Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, “Vyombo vya kidiplomasia (vya Iran) lazima vichore ramani yake ya mazungumzo kwa njia sahihi, ya uwazi na ufasaha, kwa kuzingatia kanuni za heshima, uwazi na hekima, na kuchukua hatua za ujasiri na imara katika njia hii.”

Hujjatul Islam Sayyid Mohammad Hassan Abu Torabi Fard, amesema hayo kwenye khutba za leo za Swala ya Ijumaa iliyosaliwa hapa Tehran, ambapo ameashiria mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani na kusema: “Mazungumzo haya ni mojawapo ya masuala muhimu ambayo yameathiri anga ya kisiasa ya dunia, eneo hili (la Asia Magharibi), na nchi za dunia.”

Amesema: Mkakati ulioamuliwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu umewezesha uwepo mzuri na wenye mamlaka wa vyombo vya kidiplomasia katika uwanja wa maingiliano ya kimataifa na kikanda, na mkakati huu unategemea kanuni tatu; izza, hekima, na maslahi ya taifa.

Ameashiria umuhimu wa sera za kigeni na kusema: Mojawapo ya maeneo muhimu ya uongozi ni sera za kigeni. Kuanguka kwa mamlaka ya ulimwengu wa Kiislamu baada ya Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia kulisababisha nchi za Kiislamu kuwa ndogo na kuwa mateka wa mafundisho ya kimataifa ya uliberali, ubepari, ujamaa na nguvu za Magharibi.

Hujjatul Islam Sayyid  Abu Torabi Fard amesema, “Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kwamba vyombo vya kidiplomasia vya nchi hii lazima vioanishe heshima, mamlaka, na hekima. Mambo haya lazima yatumikie maslahi ya nchi, taifa la Iran, na Umma wa Kiislamu.”

Sayyid Abu Torabifard ameyataja Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kama njia iliyoleta usawa na mabadiliko katika mahusiano ya kigeni, na kuinua hadhi ya Iran na mataifa ya eneo hili.

Akitoa salamu za pongezi kwa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani, Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amebainisha kuwa: Ramadhani ni mwezi wa ukamilifu na ubora kwa mtu binafsi na jamii. Amesema mtu anayetafuta ukweli na ana kiu ya kuupata ukweli huo, basi atapata furaha na saada, kama Alivyoahidi Mwenyezi Mungu.

Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa Tehran ameeleza kuwa, njia ya umoja inamaanisha kuwaongoza watu kwenye barabara zinazokidhi mahitaji yao ya kidunia na ya Akhera, akiongeza kwa kusema: “Njia ya kimaanawi inapasa kuambatana na ustawi, utukufu, na usalama.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *