
Kanisa Katoliki limempoteza mmoja wa viongozi wake. Ni Muadhama Polycap Kardinali Pengo. Baraza la Maaskofu (TEC) limempoteza jabali wa Maadili ya Kanisa. Taifa limempoteza kiongozi wa kijamii aliyekuwa tayari wakati wote kutoa mawazo yake kwa ajili ya ustawi wa jamii nzima.
Msiba huu umetukuta katikati ya msiba mwingine. Viongozi wetu wametawanyika huko huko kuzima mioto mbalimbali. Kwa hiyo, tunapoomboleza msiba wa Muadhama Pengo, ni muhimu “kuomboleza vizuri”. Nashauri;
1. Muadhama Pengo na TEC havitenganishwi. Huwezi kumpenda Pengo ukaichukia TEC au kinyume chake. Tumia hekima kama huna akili ya kutumia.
2. Kanisa Katoliki limeumizwa na wasioujua muundo wake. Kwenye msiba huu “Vijora viwe likizo”. Asiyependa kuomboleza, awape nafasi wanaoomboleza.
3. Muadhama Pengo ni bingwa wa Maadili ya Kiroho. Kama hukuwa naye siku za mwisho, usikimbilie kubuni alikuwa anawaza nini. Hali yake na msimamo wake wa mwisho anaujua yeye na Muumba wake. Letu ni kumuombea, si kummiliki.
4. Muadhama amefanya kazi na marais wote 6. Anawajua wote. Wanamjua kwa sehemu tu. Hilo ndilo kanisa. Marais wema na wabaya huja na kupita. Kanisa hubaki. Tusilibeze kanisa linalobaki wakati sisi tunapita. Machawa nimewawashia taa msije sema sikuwaambia.
5. Muadhama Pengo alikuwa Mkristo, Mkatoliki. Hakuna ukatoliki usio ukristo hata kama kuna ukristo usio ukatoliki. Kiunganishi ni msalaba. Jitihada za kuliunganisha Taifa, ZISIJARIBU kuwagawa wakristo kati ya TEC, CCT, PCT, SDA nk. Wote ni Wakristo hata kama kuna wanaoweza kuwepo wanaojiona bora kuliko wengine. Kanisani hakuna cha “Kanisa lina wenyewe”.
6. Muadhama Pengo alikataa katakata dhana ya dini ya Taifa. Haikufaa na haitafaa. Wakristo wanaojifanya ni wakristo kuliko Bwana Yesu, Paeni mbinguni mkaishi huko. Wale ndugu zangu wanaojifanya wana dini kuliko Mtume, nendeni muishi huko alikozaliwa. Tanzania yetu sote, wanaovaa vimini na baibui. Muadhama alipenda ukweli kama unavyosimamiwa na TEC. Tushawishiane, tusiburuzane.
Pumzika Mzee wetu. Hata Wajaluo wanakulilia.
Kwaresima Njema.
Ramadhani Kareem.