
KOCHA Mkuu wa kikosi cha Azam FC, Florent Ibenge, anasema baada ya kumalizana na michuano ya kimataifa, kazi iliyosalia ni kuhakikisha timu hiyo haiachwi hata pointi moja na Simba na Yanga.
Azam ambayo ilikuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, wikiendi iliyopita ilitolewa na Waarabu wa Morocco, Wydad Casablanca, kwa mabao 2-0 ugenini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge anasema siku zote anajivunia sana wachezaji wake walivyocheza hizi mechi za makundi kwa ubora mkubwa, tena kwa mara ya kwanza.
Anasema kuwa walifanya makosa ya kutoshinda mechi mbili za kwanza na wamejifunza.
“Tumecheza vizuri, unaona kabisa Azam ya msimu uliopita siyo ya msimu huu kwani ina mabadiliko makubwa sana na ina matumaini pia.
“Sitaacha kuwapongeza wachezaji wangu, wamecheza kama vile wana uzoefu na hii michuano, tena hatua ngumu kama ile ya makundi, wameonyesha ukomavu na ubora mkubwa sana.”
MIPANGO NI SIMBA, YANGA
Ibenge anasema kuwa kwa sasa wanarudi kupigania mashindano ya ndani na malengo yao ni kuwa ndani ya timu tatu za juu.
“Malengo yetu ya juu ni kuwa ndani ya nafasi tatu za juu katika msimamo wa ligi, lakini pia ni kupunguza tofauti ya pointi kati yetu na Simba na Yanga walio juu yetu.
“Kwa sasa hatutakiwi kuwa na utofauti mkubwa wa pointi, labda ziwe nne, tofauti na msimu uliopita ambao zilikuwa pointi 15, ni nyingi sana. Azam haitakiwi kuwa na hali kama hiyo. Tunatakiwa kufanya kazi sana kutimiza malengo yetu haya.”
Mpaka sasa Simba, Yanga na Azam zote zimecheza mechi nane, lakini matajiri hao wa Chamazi wana pointi 16.
Simba ina pointi 18 katika nafasi ya saba, zikiongozwa na Yanga yenye pointi 22 inayoshika namba tatu katika msimamo, huku Azam ikiwa katika nafasi ya tisa, ikishinda na kupata sare mechi nne kila mmoja.