Dar es Salaam. Wiki hii imekuwa ya majonzi kwa wapenzi wa muziki wa zamani, kutokana na kuondokewa na wanamuziki wakongwe wawili. Francis James Bundala na Stephen Hiza.
Moja ya maajabu ni kuwa Steven Hiza alizaliwa 1 Julai 1945, wakati Francis Bundala alizaliwa 1 Julai 1946.
Francis James Bundala, aliyekuwa maarufu kwa jina la Dj Sweet Francis, alikuwa ni kati ya madj wakongwe hapa nchini.
Sweet Francis aliingia katika tasnia ya muziki akiwa ni muimbaji. Bendi yake ya kwanza ilikuwa ni kundi lililojiita The Screamers, kundi lililoanzishwa Magomeni mwaka 1964, ni katika kundi hili ndipo alipoanza kuitwa Sweet Francis likiwa ni jina la kusifia sauti yake tamu.
Mwaka 1965 kundi la Screamers likavunjika na likaundwa kundi lililoitwa The Hot Fives, nalo lilikuwa kundi la hapohapo Magomeni. Kundi hili kila mwisho wa wiki likawa likipiga muziki wa mchana ulioitwa Buggy katika ukumbi wa Arnatougro.
Kundi la The Hot Fives likavunjika na Sweet Francis na wenzie, akina Michael Jackson Simtowe kwenye gitaa la solo, Green Jackson Simtowe akiwa katika gitaa la rythm.
John Sabatele alikuwa ndie mpiga gitaa la bezi, Alwatha Charles alikuwa ndie mpiga drums, wakaanzisha kundi lililoitwa The Tonics. Ni katika kundi la Tonics ambapo Adam Salehe Mwambile, aliyekuja kuwa maarufu kwa jina Dj Addy Sally, alipoingilia tasnia ya muziki.
Picha ya marehemu Stiven Hiza
Alianza kama mpiga conga, baadaye akawa ndie mpiga drums wa Tonics na hatimaye akawa DJ. Green Jackson Simtowe alikuja kujiunga na kundi la Maquis Du Zaire kama muimbaji wa nyimbo za kizungu. Hawa akina Simtowe asili yao ilikuwa Zambia na Michael Jackson hatimaye alirudi kwao.
Mwezi Novemba 1967, The Tonics wakapata mkataba wa kupiga muziki kila siku hapo katika ukumbi wa Splendid Hotel. Mkataba huo uliisha mwezi Mei 1968, na the Tonics wakahamia Arusha wakawa wanapiga muziki wao katika ukumbi wa Cameo Bar.
Francis aliiacha The Tonics mwaka 1970 na kuhamia Mombasa ambako aliendelea na fani yake ya uimbaji. Alipokuwa Mombasa akaongeza ujuzi na kuwa mwanamuziki wa Cabaret.
Hii ni aina ya muziki ambayo muimbaji huimba huku akizunguka kwa wateja, akiongea nao na kupiga hadithi mbalimbali. Sweet Francis alirudi Dar es Salaam na kuendelea na cabaret katika kumbi za Kilimanjaro Hotel.
Mwezi Agosti mwaka 1972, Sweet Francis aliajiriwa Hotel Africana kama DJ wa disco maarufu lililoitwa Gogo Disco. Hili lilikuwa Disco lililokuwa ‘chati’ ya juu sana wakati huo, Madj wake kabla ya Francis walikuwa Madj kutoka nchi za nje.
Sweet Francis pia alifanya kazi za Udj na cabaret Zambia, Afrika ya Kusini na hata Brazil. Sweet Francis ndie alikuwa DJ wa kwanza wa Cave Disco pale Safari Hotel, Arusha. Nafasi yake ikaja kuchukuliwa na marehemu Dj Choggy Sly. Sweet Francis ndie alikuwa DJ wa kwanza wa Keys Disco katika hoteli ya Keys pale Mnazi Mmoja.
Picha ya msanii Dj Sweet Francis
Dj Sweet Francis, alizaliwa katika Kijiji cha Kinaga wilaya ya Kahama, mkoa wa Shinyanga tarehe 1 Julai mwaka 1949. Amefariki Jumamosi tarehe 14 Februari 2026 katika hospitali ya Mwananyamala na kuzikwa Jumatatu tarehe 16 katika makaburi ya Kinondoni.
Mmoja ya wimbo maarufu Tanzania ni huu wenye maneno haya ;
Tanzania yetu ndio nchi ya kusifiwa,
Kote ulimwenguni watu wote watambua,
Tanzania yetu ndio nchi ya furaha
Umaarufu wa wimbo huu umeuwezesha kurekodiwa na wanamuziki vijana wengi na wengine hata kuingia matatani kutokana na kuurekodi bila kupata kibali toka kwa mtunzi. Kwa mapenzi yake Mungu mtunzi wa wimbo huu Stephen Hiza amefariki siku ya Jumatatu 16 Februari 2026 nyumbani kwake jijini Tanga.
Steven alijiunga na Atomic Jazz Band ya Tanga mwaka 1965 baada ya kuondoka toka bendi hiyo muimbaji alieitwa Kamaru. Kamaru alipoacha bendi ghafla mwaka 1965, ndipo walipojiunga vijana wawili waimbaji, Stephen Hizza na Ziggi Said, ambao walitokea kwenye vibendi vidogo vilivyokuwepo Tanga. Wote wawili kwa sasa ni marehemu.
Mwaka 1967 Atomic Jazz band iliingia studio na kurekodi wimbo maarufu Tanzania Yetu nchi ya Furaha, na nyimbo nyingine kadhaa zikiwemo Leo Nakupasulia, Ewe Hafidha wangu ( wimbo ambao kipande chake cha solo la utangulizi kilichukuliwa na kampuni moja ya sinema ya Norway na kuwa sehemu ya ‘sound track ya filamu yao).
Wakati huo wanamuziki waliokuwa katika bendi walikuwa ni John Mbula-Saxophone, John Kilua- Conga, Gislan Dejean (Mkongo) kwenye gitaa la bezi, Harrison Siwale kwenye gitaa la ridhim, Hassan Ngoma kwenye gitaa la solo.
Mzee Hiza amekuwa jukwaani mpaka siku yake ya mwisho kwani siku moja kabla ya kifo chake, Mzee Hiza alikuwa jukwaani kama kawaida yake.
Tunawaombea Mungu awalaze pema Francis James Bundala na Steven Hiza.