Dar es Salaam. Katika jamii yetu, kufunga ni sehemu ya maisha kwa misingi ya imani za dini na hata sababu za kiafya. Waislamu hufunga katika mwezi wa Ramadan, huku Wakristo wakitekeleza ibada ya Kwaresma.

 Hata hivyo, wataalamu wanasema bado kuna mkanganyiko mkubwa kati ya kushinda njaa na kufunga kwa kuzingatia kanuni sahihi za lishe.

Ofisa mtafiti mwandamizi wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, TFNC, Maria Ngilisho anasema kufunga ni kitendo cha kujizuia kula na kunywa kwa muda maalumu kwa lengo la kiimani au kiafya.

Anasema wakati wa kufunga mwili hutumia sukari iliyopo kwenye damu na akiba ya chakula kilichohifadhiwa, hasa mafuta, kama chanzo cha nishati. 

Hali hiyo huchangia kupunguza uzito uliozidi na kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za afya, kufunga kunapofanyika kwa usahihi huleta faida za kimwili na kisaikolojia. Husaidia kuboresha afya ya moyo na mishipa ya damu, kurekebisha kiwango cha lehemu mwilini na hata kuimarisha utendaji wa ubongo. 

Hata hivyo, anatahadharisha kuwa kufunga bila mpangilio sahihi wa lishe, kunaweza kusababisha maumivu ya tumbo, kuumwa kichwa na kukosa utulivu.

Umuhimu wa mlo kamili wakati wa kufuturu

Ngilisho anasema changamoto kubwa inayojitokeza katika familia nyingi ni kuandaa vyakula vya futari vinavyotokana zaidi na kundi moja la chakula, hasa nafaka na vyakula vya wanga, huku mbogamboga na matunda vikipewa nafasi ndogo au kutozingatiwa kabisa.

Anaeleza kuwa baada ya kufungua ni muhimu kula mlo kamili unaojumuisha makundi yote ya chakula ili kuupa mwili virutubishi vinavyohitajika kwa ajili ya kuupa nguvu, kuujenga, kuukarabatI na kuupa kinga dhidi ya maradhi. 

Mlo kamili huupatia mwili wanga, protini, mafuta, vitamini na madini kwa uwiano unaotakiwa.

“Makundi ya chakula yanayoshauriwa ni pamoja na nafaka na mizizi yenye wanga kama mahindi, mchele na viazi; vyakula vya asili ya wanyama kama nyama, samaki, mayai na maziwa; vyakula vya jamii ya kunde na karanga kama maharage na dengu; matunda; mbogamboga za majani na za matunda; pamoja na mafuta ya mimea yanayotumika kwa kiasi, ” anasema.

Anashauri kuwa makundi hayo yanaweza kugawanywa kati ya futari na daku, lakini angalau makundi manne yajumuishwe katika mlo mmoja. Pia anasisitiza umuhimu wa kula kwa utaratibu na kuepuka kula kwa wingi kupita kiasi mara tu baada ya kufungua.

Tahadhari kwa vyakula vya mafuta na sukari nyingi

Mtaalamu huyo anaonya dhidi ya tabia ya kuandaa futari zenye mafuta na sukari nyingi kama vyakula vya kukaanga, juisi zenye sukari iliyoongezwa na vyakula vilivyosindikwa. 

Anasema vyakula hivyo huongeza nishati kupita kiasi mwilini na kusababisha kuongezeka uzito kwa haraka, hali inayoongeza hatari ya kupata kisukari, magonjwa ya moyo na hata baadhi ya saratani.

Anashauri mfungaji aanze kufungua kwa vitu vya majimaji kama maji, supu nyepesi au maji ya madafu ili kuurudishia mwili maji yaliyopotea. 

“Tende pia zinaweza kutumika kwa kiasi kwa kuwa zina sukari asilia inayorudisha nguvu haraka,” anaeleza.

Aidha, anasisitiza umuhimu wa kunywa maji ya kutosha kati ya futari na daku ili kusaidia mmeng’enyo wa chakula, usafirishaji wa virutubishi mwilini na utendaji mzuri wa viungo vya mwili.

Kwa ujumla, anasema kufunga ni ibada yenye manufaa makubwa kiafya iwapo itafanywa kwa uangalifu na kwa kuzingatia kanuni sahihi za lishe. Kupanga mlo kamili, kunywa maji ya kutosha na kupunguza vyakula vyenye mafuta, sukari na chumvi nyingi ni hatua muhimu za kuhakikisha kipindi cha kufunga kinakuwa chanzo cha afya badala ya maradhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *