Dar es Salaam. Mwezi wa Ramadhani unapowadia, mamilioni ya Waislamu duniani huingia katika kipindi cha ibada, toba na kujitathmini kiroho.

Ni mwezi wa kujinyima na kujidhibiti kwa ajili ya kumridhisha Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, kwa watu wanaoishi na kisukari, mwezi huu huibua mjadala mzito kuhusu usalama wa afya zao wanapofunga.

Wapo wanaoamini kuwa kufunga ni ishara ya imani thabiti, hivyo husita kutafuta ushauri wa kitabibu kwa hofu ya kuonekana dhaifu kiimani.

Wengine, kwa upande wao, huogopa madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kubadilika kwa ratiba ya kula na kunywa. Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa kulinda maisha ni msingi muhimu katika dini, na mgonjwa haruhusiwi kujidhuru kwa namna yoyote.

Katika mafundisho ya Uislamu, mtu mwenye ugonjwa unaoweza kuathiriwa na kufunga anaruhusiwa kutofunga na badala yake kutoa fidia au sadaka.

Hivyo basi, mtu mwenye kisukari anashauriwa kumwona daktari pamoja na mtaalamu wa lishe ili kupima hali yake na kupata mwongozo sahihi. Ushauri huo ni muhimu hasa kwa wale wanaotumia insulin au dawa zinazoweza kushusha sukari kwa haraka, kwani wako katika hatari ya kupatwa na kushuka kwa sukari wakati wa mchana.

Mabadiliko ya muda wa kula yana athari ya moja kwa moja kwenye kiwango cha sukari mwilini. Kutokula kwa muda mrefu kunaweza kufanya sukari ishuke kupita kiasi, huku kula vyakula vingi au vyenye sukari nyingi wakati wa futari kukisababisha kupanda kwa kasi.

 Aidha, kukosa maji mwilini wakati wa mchana kunaweza kuathiri figo na kuongeza hatari ya matatizo mengine, hususan kwa wagonjwa wenye kisukari cha muda mrefu au wale waliokwishapata athari za ugonjwa huo.

Wataalamu wanaeleza kuwa si kila mgonjwa wa kisukari amekatazwa kufunga. Wale ambao hali zao zimedhibitiwa vizuri na hawana matatizo makubwa ya ziada wanaweza kufunga chini ya uangalizi wa karibu wa daktari. Hata hivyo, wagonjwa wenye kisukari kisichodhibitiwa, wenye matatizo ya figo au athari nyingine nzito, wanashauriwa kutofunga kabisa ili kuepusha madhara.

Kwa wale wanaoruhusiwa kufunga, maandalizi ya mapema ni jambo la msingi. Daktari anaweza kurekebisha dozi ya dawa au insulin kulingana na ratiba ya daku na futari. Kupima sukari mara kwa mara ni muhimu na hakuvunji swaumu, kwani husaidia kubaini mapema hatari ya kupanda au kushuka kwa sukari.

Lishe bora wakati wa daku na futari inapendekezwa, ikijumuisha mboga, protini na nafaka zisizokobolewa, huku vyakula vyenye sukari nyingi vikiepukwa. Iwapo kiwango cha sukari kitashuka au kupanda kupita kiasi, mgonjwa anapaswa kuvunja swaumu mara moja kwa ajili ya usalama wake.

Ramadhani si kufunga pekee bali ni mwezi wa ibada kwa upana wake. Mtu mwenye kisukari anaweza kushiriki kikamilifu katika ibada nyingine kama kuswali, kusoma Qur’an, kutoa sadaka na kusaidia wahitaji hata kama hatofunga. Uislamu umeweka urahisi kwa mgonjwa na haukusudii kumletea madhara.

Wakati huohuo, wataalamu wa afya wanaonya kuwa hata watu wasio na kisukari wanapaswa kuwa waangalifu na ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi wakati wa futari. Ulaji wa sukari kupita kiasi husababisha kupanda kwa haraka kwa kiwango cha sukari kwenye damu na kuilazimisha miili kutoa insulin nyingi.

Hali hii ikijirudia kila siku kwa mwezi mzima inaweza kuongeza uzito na hatari ya kupata kisukari cha aina ya pili, hasa kwa wenye uzito mkubwa au historia ya ugonjwa huo katika familia.

Kwa ujumla, Ramadhani ni mwezi wa baraka na rehema, lakini pia ni mwezi wa busara. Kuchukua tahadhari za kiafya ni sehemu ya wajibu wa kulinda uhai na afya, ambavyo ni amana muhimu kwa kila mwanadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *