
Klabu ya Wafungwa wa Palestina imetangaza kuwa, zaidi ya mateka na wafungwa 9,300 wa Palestina na Kiarabu wanashikiliwa katika magereza ya utawala ghasibu wa Israel na wamekuwa wakikabiliwa na sera za mateso, njaa, na mauaji ya taratibu tangu kuanza “mauaji ya kimbari ya Israel” mnamo Oktoba 7, 2023.
Klabu ya Wafungwa wa Palestina imesisitiza kwamba, kwa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani, maelfu ya wafungwa wamekabiliwa na sera ya njaa inayoendelea iliyowekwa na utawala vamizi ambayo imedumu kwa karibu miaka miwili na nusu, na wamelazimishwa kufunga siku nyingi.
Shirika hili linalotetea haki za wafungwa wa Palestina liliongeza: “Idara ya Magereza ya utawala wa Kizayuni huwapa wafungwa kiasi kidogo cha chakula, jambo ambalo huwazuia tu kufa kwa njaa.”
Taarifa ya Klabu ya Wafungwa wa Palestina imesema: Miongoni mwa wafungwa, takriban mateka 70 wa kike wanashikiliwa katika gereza la Al-Damon na vituo vya usaili, na takriban watoto 350 wanashikiliwa katika magereza ya Megiddo na Ofer, ambao pia wanakabiliwa na sera hizo hizo, ikiwa ni pamoja na mateso na njaa.
Awali kabla ya hapo, Kamati ya Masuala ya Mateka wa Palestina ilitoa taarifa ikisema kwamba ripoti zilizopokelewa kutoka kwenye gereza la Ofer kuhusiana na mashambulizi ya kikatili yaliyofanywa dhidi ya mateka wa Kipalestina yaliyohusisha kupigwa na kujeruhiwa mateka hao na kufyatuliwa mabomu ya machozi inaakisi sehemu ya mashambulizi ya kikatili ambayo wavamizi hao wanayafanya dhidi ya mateka wa Kipalestina, na ambayo yameshadidi baada ya mafanikio uliyopata Muqawama wa Palestina.