Dar es Salaam. Huenda Kardinali Polycarp Pengo (82), akazikwa Pugu, jijini Dar es Salaam, eneo alilowahi kujichimbia kaburi enzi za uhai wake, akiomba atakapofariki dunia azikwe hapo badala ya Sumbawanga mkoani Rukwa alikozaliwa.

Hata hivyo, taarifa rasmi ya eneo atakalozikwa kiongozi huyo wa kiroho, itatolewa na uongozi wa Kanisa Katoliki, ambao hadi sasa haujaweka wazi, ingawa mwenyewe aliwahi kunukuliwa akieleza nia ya kuzikwa Pugu, enzi za uhai wake.

Kadinali Pengo amefariki dunia saa 4:00 usiku wa Februari 19, 2026 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kabla ya taarifa ya kifo chake, iliyotolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Thaddeus Ruwa’ichi, iliwahi kuelezwa kuwaKardinali Pengo anatarajiwa kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu.

Katika taarifa ya kifo cha Kardinali Pengo ya jana Februari 19, 2026, iliyotiwa saini na Askofu Ruwa’ichi, inaeleza kuwa taarifa za mazishi zitatolewa baada ya mipango kukamilika.

“Taarifa za mazishi zitawajia baada ya mipango kukamilika. Tumwombee apumzike kwa amani,” imeeleza taarifa hiyo.

Mwenyewe alijitabiria kuzikwa Pugu

Hata hivyo, katika moja ya mahojiano na chombo cha habari cha mtandaoni kuhusu uamuzi wake wa kujichimbia kaburi Pugu jijini Dar es Salaam, enzi za uhai wake, Kardinali Pengo alisema, “lilikuwa wazo la kusema natamani kufia hapa kwa hiyo nitazikwa hapa pamoja na wamisionari wa kwanza waliokuja kutoa injili hapa kwetu.

“Wazo la kwamba ningeweza nikafa watu wakasema sijui aende kuzikwa labda Tunduru, Masasi au aende kuzikwa Sumbawanga alikozaliwa, hilo ndilo nilitaka kulifuta kabisa. Nimekuja Dar es Salaam, mimi ni wa Dar es Salaam, nitabaki hapa,” alisema.

Rais Samia, CCM wamlilia

Kutokana na kifo cha kiongozi huyo, Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi, akisema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho.
Amemtaja Kardinali Pengo kuwa kiongozi wa kiroho na mzalendo aliyetoa mchango katika kuimarisha imani, maadili, umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia uongozi wake wa muda mrefu ndani ya Kanisa Katoliki.

“Taifa limepoteza kiongozi aliyelitumikia kwa uadilifu na kujitolea. Mchango wake katika malezi ya kiroho na maadili utaendelea kukumbukwa, kuthaminiwa na kuenziwa,” amesema.

Rais pia ametuma salamu za pole kwa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), viongozi wa dini na waumini wote walioguswa na msiba huo.

Aidha, Rais Samia ameungana na Kanisa Katoliki na Watanzania kwa ujumla katika kipindi hiki cha majonzi, akimuomba Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi. “Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana lihimidiwe,” amesema.

CCM watoa salamu za pole

Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, chama hicho kimeungana na Wakatoliki kuomboleza msiba huo.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa Kardinali Pengo amekuwa na mchango katika kulihudumia kanisa na Taifa kupitia uongozi wake wa kiroho, maadili na huduma za jamii.

“Katika miaka yake 55 ya upadri, miaka 43 ya uaskofu na miaka 28 kama kadinali, aliweka alama ya uongozi wa unyenyekevu, mshikamano wa kijamii na kujitolea kwa ustawi wa watu,” imeeleza taarifa hiyo ya CCM.

Maisha ya Pengo

Katika historia ya uongozi wake, Kardinali Pengo alijijengea taswira ya kiongozi asiyeogopa kusema ukweli hata pale ambapo ukweli huo haukuwa wa kupendeza kwa watawala.

Katika miaka ya 2000, wakati kashfa za kifisadi zilipoibuka na kuitikisa nchi, alitumia mimbari kuonya kwamba ufisadi ni “dhambi inayomlilia Mungu.” Kwa mtazamo wake, wizi wa mali ya umma haukuwa tu kosa la kisheria bali pia la kimaadili, kwa kuwa uliwanyima maskini haki ya huduma za msingi kama afya na elimu.

Kauli zake zilitoa ujasiri kwa waumini na asasi za kiraia kuhoji uwajibikaji wa viongozi, na kuifanya sauti ya Kanisa kusikika si tu madhabahuni bali pia katika mijadala ya kitaifa.

Katika vipindi vya uchaguzi mkuu, alipaza sauti ya tahadhari na busara. Alisisitiza kuwa jukumu la Kanisa si kuchagulia waumini chama, bali kutoa mwongozo wa kimaadili na kuhimiza haki, amani na kuheshimu dhamiri ya mtu binafsi.

Msimamo huo ulionekana wazi wakati wa mjadala wa Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ambapo alihimiza utulivu huku akisisitiza umuhimu wa mchakato wa haki na huru. Kwa kufanya hivyo, alisaidia kupunguza jazba za kisiasa na kuzuia mgawanyiko wa kidini.

Mtetezi wa familia, maadili

Kadinali Pengo alijulikana pia kwa msimamo wake mkali katika kulinda taasisi ya familia kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki. Alipinga kwa uwazi misukumo ya kimataifa aliyodai ingeweza kuyumbisha misingi ya maadili ya Kiafrika na Kikristo.
Aliwahi kusisitiza kuwa taifa linaweza kuvumilia changamoto za kiuchumi, lakini lisipoteze utu na misingi yake ya maadili. Kauli hiyo ilimjengea heshima miongoni mwa wanaomuona kama nguzo ya uzalendo wa kimaadili.

Safari kutoka kijijini hadi Vatican

Alizaliwa Agosti 5, 1944, katika Kijiji cha Mwazye, mkoani Rukwa. Alipewa daraja la Upadri Juni 20, 1971, kabla ya kuendelea na masomo ya Teolojia ya Maadili katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, Roma, alikopata Shahada ya Uzamivu mwaka 1976.

Mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Askofu wa Nachingwea, kisha Tunduru-Masasi mwaka 1986. Mwaka 1990 akateuliwa kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Dar es Salaam na mwaka 1992 akawa Askofu Mkuu kamili.

Mwaka 1998, aliteuliwa kuwaKardinalina Papa Yohane Paulo II, hatua iliyomuingiza katika Baraza la Makadinali na kumpa nafasi ya kushiriki katika mikutano ya kumchagua Papa mwaka 2005 na 2013.

Alistaafu rasmi mwaka 2019 na nafasi yake kuchukuliwa na Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi.

Urithi wake

Kaulimbiu yake, “In Caritate et Veritate” (Katika Upendo na Ukweli), ilidhihirisha dira ya maisha yake ya utumishi. Alikuwa kiongozi mwenye sauti tulivu lakini maneno yenye uzito, akiamini kuwa upendo usiotenganishwa na ukweli ndiyo msingi wa haki ya kweli.

Kwa wengi, atakumbukwa kama mchungaji aliyeamini kuwa Kanisa haliwezi kukaa kimya wakati jamii inakabiliwa na dhuluma. Kwa wengine, alikuwa nguzo ya msimamo wa jadi katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi.

Katika ukurasa wa historia ya Tanzania, jina la Kardinali Polycarp Pengo litaendelea kusomwa kama alama ya uongozi wa kiroho uliogusa siasa, jamii na dhamiri ya taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *