
Unguja. Hatimaye Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoka hadharani na kuweka wazi mpango wa mazungumzo yanayoendelea na Chama cha ACT Wazalendo kupata suluhu ya mkwamo wa kisiasa, baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kwa nyakati tofauti akiwa Unguja na Pemba, Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman ameeleza namna ambavyo wameingia kwenye mazungumzo ya kupata muafaka wa siasa Zanzibar, lakini upande wa CCM haukuwa tayari kutoa kauli yoyote kuhusu mazungumzo hayo.
Kwa mujibu wa CCM, taarifa ya kuingia kwenye mazungumzo ilipokewa wakati wa kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu Taifa kilichofanyika Februari 19, 2026 kwenye Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar chini ya Makamu Mwenyekiti, Dk Hussein Mwinyi.
Katika taarifa yake leo Februari 21, 2026, Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, amesema CCM imepokea taarifa ya maendeleo ya mazungumzo yanayotafuta mwafaka wa utatuzi wa kisiasa, yenye lengo la kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Hata hivyo, amesema mazungumzo hayo yanayosimamiwa na marais wastaafu wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein, bado ni siri.
Mbali na viongozi hao wawili pande zote mbili hazijataja wajumbe wengine wa mazungumzo hayo.
Mbeto amesema msingi wa mazungumzo hayo umejiegemeza katika kuzipitia suluhu hitilafu, dosari na kasoro mbambali za kisiasa na kisheria hatimaye ziweze kurekebishwa.
“Katika majadiliano hayo zitaangaliwa kasoro na dosari endapo ni za kisheria zitapelekwa katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kufanyiwa marekebisho ya kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
“Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar imepokea taarifa ya kuendelea kwa mazungumzo kati ya CCM na ACT Wazalendo, ajenda za mjadala huo bado ni siri. Hatma ya mazumgumzo hayo ikifikiwa itatangazwa na pande zote mbili,” amesema Mbeto
Amesema katika majadiliano ikiwa kutaonekana haja ya kubadili jambo husika kisheria, suala hilo litapelekwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
“Kwa mfano huwezi kuondosha kura ya mapema bila kubadili sheria yake,” amesema Mbeto.
Katibu huyo mwenezi amesema ni majadiliano yenye nia njema kwa mustakabali na ustawi wa Zanzibar na wananchi wake.
“Wajumbe washiriki kwenye mazungumzo hayo watarudisha mrejesho kwa chama kilichowatuma. Hatua nyingine za vikao vya juu vya chama chetu zitafuata na kutoa maamuzi yake,” amesema.
ACT – Wazalendo
Akizungumza hivi karibuni na viongozi na wanachama Unguja, Othman alisema tangu Novemba 8 hadi Februari 3, pande husika zimefanya jumla ya vikao sita kujadili namna ya kumaliza mkwamo wa kisiasa uliotokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Alisema kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, uongozi wa chama ulirejea kwenye Kamati Kuu na kupewa ridhaa pamoja na mipaka ya majadiliano, akieleza kuwa msimamo wao mkuu ni kushughulikia kilichoharibika katika mfumo wa uchaguzi.
“Mojawapo si kujadili nafasi ngapi za kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, bali kuangalia lipi limeharibika na tulitengeneze,” amesema.
Othman, alieleza kuwa kushiriki kwa chama chake katika uchaguzi huo na hatua walizochukua baadaye kumeweka wazi udhaifu uliopo katika mifumo ya nchi, akisisitiza umuhimu wa kujenga taasisi zenye uwajibikaji na kuheshimu Katiba.
“Haki ya nchi hii ni kuwa na viongozi waliochaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu. Kama kwenye nchi yako huna haki ya kuchagua wala kuchaguliwa, unakuwa sawa na uliye kwenye ukoloni,” alisema.
Othman aliongeza kuwa kuna ulazima wa kuendeleza mapambano ya kisheria na kisiasa ili kuhakikisha Zanzibar inapata utawala wa kisheria na kidemokrasia.
“Ni wajibu wetu kuendeleza mapambano ya kisheria na kisiasa kuhakikisha nchi yetu inajengwa juu ya misingi ya haki na utawala wa sheria,” alisisitiza.
Pia aliwakumbusha watumishi wa umma kutekeleza wajibu wao kwa kuwatumikia wananchi wote bila upendeleo wa kisiasa, akibainisha kuwa jukumu la Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mwananchi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa alisema mazungumzo hayo yanafanyika kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia maadili ya majadiliano.
“Lengo letu ni la muda mrefu. sio kila jambo linaweza kuzungumzwa hadharani kwa sasa, kutokana na kanuni na maadili ya mazungumzo,” alisema Jussa.
Mchambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar, Ali Makame amesema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwani kuna faida kubwa kuangalia masilahi ya chi badala ya vyama.
Amesema Zanzibar imeshuhudia vipindi vigumu vya siasa za mgawanyiko na kuleta athari kubwa na katika mazingira iliyokuwa imefikia hali hiyo ilikuwa kama inaondoka lakini kurejea huko sio taswira nzuri
“Hiki kilikuwa kikisubiriwa kwa muda sasa, inapotokea changamoto kukaa mezani ni jambo jema kupata suluhu ya pamoja na kusonga mbele, kwa sasa hatutaki kuona Zanzibar tena inarejea katika vipindi vyake huko nyuma,” amesema.
Historia ya miafaka Zanzibar
Zanzibar imepitia vipindi vya misukosuko ya kisiasa vilivyozaa mfululizo wa miafaka kati ya vyama vikuu vya siasa, hususan CCM na Civic United Front (CUF), na baadaye ACT Wazalendo.
Lengo kuu limekuwa kupunguza mvutano wa uchaguzi na kuimarisha utulivu wa kisiasa visiwani humo.
Mwafaka wa kwanza wa kisasa ulihusisha juhudi za Jumuiya ya Madola mwaka 1998, kufuatia mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa 1995.
Hatua hiyo ililenga kuanzisha mazungumzo rasmi kati ya pande hasimu na kutafuta suluhu ya kudumu ya mivutano ya kisiasa.
Mwaka 1999, CCM na CUF zilitia saini Mwafaka wa kwanza ulioweka msingi wa marekebisho ya mfumo wa uchaguzi, ukiwamo uimarishaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kuweka taratibu za kuongeza uwazi katika usimamizi wa chaguzi.
Hata hivyo, malalamiko yaliibuka tena baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2000, hali iliyosababisha kufikiwa kwa Mwafaka wa pili mwaka 2001.
Makubaliano hayo yalihusisha marekebisho ya kisheria na kiutawala yaliyolenga kuziba mianya iliyobainika katika chaguzi zilizopita.
Licha ya hatua hizo, mvutano wa kisiasa uliendelea hadi kufanyika kwa mazungumzo ya juu kati ya Rais wa Zanzibar wakati huo, Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad.
Mazungumzo hayo yalipelekea kura ya maoni ya mwaka 2010 iliyoidhinisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU).
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo, CCM na CUF ziliunda serikali ya pamoja, hatua iliyotajwa kupunguza kwa kiasi kikubwa mivutano ya kisiasa.
Hata hivyo, kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015 kulirejesha sintofahamu ya kisiasa.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, juhudi mpya za maridhiano zilifanyika chini ya Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, aliyefanya mazungumzo na Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa amehamia ACT Wazalendo.
Mazungumzo hayo yalizaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya mwaka 2020 kati ya CCM na ACT Wazalendo, ikiendeleza mkondo wa maridhiano kama njia ya kulinda amani, mshikamano na utulivu wa kisiasa Zanzibar.