
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Marekani haijawahi kudai kusitishwa kabisa kwa urutubishaji wa urani katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea, huku akionya kuwa baadhi ya wenye misimamo mikali wanajaribu kuisukuma sera ya Marekani kuelekea katika “vita visivyo vya lazima na vya maafa.”
Abbas Araghchi alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Morning Joe cha kituo cha televisheni cha Marekani, MSNBC, siku ya Ijumaa.
Akirejelea duru ya hivi karibuni ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, yaliyofanyika Geneva siku ya Jumanne, Araghchi amesema mazungumzo hayo yamelenga kuhakikisha kuwa mpango wa nyuklia wa Iran, ikiwemo urutubishaji ,unabaki kuwa wa amani.
Ameielezea duru hiyo kuwa “nzuri sana,” akiongeza kuwa pande zote mbili zilikubaliana juu ya kanuni kadhaa za msingi zitakazoongoza mchakato wa mazungumzo.
Kwa mujibu wa Aragchi, Tehran itatayarisha rasimu ya makubaliano yanayowezekana ndani ya “siku mbili au tatu zijazo,” ambayo baada ya kuidhinishwa na mamlaka za juu, yatakabidhiwa kwa Steve Witkoff, mkuu wa ujumbe wa mazungumzo wa Marekani.
Araghchi pia amelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa vitisho vya kijeshi vya Marekani dhidi ya Iran katika wiki za hivi karibuni, licha ya kuendelea kwa mazungumzo ya kidiplomasia. Amesema: “Natumaini kwamba wale wanaotafuta vita, na wanaotaka kuikokota Marekani tena katika vita isiyo ya lazima na yenye madhara makubwa, hawatafanikiwa, na watawaruhusu wanadiplomasia kufanya kazi kwa pamoja ili kupata suluhisho la kidiplomasia ambalo naamini lipo ndani ya uwezo wetu na linaweza kufikiwa kwa muda mfupi.”
Kauli hizi zinajiri wakati ambapo ripoti zimewanukulu maafisa wa Marekani wakisema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiishinikiza Ikulu ya White House kumshawishi Rais Donald Trump kuidhinisha shambulio dhidi ya Iran.
Trump siku ya Alhamisi alikariri tena vitisho vyake vya hatua za kijeshi dhidi ya Tehran, siku chache tu baada ya mazungumzo ya Geneva, ambayo yalitathminiwa kwa ujumla kuwa na matokeo chanya.
Waziri Araghchi amesisitiza kuwa hatua za kijeshi haziwezi kamwe kutatua suala la nyuklia la Iran, akibainisha kuwa njia hiyo ilishajaribiwa wakati wa uchokozi wa Marekani na Israel mwezi Juni, na ikathibitika kuwa imeshindwa.
Aidha amesisitiza kuwa: “Hakuna suluhisho la kijeshi kwa mpango wa nyuklia wa Iran,” na kuongeza kuwa Iran iko tayari kwa amani na diplomasia, kama ambavyo iko tayari pia kujilinda pale inapolazimika.