DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Tanzania Health Summit (THS) limewataka watoa huduma za afya na vituo vya afya nchini kufanya tathmini ya ubora wa huduma wanazozitoa ili kuboresha utoaji wa huduma katika vituo vyao na kufikia viwango vya kimataifa.
Wito huo ulitolewa na Rais wa THS, Dk Omary Chillo, katika hafla ya kukabidhi cheti cha ubora cha SafeCare ngazi ya nne kwa Kituo cha Afya cha Qualitas kilichopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Chillo alisisitiza umuhimu wa watoa huduma na vituo vya afya kufanya tathmini za mara kwa mara ili kubaini mapungufu yaliyopo na kuyafanyia kazi kwa lengo la kufikia viwango vinavyotakiwa.
Alieleza kuwa ubora unapaswa kuzingatiwa katika hospitali na vituo vyote vya afya, bila kujali tofauti ya huduma wanazotoa.
“Ubora unatakiwa uzingatiwe katika hospitali na vituo vyote vya afya. Siyo kwamba hospitali moja iwe bora zaidi kuliko nyingine, huduma zinaweza kutofautiana lakini ubora unapaswa kuwa uleule,” alisema Dk Chillo.

Akieleza hayo alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya katika kufikia utoaji wa huduma bora kuwa ni pamoja na udhaifu katika utawala, miundombinu isiyokidhi mahitaji kama majengo na vifaa, pamoja na utendaji wa wafanyakazi kuwa chini ya kiwango.
Alidai changamoto hizo zinayochangia kukosekana kwa taratibu za uendeshaji, Akiongeza kuwa THS wana jukumu la kuchambua changamoto hizo na kuvishauri vituo vya afya namna ya kuboresha maeneo yenye mapungufu.
Lengo lao ni kuzifikia taasisi na vituo mbalimbali vya afya katika mikoa yote ya Tanzania na kuhamasisha maboresho ya huduma kwa ujumla.
Kuhusu SafeCare, Dkt Chillo alieleza kuwa ni programu inayofanya tathmini ya ubora wa utoaji huduma katika hospitali, zahanati, vituo vya afya na kliniki nchini ambayo inatekelezwa katika mataifa mbalimbali kwa zaidi ya miaka kumi na imekuwa chachu ya kuimarisha huduma za afya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali ya Qualitas, Dk Jane Manyahi aliwashauri watoa huduma wa sekta binafsi kujiunga na mifumo ya kujipima ubora wa huduma wanazotoa.
Pia aliishauri hospitali za umma na binafsi kuzingatia viwango vya kimataifa ili kutoa huduma salama na zenye ubora akibainisha kuwa kufuata viwango kunasaidia watumishi kufanya kazi katika mazingira bora na salama, jambo linaloongeza uaminifu kwa wagonjwa na jamii kwa ujumla.
“Ni jambo jema kwani linaongeza imani kwa jamii inayowazunguka, wakijua kuwa huduma wanazopata ni salama na bora,” alisema Dk Manyahi.
Alieleza furaha yao kupokea cheti cha ubora cha nyota nne, akisema ni hatua kubwa katika juhudi zao za kuhakikisha wanatoa huduma salama na kuokoa maisha ya wagonjwa.
Naye mkazi wa Kigamboni, Esther Medson, aliyefika hospitalini hapo kupata huduma, alisema ameridhishwa na huduma alizopata na kuipongeza hospitali hiyo kwa kustahili cheti cha ubora wa ngazi ya juu.
Pia alizitaka taasisi za sekta ya afya kuendelea kuwahudumia wagonjwa kwa weledi na kutumia taaluma zao ipasavyo ili kuboresha zaidi huduma wanazotoa.