
Ujumbe wa kutafuta ukweli wa Umoja wa Mataifa umesema ukatili uliofanywa na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF wakati wa kuutwaa mji wa El-Fasher huko Darfur Magharibi nchini Sudan mwezi Oktoba mwaka jana, una “alama za mauaji ya kimbari” dhidi ya jamii za Zaghawa na Fur.
Ripoti iliyotolewa jana Alkhamisi na Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Kutafuta Ukweli Sudan imesema ushahidi waliokusanya unathibitisha kwamba, angalau vitendo vitatu vya msingi vya mauaji ya halaiki vilitokea, ikibainisha kwamba wanamgambo wa RSF walifanya mauaji yaliyochochewa kikabila, ukatili mkubwa wa kijinsia na kuwafurusha watu kwa nguvu katika eneo la Darfur nchini Sudan.
“Kuwaua wanachama wa kundi la kikabila; kuwasababisha madhara makubwa ya mwili na kisaikolojia; na kuwasababisha kwa makusudi hali ngumu ya maisha ni alama za mauaji ya kimbari,” imesema sehemu moja ya ripoti hiyo.
Mohamed Chande Othman, Mwenyekiti wa ujumbe huo, amelituhumu kundi la waasi la RSF na washirika wake “wanamgambo wa Kiarabu” – kwa kufanya uhalifu mkubwa ikiwa ni pamoja na mauaji, mashambulizi ya makusudi na ya kiholela dhidi ya raia, utumiaji wa njaa kama silaha ya vita, pamoja na ukatili wa kingono, uporaji na kuwasajili watoto kama wapiganaji vitani huko El-Fasher.
Wiki iliyopita, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema kwamba, uhalifu unaofanywa na wapiganaji wa kundi la RSF huko El-Fasher nchini Sudan ni sawa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN imeeleza kwamba, nyaraka za uhalifu huo zimetegemea mahojiano yaliyofanywa na zaidi ya waathiriwa 140 na mashahidi katika Jimbo la Kaskazini mwa Sudan na mashariki mwa Chad, mwishoni mwa mwaka 2025, ikibainisha kuwa zaidi ya watu 6,000 waliuawa katika siku tatu za kwanza za shambulio la RSF huko El Fasher, baada ya mji huo kuzingirwa na waasi hao.