Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, amesema hakutakuwa na usitishaji mapigano mpaka pale Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) vitakapojiondoa kwenye kile alichokieleza kuwa ni maeneo vinayoyakalia na kujikusanya upya katika maeneo yaliyotengwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Sudan (SUNA), Al-Burhan ametoa matamshi hayo katika hafla ya hadhara iliyofanyika mjini Omdurman, magharibi mwa mji mkuu, Khartoum.

Mapigano kati ya Jeshi la Sudan SAF na RSF yamekuwa yakiendelea tangu Aprili 2023, chanzo kikiwa ni mzozo kuhusu kuunganishwa wanamgambo wa RSF katika vikosi vya kawaida vya jeshi. Mgogoro huo umesababisha baa la njaa katika sehemu kadhaa za Sudan, kuzusha moja ya hali mbaya zaidi ya kibinadamu duniani, kupelekea kuuawa makumi ya maelfu ya watu na kuwalazimisha kuyahama makazi yao karibu watu milioni 13.

Katika hotuba yake hiyo, Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan amesema, vijana walioongoza vuguvugu la Desemba 2019 lililomng’oa madarakani rais wa zamani Omar al-Bashir wana “uwezo wa kuwang’oa wanamgambo”, akimaanisha RSF, ili kurejesha usalama na utulivu nchini.

Ameongezea kwa kusema: “hakutakuwa na suluhu itakayofikiwa na wanamgambo waasi, wakati wao wanaikalia miji na maeneo na kufanya vitendo vya ukiukaji dhidi ya raia.”

Halikadhalika, Al-Burhan amesisitiza kwamba, Sudan haitakubali nafasi yoyote ya upatanishi ya Muungano wa Falme za Kiarabu, akiishutumu nchi hiyo kwa kuunga mkono uasi.

Hii ni katika hali ambayo, Imarati imekuwa ikikanusha mara kwa mara shutuma za kutoa msaada kwa RSF na kusisitiza kwamba haiingilii masuala ya ndani ya Sudan…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *