ZANZIBAR: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amewataka wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu Zanzibar kuwa mstari wa mbele kulinda, kuuenzi na kuutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Masauni ametoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa Kongamano kuhusu muungano kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Februari 19, 2026.

Amesema vijana ni nguvu kazi na ni tumaini la taifa, hivyo wanawajibu kuhakikisha urithi wa amani na upendo ulioasisiwa na waasisi wa taifa unaendelea kudumu.

Amesema kongamano hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Aprili 23, 2024 wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ambapo alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya muungano kwa makundi mbalimbali ya jamii, hususan vijana.

“Idadi kubwa ya Watanzania ni vijana waliozaliwa baada ya Muungano, hivyo ni muhimu wapate uelewa mpana kuhusu historia, misingi na manufaa yake ili wawe mabalozi wazuri wa kuulinda,” amesema Masauni.

Masauni amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Julius Nyerere na Abed Amani Karume, umeendelea kudumu kwa zaidi ya miaka 61, ukiwa nguzo ya amani na utulivu nchini.

“Uzalendo si maneno pekee bali ni matendo. Vijana mnapaswa kusuluhisha migogoro kwa mazungumzo, kuheshimu maoni tofauti, kupinga rushwa, kulipa kodi kwa uaminifu na kulinda rasilimali za taifa,” amesisitiza.

“Serikali iko tayari kushirikiana na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kuhakikisha Muungano unaendelea kuwa msingi wa kudumisha amani, utulivu na maendeleo kwa kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Suleiman Masoud Makame amesema kongamano hilo limewezesha kupata maarifa na uelewa zaidi kuhusu upekee wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Tukiwa na uelewa pana kuhusu wajibu kama vijana wa taifa, na kwamba nmakwenda kutumia maarifa na uzoefu mlioupata katika kuendeleza misingi ya muungano ya amani, utulivu na mshikamano,” amesema,”Makame.

Amesema kongamano hilo litasaidia kuongeza uelewa kuhusu mafanikio yaliyopatikana tangu kuasisiwa kwa Muungano, changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wake, pamoja na malengo na dira ya kuudumisha na kuuenzi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.]

Naye, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Zanzibar (SUZA), Juma Omar Nkwede amesema kongamano hilo limekuja wakati sahihi kwao kwa kuwapa elimu ya historia kuhusu taifa.

Amesema elimu waliyoipta imezidi kuwa msingi imara juu ya kuendelea kutetea muungano kwa kujua misingi ambayo imewekwa na waasisi kwa maslahi mapana ya nchini kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *