Kigoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema endapo mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa soko la kisasa la Mwanga, Manispaa ya Kigoma Ujiji, atazembea, kitaielekeza Serikali iwakate fedha zao kwa mujibu wa sheria.
Chama hicho tawala kimesema wananchi wana ufahamu kuhusu mwenendo wa ujenzi wa soko hilo, hivyo lazima ukamilike ili wafanye biashara za kujiingizia kipato.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Februari 21, 2026 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi alipotembelea kukagua ujenzi wa soko hilo linalojengwa kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji Tanzania (Tactic).
Sababu za Kihongosi kueleza hayo ni hofu yake yaliyotokana na maelezo ya mkandarasi aliyemweleza kiongozi huyo kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati, lakini mwenezi huyo hajaona dalili hizo.
“Nimemuuliza mtu wa Serikali na mkandarasi na mmejidhatiti kuwa mtakamilisha kwa wakati, sasa endapo mtazembea tutaanza kuwakata,” amesisitiza Kihongosi.
Ujenzi wa soko la kisasa la Mwanga la Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Kihongosi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Simiyu, amesema uzoefu aliyonao maeneo mengi wakandarasi wanazembea hawamalizi kwa wakati miradi huku wananchi wakisubiri huduma.
“Watu hawataki kuona haya majengo wanataka kuingia ili kufanya biashara, hivyo lazima mradi ukamilike kwa wakati. Miradi hii ina tija kubwa sasa hatuwezi kucheka na wakandarasi ambao watataka kuongezewa muda,” ameeleza.
Kihongosi amemuelekeza mkandarasi huyo kuhakikisha anakamilika ujenzi huo kwa wakati kwa muda wa mwezi mmoja uliosalia kwa mujibu wa mkataba wake.
Haki itendeke
Katika hatua nyingine, Kihongosi ametaka haki itendeke baada ya mradi wa ujenzi wa soko hilo kukamilika, akiagiza waliokuwa wanafanyabiashara katika eneo kupata kipaumbele cha vizimba.
“Isotokee walikuwa wafanyabiashara hapa wanapoteza vibanda vyao. Watu wa chama na Serikali hatuna sababu ya kuja hapa, tuache watu wapewe kama vitabaki na sisi tutafuata utaratibu,” ameeleza Kihongosi.
Mmoja wa wafanyabiashara wa nafaka aliyekuwa katika eneo hilo, Oliver Gregory amesema Kihongosi amezungumza ukweli hivyo watu wa manispaa wakizingatia ushauri huo wataepuka migogoro.
“Tuliokuwa tunafanya shughuli hapa tupewe kipaumbele baada ya mradi kukamilika na si vinginevyo,” amesema Oliver.
Mratibu wa mradi huo, Eliazer Ndaisaba amesema uliofikia asilimia 63 una thamani ya zaidi ya Sh16 bilioni ukijumuisha masoko ya Mwanga na Katonga, ulianza kutekelezwa Desemba 30, 2026 na utakamilika Aprili 24, 2026.