Hoja kuu za Volker Türk kuhusu AI

  • Haki za binadamu zinatoa mfumo wa kuendeleza, kubuni na kutumia AI kwa usalama
  • Athari za AI zinahusu nguvu na jinsi inavyotumika
  • Ukosefu wa usawa, upendeleo na ubaguzi ni hatari kubwa kwa haki za binadamu kutokana na kasi ya upanuzi wa AI
  • Tathmini za athari kwa haki za binadamu zinahitajika katika hatua za kubuni, kuendeleza na kusambaza AI
  • Kampuni za teknolojia lazima ziheshimu kanuni za Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na haki za binadamu
  • Bila uelewa wa kina wa misingi ya kijamii na kimaadili, watengenezaji wa AI wanaweza kuunda ‘jitu’ linaloweza kudhuru binadamu na kisha kushindwa kulidhibiti

Türk amesema hayo katika mahojiano maalum na Idhaa ya Umoja wa Mataifa (UN News) kando ya Mkutano wa Athari za AI unaomalizika jijini New Delhi, nchini India Jumamosi Februari 21, akiongeza kuwa teknolojia hiyo inapaswa kuongozwa na mfumo wa haki za binadamu unaohakikisha uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji.

Mahojiano hayo ni kama ifuatavyo:

Volker Türk: Akili mnemba (AI) ni chombo cha kiteknolojia na kinapaswa kuendelezwa kwa kuzingatia tathmini ya hatari. Zana za teknolojia hutumika kutekeleza nguvu — kwa mema lakini pia kwa mabaya — hivyo tunahitaji kuhakikisha kuna mfumo unaoongoza namna zinavyobuniwa, kuendelezwa na kutumika, na hapo ndipo haki za binadamu zinapokuwa muhimu.

UN News: Ni hatari zipi kubwa zaidi kwa haki za binadamu unazoziona kutokana na kasi ya upanuzi wa AI zama za sasa?

Volker Türk: Kuna tatizo kubwa la ukosefu wa usawa, ndiyo maana ninafurahi mkutano huu wa AI unafanyika India. Ni muhimu sana zana hizi zitumike kila mahali na ziendelezwe kila mahali.

Kuna pia suala la upendeleo na ubaguzi. Ikiwa data zitakusanywa kutoka sehemu moja tu ya dunia, au kama ni wanaume pekee wanaoendeleza AI, basi upendeleo wa ndani kwa ndani utaingizwa katika mifumo hiyo. Tunaamini ni muhimu kuzingatia makundi yaliyo hatarini na wachache, kwa sababu mara nyingi huachwa nje katika maendeleo ya AI. Hii ni kuhusu ushiriki wa maana na kutoa dira ya dunia bora. Haki za binadamu zinatoa dira hiyo.

UN News: AI zalishi au (GenAi) inakua kwa kasi kuliko kanuni za udhibiti. Serikali na kampuni zinapaswa kuweka hatua gani za haraka za ulinzi?

Volker Türk: Chukua mfano wa sekta ya dawa: majaribio yanaweza kuchukua muda mrefu kwa sababu ni lazima uhakikishe hatari zote zinazoweza kuhusishwa na bidhaa mpya zinatambuliwa kabla ya kuingia sokoni.

Wanaume wawili waliovaa suti wamesimama mbele ya nembo ya Umoja wa Mataifa. Mmoja ni mvivu na miwani na tai nyekundu, mwingine ana ndevu kijivu na tai ya bluu.

© UN India/Blassy Boben

Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Turk akiwa na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini India, Stephan Priesner.

Kwa zana za AI, tunapaswa kudai kampuni zifanye tathmini ya athari kwa haki za binadamu wanapozibuni, kuzisambaza na kuziuza.

Kwa muda sasa tumeshuhudia baadhi ya kampuni zikiwa na bajeti kubwa kuliko hata nchi ndogo. Ukiweza kudhibiti teknolojia si tu katika nchi yako bali duniani kote, unakuwa na nguvu kubwa. Unaweza kuitumia kwa mema — kama kusaidia sekta ya afya, elimu na maendeleo endelevu — lakini pia kwa mabaya, kama silaha zinazojiendesha zenyewe, kusambaza taarifa potofu, chuki na dhuluma dhidi ya wanawake.

UN News: Ni aina gani ya uongozi au kanuni za AI zinahitajika kuzuia mifumo hiyo kuimarisha upendeleo na ukosefu wa usawa?

Volker Türk: Nimepata fursa ya kuzungumza na watu wanaozalisha na kubuni teknolojia hizi. Kinachonishangaza ni kwamba mara nyingi wana uelewa wa juu juu kuhusu misingi ya kimaadili na kijamii wanapoanza hatua ya maendeleo.

Hii inanifanya nikumbuke hadithi ya jitu la Frankenstein, — unatengeneza kitu ambacho baadaye hukidhibiti tena, kama vile kumwachia jini kutoka kwenye chupa.

Usipokuwa makini na hatari zake, unaweza kusababisha madhara makubwa. Tumeona hilo Myanmar, ambako hotuba za chuki dhidi ya Rohingya zilienezwa sana kupitia mitandao ya kijamii.

Ni muhimu sana kuleta mitazamo ya kila kundi la jamii, hasa wanawake na vijana, na kutambua kuwa akili zetu hukua kwa njia tofauti.

Hatupaswi kuunda mifumo inayozalisha uraibu unaoharibu akili na roho zetu. Tunapaswa pia kutambua jinsi taarifa potofu zinavyoweza kuharibu mshikamano wa kijamii na kuunda jamii zilizogawanyika ambako kila mtu anaishi katika “bubujiko” lake.

Pia tunaona ongezeko la chuki dhidi ya wanawake. Wanasiasa wengi wa kike wamenieleza wanafikiria kuacha siasa kutokana na wanayokumbana nayo mitandaoni.

UN News: Miaka mitano ijayo, unafikiri AI yenye uwajibikaji itakuwa vipi?

Volker Türk: Natumaini tutakuwa na maendeleo jumuishi ya akili mnemba, ambapo nguvu haitakuwa mikononi mwa kampuni chache tu Amerika Kaskazini, na ambapo maendeleo ya AI yataakisi utajiri na utofauti wa kila jamii.

Ninatamani kuona maendeleo ya ushirikishwaji wa maana, yatakayosaidia kutatua changamoto nyingi za dunia ya leo — kama janga la tabianchi, upatikanaji wa huduma za afya na elimu kwa wote. AI inaweza kuwa chombo bora sana kufikia malengo hayo.

Lakini tusipokuwa na maono ya dunia bora, tunaweza kuishia na jamii zilizogawanyika zaidi, na hata vita visivyodhibitiwa na binadamu — jambo ambalo ni hatari sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *