa kushuhudia au kutekeleza mateso dhidi ya wenzao ili kutii amri. Pia, familia zao zilipigiwa simu za video kuoneshwa mateso ili kushinikizwa kutoa fedha za kuwakomboa au kikombozi.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN, Volker Türk, amesema ukatili huo “unashtua na kuvunja moyo,” akisisitiza kuwa badala ya waathirika kupata ulinzi na haki, mara nyingi hukumbana na unyanyapaa na hata adhabu zaidi.
Nini kifanyike?
Ripoti inapendekeza nchi husika kuimarisha sheria za kupambana na usafirishaji haramu wa watu kwa kutambua wazi dhana ya “uhalifu wa kulazimishwa” na kuhakikisha waathirika hawaadhibiwi kwa makosa waliyolazimishwa kuyatenda.
Pia inataka operesheni za uokoaji ziwe za haraka, salama na zenye uratibu, kuheshimiwa kwa kanuni ya kutowarejesha watu katika hatari, pamoja na huduma za matibabu na msaada wa kisaikolojia.
Ripoti hiyo pia inapendekeza kuanzishwa kwa njia salama na halali za uhamiaji wa kazi, pamoja na usimamizi madhubuti wa matangazo ya kazi mtandaoni ili kuzuia ajira za ulaghai.
Soma ripoti nzima hapa