
KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker amesema licha ya kuridhika na ubora unaoonyeshwa na wachezaji wa kikosi hicho, amekiri kuwa na ratiba ngumu ambayo inawapa wakati mgumu kutoboa huku akipanga silaha zake vizuri kuhakikisha anakusanya pointi zote tisa.
Ndani ya wiki moja, Simba inakabiliwa na mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara itakazocheza ugenini dhidi ya Tanzania Prisons (leo Jumapili), Dodoma Jiji (Jumatano Februari 25) na Yanga (Jumapili Machi 1).
“Nafurahishwa na maendeleo ya wachezaji wangu wameanza kuingia kwenye mfumo na wana hali nzuri ya ushindani, hili ni moja na ni faida kwetu, lakini kiukweli tuna ratiba ngumu kidogo, licha ya yote mpango ni kuhakikisha tunakuwa bora kwenye kila mechi ili kufikia malengo ya kukusanya pointi zote tisa.
“Hatupaswi kulalamika isipokuwa kupambana na hali halisi, ingawa ukweli ni kwamba tuna wakati mgumu wa kuhakikisha tunakuwa imara, nina imani kwamba wachezaji wangu watafuata maelekezo kwa kuhakikisha tunapata matokeo mazuri na wanakuwa bora kwenye kila mechi,” alisema Barker.
Alisema faida waliyonayo kuelekea mechi mbili dhidi ya Prisons na Dodoma Jiji licha ya kuwa ugenini ni kucheza kwenye uwanja mmoja, hivyo watakuwa na nafasi ya muda wa kufanya maandalizi mazuri mechi baada ya mechi, kisha watakuwa na safari ya kuifuata Yanga.
“Dodoma tuna faida, tunacheza mechi mbili ugenini lakini kwenye uwanja mmoja, hili linarahisisha safari moja hadi nyingine, tunatakiwa kutumia faida hii kuhakikisha tunapata pointi zote sita japo haitakuwa rahisi kwani tunacheza na timu ambazo pia zinataka matokeo, lakini mbinu sahihi ndio zitaamua ubora.
“Ligi ni ngumu na ushindani ni mkubwa, ili kuwa bora unahitaji kuwa mshindani na kuandaa timu katika hali nzuri ili iweze kupambania nembo ya timu tuweze kufikia malengo japo sio rahisi, lakini kila kitu kinawezekana,” alibainisha.
Barker amesifu upana wa kikosi chake kuwa unampa nafasi kubwa kutumia mfumo wowote bila kuathiri ufanisi wa timu na anaamini wachezaji hao ndio watakaoamua matokeo mazuri.
“Simba tuna utajiri mkubwa wa vipaji ambao unanipa wasaa wa kutumia mfumo wowote bila kuathiri ufanisi wa mchezaji mmoja mmoja. Ingawa mimi siamini sana kwenye mfumo bali namna gani sahihi ya kutengeneza nafasi na kuzitumia. Nina mawasiliano mazuri sana na wachezaji wangu wote licha ya kwamba sio wote wanapata nafasi,” alisema Barker na kuongeza;
“Kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi, hilo limeanza kwenye mchezo wa Kombe la CRDB, tunatarajia kuwa na mwendelezo kwenye mechi zijazo lengo ni kuona tunatengeneza mzani mzuri wa ubora wa wachezaji ambao wanatumika na wasiotumika hasa kipindi hiki cha ratiba ngumu.”
AIPOTEZEA DABI
Ukiwauliza mashabiki ni mechi gani ambayo wanaisubiri kwa shauku kubwa, watakwambia ni Kariakoo Dabi inayozikutanisha Yanga na Simba, lakini cha kushangaza, Barker ni kama anaficha anachokijua kuhusu mabingwa watetezi hao, huku akisema kwa sasa haiwazi kabisa mechi hiyo kwani ana wapinzani wawili wanaompasua kichwa.
Machi Mosi mwaka huu, Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba katika mechi yao ya kwanza kuwakutanisha katika Ligi Kuu Bara msimu huu itakayochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Kabla ya mechi hiyo, watani hao wa jadi kila mmoja ana mechi mbili za ligi.
Barker alisema Yanga anaijua na ameiona ikicheza, lakini kwa sasa akili yake haipo kwenye mechi hiyo ya Dabi huku akisisitiza kwamba anataka kuhakikisha kwanza wanashinda mechi mbili zijazo ambazo zote Simba itakuwa ugenini, baada ya hapo ndipo watakapokuwa na muda wa kuzungumza kuhusu Kariakoo Dabi.
“Tunaenda Dodoma kukutana na Tanzania Prisons, wasiwasi wangu ni ubora wa uwanja wa huko, lakini kwa vyovyote tutahakikisha tunarudi na pointi zote sita kwani tumejiandaa na ugumu kwa kuwa Prisons siyo timu rahisi, ina wachezaji wanaotumia nguvu zaidi.
“Kuwaza dabi kwa sasa ni mapema kwa sababu tayari tuna kazi ngumu mbele yetu. Yanga ni timu ambayo tutakutana nayo baada ya kumalizana na hizi mechi mbili, hivyo bado hatujajipanga kukabiliana nayo.
“Ukiniuliza kitu gani kinanipasua kichwa kwa sasa ni ubora wa viwanja. Kwa sasa sitamani mchezaji wangu yeyote apate majeraha. Unajua nini? Kama kiwanja kikiwa na mashimo au nyasi ambazo si nzuri, ni rahisi kwa mchezaji kuumia.
“Lakini naamini kabisa kwamba tutamaliza salama na kubeba alama tatu katika kila mechi, ingawa tunakwenda kukutana na wapinzani ambao wanacheza soka la nguvu, hivyo lazima wachezaji watakaopangwa wanatakiwa wawe fiti sana,” alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.
Leo Jumapili, Simba itakuwa mgeni wa Tanzania Prisons, kisha Februari 25 mwaka huu ni dhidi ya Dodoma Jiji, mechi ambazo zote zimepangwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. Baada ya hapo, ndipo itaelekea Zanzibar kuikabili Yanga.
Ikumbukwe kuwa, Simba inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa imecheza mechi nane na kushinda sita, ikipoteza moja na kutoka sare moja, ikifikisha jumla ya pointi 19.
Rekodi zinaonyesha Simba haijapata ushindi wowote mbele ya Yanga katika mechi sita mfululizo zilizopita za Dabi ya Kariakoo kwa mashindano yote na mara ya mwisho katika Ligi Juni 25, mwaka jana ilipasuka mabao 2-0 na kuwapa watani wao ubingwa wa msimu wa nne mfululizo.
Hii itakuwa Kariakoo Dabi ya kwanza kwa Steve Barker sambamba na Pedro Goncalves wa Yanga ambao wote wametua msimu huu. Alianza Pedro kutambulishwa Yanga Oktoba 25, 2025 akichukua nafasi ya Romain Folz aliyeshinda Dabi ya Septemba 16, 2025 katika Ngao ya Jamii dhidi ya wekundu hao, kisha Simba ikamtambulisha Barker Desemba 19, 2025 kurithi mikoba ya Dimitar Pantev.