
Dar es Salaam. Siku tatu baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuhitimisha ziara mkoani Tanga na kubaini madudu, akitaka hatua zichukuliwe kwa wahusika, watumishi 14 wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza wamesimamishwa kazi.
Februari 17, 2026, Dk Mwigulu alihitimisha ziara yake mkoani Tanga ambapo alieleza kutoridhishwa na utekelezaji wa miradi katika Halmashauri ya Muheza huku akiagiza hatua za haraka kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Katika kikao hicho cha majumuisho kilichofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Dk Mwigulu alitaja Halmashauri ya Muheza kumuangusha baada ya kubaini vifaa vilivyopaswa kupelekwa eneo la mradi kuchepushwa.
Baadhi ya mambo aliyoyataja ni pamoja na vifaa vya ujenzi vilivyonunuliwa lakini havikufika eneo la mradi, ikiwemo nondo zenye thamani ya Sh9.2 milioni, marine boards 192 zenye thamani ya Sh7.8 milioni.
Pia, alibaini kwamba mifuko ya saruji 300 haikufikishwa eneo la mradi licha ya fedha kulipwa, mshauri elekezi alilipwa Sh11.9 milioni bila mkataba huku Sh343 milioni zikitumika kulipana posho.
Dk Mwigulu alimuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, kusafisha watumishi wote waliohusika na ubadhirifu wa fedha za jengo la ofisi.
Hatua zachukuliwa
Leo, Februari 20, 2026, Waziri wa Tamisemi, Profesa Shemdoe, amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga kuwapumzisha watumishi 14 ili kupisha uchunguzi dhidi yao.
Profesa Shemdoe, kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, amefafanua kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo aliyopewa na Waziri Mkuu, yeye pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete.
Taarifa hiyo inamnukuu Profesa Shemdoe akisema katika kutekeleza agizo la kiongozi huyo, walipeleka wataalamu kutoka pande zote mbili ili kushughulikia suala hili katika hatua za awali.
“Nimemuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa kufuatilia na kumsimamia Mkurugenzi wa Halmashauri kupata timu ya watu waadilifu watakaokuwa kwenye kamati hiyo ili kufanya uchunguzi wa suala hilo,” amesema.
Pia, amemtaka Mkurugenzi huyo kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliotajwa na ambao hawakutajwa endapo watabainika kuhusika katika kusababisha changamoto katika utekelezaji wa mradi huo baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
Aidha, kwa wahusika waliotajwa katika taarifa za awali wasio watumishi wa umma, Profesa Shemdoe amevielekeza vyombo vinavyohusika na uchunguzi, ikiwemo Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuchukua hatua stahiki dhidi yao.
Kwa upande wake, Waziri Ridhiwani amesema majukumu ya ofisi yake pamoja na ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi ni kuratibu masuala ya utumishi wa umma nchini, kwani Ofisi ya Rais, Utumishi ndiyo mwajiri mkuu anayewapangia watumishi vituo vya kazi na vituo hivyo vinasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi.
Ameongeza kuwa linapotokea jambo linalohusu masuala ya kiutumishi, yeye, Waziri wa Utumishi na Waziri wa Tamisemi wanahusika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa umma na ndiyo maana Waziri Mkuu amewaelekeza kushughulikia changamoto hiyo ya utekelezaji wa mradi wa jengo hilo.