
Arusha. Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC) imepitisha mapendekezo ya bajeti ya Sh75.4 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni ongezeko la Sh7.4 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/2026 ya Sh68 bilioni.
Akizungumza katika baraza maalumu la madiwani lililofanyika Februari 20, 2026, mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye pia ni diwani wa Kata ya Olturoto, Baraka Ole Simioni, amesema bajeti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia ongezeko la mahitaji ya miradi ya maendeleo, pia, mwongozo wa mpango wa bajeti ya Serikali na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Amesema bajeti hiyo imelenga kuimarisha sekta za afya, maji, elimu, barabara na umeme hadi ngazi ya kaya, kwa lengo la kuboresha ustawi wa wananchi na kuleta maendeleo endelevu.
“Katika bajeti hii, mapato ya ndani yanatarajiwa kufikia Sh9.2 bilioni, yakipanda kutoka Sh7 bilioni za mwaka uliopita na miradi ya maendeleo imetengewa Sh11 bilioni,” amesema Ole Simioni.
Ameeleza kipaumbele kikubwa kimewekwa katika maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2027, kufuatia wimbi kubwa la wanafunzi wa darasa la sita na la saba kumaliza kwa pamoja kutokana na mabadiliko ya mtaala.
“Zaidi ya wanafunzi 20,000 wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza, Hivyo, tunakabiliwa na mahitaji ya zaidi ya vyumba 200 vya madarasa na kwa awamu hii, tumepanga kujenga madarasa 25 pamoja na madawati yake,” amesema.
Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuwaunga mkono kukamilisha mahitaji ya madarasa na madawati yaliyobaki.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kimnyak na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Eliakimu Marvey amesema halmashauri imejipanga kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kufungua vituo vipya vya ukusanyaji katika maeneo ya Ngaramtoni, Kiserian na Kisongo.
“Lengo letu ni kuvuka Sh10 bilioni za mapato ya ndani katika miaka ijayo ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi,” amesema Marvey.
Ameongeza kuwa bajeti hiyo, pia, itagusa uboreshaji wa miundombinu ya barabara ambapo kila kata itanufaika na angalau kilomita moja ya kiwango cha changarawe, ujenzi wa vivuko, ukarabati wa shule kongwe, ujenzi wa matundu ya vyoo, pamoja na kuboresha sekta ya afya na upatikanaji wa maji katika kata zote 27 kwa kushirikiana na Ruwasa na Rea.
Naye diwani wa viti maalumu, Nina Masanja wa Kata ya Kiutu amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni uboreshaji wa barabara ambazo zimekuwa zikiharibiwa na maji ya mvua kila mwaka.
“Kila mwaka barabara hizi zinahitaji bajeti mpya ya ukarabati, ingekuwa si hivyo, fedha nyingi zingekuwa zinaenda kwenye miradi mingine, hivyo niombe wananchi wawe watunzaji wa miundombinu hii, kila inapokarabatiwa hasa katika usafirishaji vitu vizito katika barabara zenye kikomo ya uzito,” amesema.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dk Johannes Lukumay ametumia fursa hiyo kuwataka madiwani kuendelea kutoa elimu ya bima ya afya kwa wote ili wananchi wengi zaidi wajitokeze kujiandikisha na kunufaika na huduma bora za afya.