Mjumbe mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Yemen ya Ansarullah ametoa taarifa akieleza kwamba kuzungumziwa duru mpya ya vita vinavyotaka kuanzishwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Muqawama ni sawa na adui kukiri kwamba alishindwa katika vita vilivyopita.

Nasruddin Amer ameandika kwenye ukurasa wake binafsi kwenye Telegram: “Kuzungumzia vita vipya ni ishara kwamba Uzayuni wa kimataifa, pamoja na suhula zake zote ulizonazo ambazo hazijawahi kushuhudiwa, haujaweza kuushinda Mhimili wa Muqawama, ambao unajumuisha wale wote wanaonyongeshwa na waliokomboka kimawazo, wenye mwamko na walio makini katika Umma wa Kiislamu”.

Amer ameongezea kwa kusema: “kama ni kweli Mhimili wa Muqawama na Jihadi umeshindwa na kuangamizwa kama maadui walivyoeneza kipropganda katika miezi iliyopita, nini basi lengo la harakati hii ya kujizatiti kijeshi na kutuma manowari za kivita? Kuzungumzia vita vipya ni kuungama adui kwamba alishindwa katika vita vilivyopita”.

Mjumbe huyo wa Ansarullah amebainisha kuwa, suhula za kimaada za wanaonyongeshwa na waliokomboka kifikra haziwezi kulinganishwa na suhula za madola ya kitaghuti na ya kibeberu, lakini wao wanaonyongeshwa wanamtegemea Mwenyezi Mungu, na hiyo ndiyo siri ya uthabiti na ushindi wao katika vita vyovyote vijavyo.

Awali kabla ya hapo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen alituma salamu rasmi kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, akimpongeza kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitizia mshikamano kamili wa Sana’a na Tehran dhidi ya vitisho.

Katika ujumbe huo kwa Sayyid Abbas Araghchi, Abdul Wahab Abu Rass ameashiria mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na akataja kukomeshwa utegemezi kwa madola ya kigeni kuwa ni moja ya mafanikio hayo muhimu zaidi ya mageuzi hayo ya kihistoria.

Aidha, ameusifu uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa masuala ya haki ya Ulimwengu wa Kiislamu, hususan suala la Palestina…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *