Tanga. Wanafunzi wa darasa la tano na sita katika Shule ya Msingi Ziwani, iliyopo Kata ya Pongwe, jijini Tanga, wanalazimika kukaa kwenye mikeka darasani wakifuatilia masomo yao kutokana na uhaba wa madawati unaoikumba shule hiyo.

Chanzo cha kuaminika kutoka katika shule hiyo, kimesema changamoto hiyo ilianza mwaka jana kufuatia ongezeko kubwa la wanafunzi wanaohamia kutoka maeneo mbalimbali.

“Tatizo hili linawahusu wanafunzi wa darasa la tano na sita pekee. Limeanza mwaka jana baada ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaohamia,” kimeseme chanzo hicho.

Amefafanua kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,400, hali iliyosababisha msongamano katika baadhi ya madarasa.
“Ongezeko hili limetokana na wakazi wapya kuhamia Pongwe na kuwaleta watoto wao hapa shuleni. Tunashughulikia tatizo hilo kwa kushirikiana na mamlaka husika,” ameongeza.
Mtendaji wa Kata ya Pongwe, Vuai Shame amekiri kuwepo kwa uhaba wa madawati lakini akasisitiza kuwa serikali tayari imelipokea na inalifanyia kazi suala hilo.
“Taarifa tulishaziwasilisha kwa Mkurugenzi tangu mwezi wa kumi mwaka jana na shule imeingizwa kwenye mpango wa kupatiwa madawati,” amesema Shame.
Amesema wadau mbalimbali wameahidi kusaidia na matarajio ni kwamba madawati mapya yatawasili ndani ya mwezi huu.
“Hatuwezi kuwazuia wanafunzi kujiandikisha kwa sababu ni haki yao, lakini hilo linaongeza changamoto ya miundombinu kama madawati na madarasa,” ameeleza.
Akizungumzia hali ya jumla ya shule za msingi jijini humo, Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu wa Jiji la Tanga, Leen Chamba, alisema halmashauri ina uhaba wa madawati 1,864.
“Kwa wastani tunahitaji madawati 1,864 kwa ajili ya wanafunzi zaidi ya elfu sitini katika shule za msingi za jiji letu,” amesema Chamba.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu Shule za Msingi wa Jiji la Tanga, Rose Ngowi, alikiri kuwepo kwa wanafunzi wanaosoma sakafuni katika baadhi ya shule na kueleza kuwa madawati yanayoagizwa husambazwa kulingana na uhitaji.
“Madawati yanaagizwa kwa wingi lakini bado hayatoshi kwa sababu mahitaji ni makubwa katika shule nyingi,” amesema Ngowi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Sebastian Danda alisema halmashauri imeagiza madawati ya plastiki kutoka kampuni ya Cello na kwamba Shule ya Msingi Ziwani itanufaika mara yatakapowasili.
“Tunataka shule zetu zisiwe na uhaba wa madawati na wanafunzi wasome kwa furaha katika mazingira bora,” amesema Danda.
Kupatikana kwa madawati 1,864 kunatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya uhaba wa madawati katika shule za msingi jijini Tanga, huku wanafunzi wa darasa la tano na sita katika Shule ya Msingi Ziwani wakiendelea kusubiri suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *