Kigoma. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amehitimisha ziara yake ya siku tano mkoani Kigoma, akiacha gumzo baada ya kuishinikiza Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kumlipa papo hapo mkandarasi aliyekuwa akidai Sh620,000 tangu mwaka 2023.

Tukio hilo linafanana na lililowahi kutokea Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, ambako mkandarasi mmoja alidai zaidi ya Sh2.8 milioni kwa kazi ya ujenzi wa vyoo katika Shule ya Sekondari Gonja tangu mwaka 2022 bila kulipwa.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba baada ya kujiridhisha kwa kuwauliza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Same kuhusu deni hilo, alishangazwa na ucheleweshaji huo na kuagiza viongozi hao kuchangishana fedha papo hapo kulipa deni hilo.

Wilayani Kasulu

Moja ya matukio yaliyogusa hisia za wananchi katika mkutano

mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Nyamisundu wilayani Kasulu ni kilio cha mkandarasi, Joseph Wilbroad, aliyedai Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Sh620,000 zilizosalia baada ya kukamilisha ujenzi wa nyumba za walimu na bweni katika Shule za Sekondari Nyumbikwampya na Nyumbigwa.

Wilbroad alieleza kuwa tangu mwaka 2023 amekuwa akizungushwa bila kulipwa fedha zake, licha ya kutekeleza kazi aliyopewa.

“Tangu mwaka 2023 hadi leo napigwa danadana na halmashauri. Mimi nina familia, naomba unisaidie mwenezi,” alisema kwa masikitiko.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Kihongosi, alilitaja suala hilo kuwa ni uzembe wa wazi wa kiutendaji.

Alimtaka mkandarasi huyo kusimama mbele ya meza kuu, huku akiwaagiza wakuu wa idara, viongozi wa chama, wabunge, madiwani na mwenyekiti wa halmashauri kuchangishana fedha papo hapo ili kumaliza deni hilo.

“Haya ni mambo madogo sana, lakini kuna mtu amekaa mahali kazi yake ni kusaini, anaamua kupuuza. Sasa waipate dawa waone inavyouma,” alisema Kihongosi.

Dakika chache kabla ya kuhitimisha mkutano huo, Wilbroad aliitwa jukwaani na kukabidhiwa Sh620,000 zilizochangwa na watendaji hao, hatua iliyozua shangwe miongoni mwa wananchi waliohudhuria.

Pia, Kihongosi, amesisitiza kuwa hakwenda mkoani humo kwa kucheza bali kukagua na kufuatilia utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

Kutokana na hilo, Kihongosi amewataka watumishi wa umma kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na chama hicho tawala kuhusu utatuzi wa kero za wananchi wa mkoa wa Kigoma.

Kihongosi ametoa msimamo huo jana Ijumaa Februari 2026 akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Nyamisundu wilayani Kasulu katika mwendelezo wa ziara yake mkoani hapa.

“Niwaomba watumishi wa umma, haya maagizo ninayoyatoa yakatekelezwe sijaja Kigoma kucheza kabisa. Nimekuja hapa kufanya kazi na mimi mfuatiliaji kwelikweli, nitapiga simu,”.

“Asitokee mtu akasema limepita, halitafuatiliwa, tutakuja kukosana hapa.Chama kinapoagiza jambo lazima litekelezwe, wajibu ni kuona haki inatendeka, kila mtumishi atimize wajibu wake,” amesisitiza Kihongosi.

Katika mkutano huo licha ya na mvua za hapa na hapa, kunyesha lakini hazikuwazuia wananchi kuwasilisha kilio cha kero mbalimbali zilizojibiwa na kupatiwa ufumbuzi wa papo na Kihongosi.

Pia, Kihongozi amewahimiza wananchi wa Kasulu kutunza amani iliyopo na wasikubali kushawishika kuivuruga kwa maslahi ya watu wasioitakia mema Tanzania.

Amejenga hoja hiyo akirejea namna Mkoa wa Kigoma unavyohifadhi wakimbizi wanaotoka nchi za jirani kutokana na machafuko na kukimbilia Tanzania kwa sababu ni kisiwa cha amani.

“Msidanganywe na watu wasiwalaghai, mkaharibu amani ya hapa Kasulu, hakuna shida kubwa kama kutanga tanga kwenye nchi za watu. Sasa wasije watu wakawaeleza fanyeni vurugu au kufanya mambo mengine ya ovyo kataeni, lindeni amani ya hapa kwenu,”

“Tulinde utulivu na amani Kasulu, na wanasiasa wanaochochea vurugu wakaeni hadharani kwa sababu asilimia kubwa hawaishi hapa Kasulu wala hamuajui.Sasa usiende kucheze ngoma msioijua wimbo wake,” ameeleza Kihongosi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *