MBIO za kuwania kupanda Ligi Kuu Bara zinazidi kunoga wakati Ligi ya Championship ikiendelea tena wikiendi hii, na kesho Jumapili zitapigwa mechi saba na moja Jumatatu kuhitimisha raundi ya 19, huku ushindani ukizidi kwa vigogo vinavyowania nafasi za juu.
Kwenye Uwanja wa Amani uliopo Njombe, wenyeji Hausung waliochapwa bao 1-0 na Mbuni ya Arusha, watakuwa wanajiuliza mbele ya Gunners ya Dodoma yenye kumbukumbu pia ya kuchapwa 1-0 na African Sports ya Tanga.
Timu hizo zinakutana zikiwa zote zinacheza Championship kwa mara ya kwanza msimu huu na Hausung iliongoza Ligi Daraja la Kwanza kundi A na pointi 25, huku Gunners ikiongoza kutokea kundi B na pointi 35.
Baada ya timu hizo kuongoza makundi na kupanda Championship, zilicheza fainali kusaka bingwa mpya wa First League 2024-2025, ambapo kikosi cha Gunners kilitwaa ubingwa baada ya kuifunga Hausung mabao 3-0.
Vinara wa Ligi, Geita Gold wenye pointi 46 baada ya kuifunga Mbeya Kwanza mabao 2-1 watakuwa na kibarua cha kupambana na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi, waliotoka kuifunga Stand United ‘Chama la Wana’ mabao 2-0.
Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025 wa Ligi ya Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara baada ya kufeli mechi za ‘play-off’.
Timu hiyo ilicheza ‘play-off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya sare nyumbani ya 2-2 kisha kuchapwa ugenini 2-0.
Polisi haikuwa na msimu mzuri 2024-2025, baada ya kumaliza nafasi ya 10 katika Ligi ya Championship na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13 na safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25, kufuatia kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
Mbeya Kwanza iliyochapwa mabao 2-1 dhidi ya Geita Gold, itaikaribisha Transit Camp iliyoichapa Songea United mabao 3-1, huku Bigman iliyofungwa na Kagera Sugar mabao 2-0 ikicheza na Barberian inayoburuza mkiani mwa msimamo na pointi tisa.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, African Sports itaikaribisha Kagera inayoshika nafasi ya pili na pointi 43, huku TMA iliyolazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya B19 FC, itacheza na KenGold iliyotoka kuichapa Barberian FC 2-0.
Baada ya msimu bora wa 2023-2024, mashabiki na wapenzi wa soka hususani wa jijini Mbeya walitarajia KenGold ingeendeleza ilichokifanya katika Ligi ya Championship, japo baada ya kupanda daraja mambo yalikuwa ni tofauti na kurejea ilipotoka.
Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, iliyorejea Ligi Kuu baada ya miaka 21, tangu iliposhuka mwaka 2001.
Licha ya kiwango hicho bora, ila KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu na msimu wa 2024-2025, iliburuza mkia na pointi 16, ikishinda mechi tatu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza ya 15 na pointi 23.
Mechi ya mwisho kwa kesho Jumapili itapigwa Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga na wenyeji Stand United yenye kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-0 na Polisi Tanzania, itaikaribisha B19 FC, iliyotoka sare ya bao 1-1 na TMA FC.
Raundi ya 19, itahitimishwa keshokutwa Jumatatu kwa mechi moja kupigwa kwenye Uwanja wa Majimaji Ruvuma na Songea United iliyochapwa uwanjani hapo mabao 3-1 na Transit Camp itaikaribisha Mbuni FC iliyoifunga Hausung FC bao 1-0.
Akizungumzia mwenendo wa ligi hiyo, Kocha wa African Sports, Khalid Adam amesemamechi zote kwa sasa ni ngumu kutokana na mahitaji ya kila timu bila kujali sehemu wanayocheza, jambo linaloongeza mvuto na ushindani.
“Tayari kuna timu zinapiga hesabu ya kumaliza nafasi nne za juu, nyingine zinataka kuendelea kubakia na zipo pia ambazo zinapambana zisishuke daraja, kwa hali ya namna hiyo maana yake ushindani unakuwa mkubwa kwa kila mechi,” amesema Adam.